Follow us: Subscribe via RSS Feed Connect on YouTube Connect on YouTube
Maganga One Blog kwa habari za kitaifa,kimataifa,burudani na michezo kila siku. Tutumie habari na matukio yoyote kwa email yetu ya magangaone@gmail.com

Jul 12, 2016

Polisi yanasa meno 666 ya tembo nchini

JESHI la Polisi Tanzania kwa kushirikiana na Polisi wa Interpol, wameendesha oparesheni na kukamata vipande 666 vya meno ya tembo, ambavyo ni kilo 1,279.19 vyenye thamani ya Sh bilioni 4.6.
Pia limewatia nguvuni watuhumiwa tisa, wakiwamo raia wawili wa Guinea na mmoja wa Uganda. Meno hayo yalikamatwa kabla ya kufanyika kwa oparesheni kati ya Jeshi la Polisi, wakishirikiana na ofisi za Interpol Kanda ya Kusini zilizopo Harare nchini Zimbabwe na ofisi za Interpol Kanda ya Afrika Mashariki zilizopo Nairobi nchini Kenya.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Diwani Athuman alisema ukamataji huo, ulitokana na taarifa za kiintelijensia zilizokusanywa wakati wa matayarisho ya oparesheni Usalama III.
Alisema kulingana na hali halisi, ilibidi timu ya maofisa wa Kikosi Kazi, wayakamate siku nne kabla ya tarehe ya oparesheni, kuepuka watuhumiwa kutoroka na kutorosha meno hayo.
Alisema oparesheni hiyo iliyopewa jina la Oparesheni Usalama III, ilifanyika Juni 29 na 30, mwaka huu kwa nchi nzima na ilishirikisha pia taasisi na idara za serikali.
Alisema jumla ya nchi 26 zilishiriki kufanya oparesheni hiyo kwa pamoja na wakati mmoja.
DCI Athumani alisema oparesheni hiyo, imekuwa na mafanikio makubwa kwani wamekamata vielelezo na watuhumiwa 265 kwa makosa mbalimbali, yaliyopewa kipaumbele na hata yale ambayo hayakupewa kipaumbele, kukamata wahamiaji haramu 43 ambao ni Wakongo 18, 22 kutoka Burundi, wawili wa Rwanda na mmoja wa Kenya.
Aliongeza kuwa walikamata dawa mbalimbali za kulevya ikiwemo heroin gramu 83, bangi kilo 398.6, mirungi kilo 30 na silaha haramu ambazo ni bunduki aina ya shotgun moja, magobori 11, risasi 104, mkuki mmoja na vipande 15 aina ya exprojel v6 na milipuko.
Aidha, DCI Athumani alisema katika oparesheni hiyo, walikagua magari 1,632 na kati ya magari hayo 10 yaliripotiwa kuibwa na matano yaligunduliwa kubadilishwa chassis.
Alisema magari hayo yaliibwa kutoka Afrika Kusini magari matatu, Uingereza magari matano, Malaysia magari mawili na magari mengine matano yanafanyiwa uchunguzi.
Alisema katika oparesheni hiyo, walifanya ukaguzi katika kampuni mbalimbali zinazofanya biashara ya madini ambapo kampuni tatu zilionekana kukosa uhalali wa kupewa leseni ya kuendelea kufanya biashara ya madini, na pia walikamata madini aina ya Acquamiline Smoky Quatz kilo 20.
Alitaja kampuni hizo ni Delicore Metal Company Ltd, Madandwa Gold Mining Export Import Ltd na Adex Mining Co. Ltd na tatizo lao linaendelea kushughulikiwa na Wizara ya Nishati na Madini. Pia walikamata jumla ya lita 960 za gongo na mitambo 18 ya kutengenezea gongo na bidhaa bandia mbalimbali, zikiwemo manukato na mafuta ya nywele.
“Pamoja na mafanikio yaliyopatikana katika oparesheni hii, Jeshi la Polisi litaendelea kufanya misako mara kwa mara ili kupunguza uhalifu nchini, tunawaomba wananchi muendelee kutoa ushirikiano wao katika harakati za kupambana na uhalifu wa aina yoyote hapa nchini,” alisema DCI Athuman.

Share this article :

0 Maoni:

 
Maganga One Blog © Copyright 2017. All Rights Reserved.

Powered by Maganga One.
Back to TOP