Mbunge wa Kaliua, Magdalena Sakaya
MBUNGE wa Kaliua mkoani Tabora, Magdalena Sakaya (Cuf), amewaomba wananchi kutoa ushirikiano kwa vyombo vya usalama ili kukomesha mauaji yanayoendelea wilayani humo.
Sakaya alitoa kauli hiyo kwenye mkutano wa hadhara wakati akizungumza na wananchi wa kijiji cha Usangi, kata ya Igwisi, wilayani Kaliua.

Alisema mauaji hayo yamekuwa yakimnyima usingizi kwani yanakithiri kila uchao hali ambayo inahitaji kuangaliwa kwa ukaribu na serikali.
Aidha, alisema amekuwa akipokea taarifa za mara kwa mara za watu kuuana kinyama kwa sababu mbalimbali na kueleza kuwa, wananchi wanapaswa kutoa ushirikiano kwa vyombo vya dola na serikali kuongeza ulinzi kwa wananchi wake.
Sakaya alisema baadhi ya sababu za mauaji hayo alielezwa kuwa ni visasi, kufumaniwa, mali, mashamba, vurugu za wafugaji na baadhi ya askari wa Maliasili.
Aidha, alisema hata katika vilabu vya pombe, minada, wakulima waliouza mazao na tumbaku na hata katika mchezo wa Pool, mauaji yametokea.
Alitolea mfano wa mauaji ya hivi karibuni ya kijana kumpiga mwenziwe na fimbo ya mchezo huo (pool table) na kusababisha kifo chake. Sakaya alidai pia kuwa, vipo vitisho vinatolewa kwa viongozi wa kisiasa na kueleza kuwa mambo hayo hayapaswi kufumbiwa macho na wenye dhamana ya usalama wa raia na mali zao.
Alisema ana ushahidi wa kiongozi mmoja wa ngazi ya Kata ya Igwisi na kundi lake kumtishia kumuua Mwenyekiti wa Kitongoji cha Upele, Madiseni Selina.
Alisema kiongozi yupo kwa ajili ya wananchi wote bila kujali itikadi cha vyama na hapaswi kuwa sababu ya vitisho kwa namna yoyote na kwa mtu yeyote.
Pia, alikemea baadhi ya watu katika kikosi cha ulinzi cha Sungusungu katika maeneo ya Kaliua kujichukulia sheria mkononi ya kukamata watu ovyo na wakati mwingine kuwajeruhi kwani inaondoa sifa ya Sungusungu kama jeshi la kulinda amani vijijini.
Siku chache zilizopita, Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri, alimuaagiza Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo, Khamis Issa, kukomesha mauaji ya kinyama yanayoendelea katika maeneo mbalimbali wilayani humo.