|
MAKAMU wa Rais, Samia Hassan Suluhu, amezitaka nchi za Afrika kuunganisha nguvu kudhibiti uhalifu ukiwemo ugaidi, utekaji nyara, biashara haramu ya binadamu na dawa za kulevya.
Samia alisema hivyo juzi, baada ya kuwatunuku watendaji mbalimbali katika sekta ya ulinzi kutoka nchi za Afrika, waliopata Stashahada na Shahada ya Uzamili katika Usalama na Strategia kutoka Chuo cha Ulinzi wa Taifa (NDC).
Akitunuku shahada hizo, alisema ushirikiano katika masuala ya usalama unazidi kukua kwa nchi rafiki na Tanzania, baada ya watendaji wa masuala hayo kupata elimu katika chuo hicho cha taifa.
Alisema, watendaji kutoka nchi za Botswana, Burundi, Kenya, Malawi, Namibia, Nigeria, Afrika Kusini, Zambia, Zimbambwe na China wamejumuika katika kupata mafunzo kutoka chuo hicho jambo linaloonesha kuendelea kukuza ushirikiano.
“Tunaweza na lazima kufanya kazi kwa pamoja ili kujenga nguvu na umoja dhidi ya wahalifu katika nyanja zote na si ushirikiano katika silaha pekee, lakini pia kwa kutumia akili zetu kuweka mikakati ya kukabiliana nao,” alisema Samia.
Alieleza kuwa kwa kuhakikisha nchi hizo zinafanya kazi pamoja ni vyema pia kutumia busara kwani kuwepo mataifa mbalimbali katika kumaliza shahada hiyo ya usalama ni ishara tosha kuwa vitendo vya uhalifu na ugaidi inahitaji ushirikiano kutoka kwa nchi zote jirani.
Pia aliwataka wahitimu hao kutoka nchi mbalimbali kuhakikisha elimu waliyopata inawasaidia katika kufanikisha kuhakikisha nchi hizo zinafanya kazi kwa pamoja huku wakiwa mabalozi wa chuo hicho katika nchi zao.
Akizungumza katika mahafali hayo, Mkuu wa Chuo cha NDC, Meja Jenerali Yakub Mohamed, alisema katika mahafali hayo wanafunzi 39 waliohitimu masomo, 22 walipata Shahada ya Uzamili na 17 Stashahada ya Usalama na Strategia.
0 Comments