USHIRIKIANO imara kati ya Tanzania na Rwanda, umeanza kuzaa matunda ambapo jana Rais John Magufuli aligusia sehemu ya matokeo ya ushirikiano huo kwamba ni pamoja na mbinu za kufufua na kuimarisha Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL).

Akizungumza Ikulu Dar es Salaam jana, baada ya mawaziri wawili wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ya Rwanda na Tanzania kutia saini mkataba wa makubaliano ya ushirikiano baina ya nchi hizo mbili, Rais Magufuli aligusia matunda ya urafiki wa nchi hizo.
Alisema nchi hizo mbili ni marafiki wa kihistoria na kwa kuonesha mshikamano wao, Rwanda imempa mbinu za kufufua ATCL, ambapo wataalamu wa Rwanda kupitia shirika lao la RwandAir, watasaidia harakati za kufufua ATCL.
“Nimepata tunaita ‘Desa’ kutoka kwa rafiki yangu Kagame (Paul, Rais wa Rwanda), wenzetu wa RwandAir wametupa mbinu za kufufua ATCL na tunaenda vizuri na ifikapo Septemba mwaka huu tutakuwa tumepata ndege zetu mbili aina ya Bombardier na tutaendelea hadi kwenye Boeing,” alisema Magufuli.
Alisema juhudi hizo ni matokeo ya ushirikiano mzuri uliopo baina ya nchi hizo na kwamba lengo ni kuhakikisha nchi hizo zinakua kiuchumi na kutimiza malengo endelevu pamoja na azma ya Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati ifikapo 2025.
Miezi michache iliyopita, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alipokuwa akiwasilisha Mpango wa Maendeleo wa Taifa katika kikao cha Bunge, alitaja vipaumbele vya serikali katika kuhakikisha nchi inakua kiuchumi kuwa ni pamoja na kufufua ATCL kwa kununua ndege hizo mbili.
Alisema ndege hizo aina ya Bombardier Q 400 ni kwa ajili ya kufufua safari za ndani za shirika hilo na mipango yake pia ni kununua ndege nyingine aina ya Boeing kwa ajili ya kuboresha safari za nje.
Wataalamu wa kodi
Katika hatua nyingine, Rais Magufuli alisema katika kuhakikisha nchi inakusanya mapato yake na kuepukana na udanganyifu na wizi, wataalamu wa Rwanda kwenye masuala ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), watasaidia pia eneo hilo ili kuhakikisha nchi inakuwa na kituo kimoja cha kukusanya mapato yake.
Alisema kituo hicho kitakuwa chini ya Serikali Mtandao (e-government), ambao wataratibu fedha zote zinazoingia badala ya utaratibu wa sasa wa kila taasisi kutumia mfumo wake wa ukusanyaji kodi.
“Tutapewa pia wataalamu watakaosaidiana na wa kwetu ili kuhakikisha makusanyo ya mapato yote ya serikali yanakuwa chini ya mfumo mmoja unaoangaliwa na serikali mtandao, lengo ni kuziba mianya ya wizi na ubadhirifu, kwa kuwa hivi sasa kila taasisi inakusanya fedha kwa kutumia mfumo wake ambao serikali haina mawasiliano ya kubaini kilichoingia,” alisema Rais Magufuli.
Kwa upande wake Rais Kagame wa Rwanda alisema uhusiano wa nchi hizo ni mzuri na wako tayari kuendeleza ushirikiano huo, ili kunufaisha nchi hizo na watu wake kwa kufungua milango ya biashara.
Katika hatua nyingine, Rais Kagame alifungua Maonesho ya 40 ya Biashara ya Kimataifa, ambayo yamehudhuriwa na nchi zaidi ya 30, Kampuni 650 na wajarisiamali tofauti zaidi ya 2,000 kutoka ndani na nje ya nchi.
Katika maonesho hayo, Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), imeibuka mshindi wa jumla hatua iliyotokana na mamlaka hiyo kuwa na mbinu nyingi za ubunifu wa mafunzo mbalimbali yenye tija kwa wananchi hususan vijana.