Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwapungia mkono wakazi wa Igunga mkoani Tabora mara baada ya kuwahutubia Wilayani hapo.  

Mke wa Rais Mama Janeth Magufuli akiwasalimia wakazi wa Misigiri Mkoani Singida. PICHA NA IKULU
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe  30 Julai, 2016 ameendelea na ziara yake katika Mkoa wa Tabora akitokea Mkoa wa Singida.

Kabla ya kuingia Mkoani Tabora, Rais Magufuli
amezungumza na wananchi wa Mji wa Misigiri katika Wilaya ya Iramba
ambapo amemuagiza Meneja wa Wakala wa Barabara katika Mkoa wa Singida
kuhakikisha mkandarasi anayejenga daraja la Sibiti anarejea kazini mara
moja kukamilisha ujenzi wa daraja hilo.

Rais Magufuli amesema
serikali yake imejipanga kumlipa fedha mkandarasi huyo na hivyo hakuna
sababu ya kuendelea kusimamisha ujenzi huo.Mkoani Tabora, Rais Magufuli
amezungumza na wananchi waliosimamisha msafara wake katika vijiji vya
Nanga na Ziba na amefanya mikutano ya hadhara katika miji ya Igunga na
Nzega ambako amewahakikishia wananchi kuwa serikali yake itahakikisha
inatekeleza ahadi zilizopo katika Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya Mwaka 2015.

Katika
mkutano wa hadhara uliofanyika Igunga, Rais Magufuli amepokea
malalamiko ya wananchi kuhusu kutoanza kutumika kwa kituo cha mabasi na
soko na amewaagiza viongozi wa Mkoa wa Tabora kuhakikisha kituo cha
mabasi cha Igunga na soko la Igunga vinaanza kutumika kuanzia Jumatatu
ijayo ya tarehe 01 Agosti, 2016.

Kuhusu kero ya maji, Dkt.
Magufuli amesema Tanzania imepata mkopo wa dola za kimarekani Milioni
268.35 kutoka nchini India ambazo zitatumika kutekeleza mradi wa
kusambaza maji ya ziwa Viktoria katika Miji ya Tabora, Igunga, Nzega,
Sikonge na Uyui pamoja na vijiji vilivyopo kandokando mwa bomba kuu
kuanzia mwaka huu ambapo watu milioni moja na laki moja (1,100,000)
watanufaika.

Dkt. Magufuli ameongeza kuwa pamoja na juhudi hizo
Serikali imefanya usanifu na upembuzi yakinifu kwa ajili ya kutekeleza
mradi wa kusambaza maji ya kutoka mto Malagarasi kwa ajili ya Miji ya
Urambo, Kaliua na Nguruka pamoja na vijiji vilivyopo kandokando mwa
bomba kuu ambako watu laki sita (600,000) watanufaika.

Aidha, Rais Magufuli amepiga marufuku wakulima wadogo kutozwa ushuru wa mazao watokapo na mazao mashambani.


"Ninapenda tukusanye kodi, lakini sio kukusanya kodi kutoka kwa watu
masikini, mtu ametoka shambani na magunia yake mawili au hata matano
halafu nyinyi mnamtoza kodi."Mimi sipendi kuwanyanyasa hawa watu
wanyonge, mtu akiwa na mazao lori zima hapo sawa lakini sio kwa mtu
mnyonge mwenye gunia moja" Amesema Rais Magufuli.



Kuhusu
maombi ya Mkoa wa Tabora kutaka kuanzishwa Mkoa mwingine kutokana na
ukubwa wa baadhi ya Wilaya Rais Magufuli amesema haioni umuhimu wa
kuanzisha Mikoa mipya hapa nchini kwa sasa, na badala yake fedha
zitaelekezwa katika huduma kwa wananchi kama vile maji, barabara,
miundombinu na huduma za afya.

Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Nzega
30 Julai, 2016