Rwanda imeanza kutekeleza uamuzi wa kuongeza ushuru unaotozwa nguo za mitumba zinazoagizwa kutoka nje.
Uamuzi huo ulichukuliwa na nchi za jumuiya ya afrika mashariki japo baadhi ya nchi zilijipatia muda ili kujitayarisha zaidi kuingia katika mfumo huo mpya wa kutumia nguo zinazotengenezwa na viwanda vya nguo vya ndani.
Viongozi wa Rwanda wamekuwa katika kampeni kabambe ya kutaka wananchi kutumia bidhaa zinazotengezwa nyumbani, licha ya kwamba nchi hiyo ina kiwanda kimoja tu cha kutengeneza nguo.
Kulingana na serikali,nguo za mitumba zimeanza kutozwa ushuru wa dollar 2,5 toka dollar 0,5 kwa kilogramu moja ilhali ushuru kwa viatu vya mitumba umepanda toka dollar 0,2 hadi dollar 5 za Marekani.

Image captionWafanyabiashara wa nguo kuukuu Kigali

Katika soko la Biryogo, mjini Kigali ,wachuuzi wa nguo za mitumba wamekata tamaa kutokana na uwamuzi huo.
Baadhi wameiambia BBC kuwa kazi hiyo sasa haina faida yoyote tena.
‘’ni kama tumevunjwa nguvu.tulikuwa tunaishi kutokana na hii kazi,lakini kutokana na kupanda kwa ushuru ni kama hatuna kazi tena. Pesa ni nyingi,huwezi kupata pesa za kulangua na nyingine za kutoa ushuru.

Image captionRwanda Mitumba

Bora kuhamia katika nchi nyingine isiyokuwa hii”mmoja amesema.
Mwingine amesema:’’tangu utotoni nilifanya kazi ya kuuza nguo za mitumba,lakini sasa inavurugika,sijui kama tutakuwa wakulima au?”
Rwanda ina wakazi takribani milioni 12 . ina kiwanda kimoja tu cha kutengeneza nguo na haina viwanda viwanda vya viatu.
Kuna wanaoona kuwa uamuzi huu umetekelezwa haraka bila hata nchi yenyewe kujipa muda wa kujipanga sawa sawa:

Image captionViatu vinavyouzwa Kigali

“Rwanda kuna kiwanda kimoja tu cha kutengeneza nguo .wewe fikiria nchi yenye watu milioni 12 kwa kiwanda ambacho hata uwezo wake unatiliwa shaka.''
''Ingekuwa vizuri watuonyeshe namna tutakavyopata nguo au hata wakubali kuwepo ushindani baina ya nguo za mitumba na hizo nguo zinazopigiwa debe,ili wananchi wenyewe wachague nguo gani za kuvaa''
Serikali imekuwa katika kampeni kabambe ya kupigia debe matumizi ya bidhaa zinazotengenezwa na viwanda vya ndani ikisema uagizwaji wa bidhaa za mitumba kama nguo na viatu unagharimu nchi dolla za Marekani milioni 15 kila mwaka.