UJENZI wa Reli ya Kati kwa kiwango cha kisasa cha standard gauge, unatarajiwa kuanza kwa vipande vipande na wakandarasi tofauti; mmoja kutoka Dar es Salaam kwenda Kigali na mwingine kutoka Kigali kwenda Dar es Salaam, ili kuharakisha ukamilishaji wake.

Rais John Magufuli alisema hayo alipokuwa akimkaribisha mgeni wake, Rais Paul Kagame wa Rwanda, Ikulu, Dar es Salaam jana na kuagiza Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa akutane na Waziri wa Ujenzi wa Rwanda, kujadili utekelezaji huo.
“Sisi tumetenga Sh trilioni moja kuanza ujenzi wa reli hii na tunataka tujenge vipande vipande, mawaziri wa nchi hizi wa Ujenzi watakaa waangalie utekelezaji wake, ili wengine waanze kujenga Kigali na wengine waanze Dar es Salaam,” alisema Rais Magufuli.
Reli hiyo inahusisha njia kutoka Dar es Salaam mpaka Kigoma, Tabora-Mwanza, Kaliua-Mpanda, Kalema-Uvinza na Gitega-Msongati nchini Burundi na Isaka-Rusumo hadi Kigali, Rwanda.
Rais Magufuli alisema ujenzi wa reli hiyo ni kichocheo muhimu cha maendeleo baina ya nchi hizo mbili na kwamba mara baada ya ujenzi wake kukamilika, reli hiyo itaimarisha biashara na kukuza uchumi.
Alisema nchi za Afrika Mashariki na nchi nyingine jirani, zinategemea Bandari ya Dar es Salaam kupitishia mizigo yao na kama ujenzi wa reli hiyo utakamilika na kuanza kazi, utarahisisha uchukuzi wa mizigo kutoka bandarini kwenda katika nchi hizo.
Rais Magufuli alisema hivi sasa asilimia 70 ya bidhaa ziendazo Rwanda zinapitia Bandari ya Dar es Salaam na mizigo hiyo imekuwa ikitumia muda mrefu kufika nchini Rwanda, kutokana na uwepo wa vizuizi vingi barabarani, lakini uwepo wa reli utapunguza tatizo hilo na kufanya mizigo kubebwa kwa ujazo mkubwa kwa mara moja.
Hata hivyo, alisema wakati ujenzi wa reli hiyo ukiwa mbioni kuanza, Serikali ya Tanzania imepunguza vizuizi hadi kufikia vitatu na ili kujenga ushirikiano mzuri na Rwanda, Tanzania imetoa eneo la kujengwa Bandari Kavu (ICD) kwa ajili ya mizigo ya nchi hiyo, wakati ikisubiri kusafirishwa.
Aidha, Rais Magufuli alisema Mamlaka ya Bandari imefungua ofisi jijini Kigali ili kurahisisha utoaji wa nyaraka na kupunguza gharama kwa wafanyabiashara wanaotumia bandari ya Dar es Salaam.
Alisema uchumi wa nchi hizo unaweza kukua kwa kasi iwapo msukumo wa dhati utajengwa ndani yao na hatua hiyo imeanza na mfano mzuri ni Ujenzi wa Daraja la Rusumo lililoko mpakani mwa Tanzania na Rwanda.
Kupitia daraja hilo, Rais Magufuli alisema baada ya kuanza kutumika, makusanyo ya mapato yameongezeka zaidi ya mara 100 ukilinganisha na awali na hiyo ni fursa moja na nyingine nyingi zinafunguliwa kwa lengo la kukuza uchumi wa mataifa hayo.
Kwa unade wake Rais Kagame alisema Rusumo ni mfano mzuri wa kiunganisho cha mataifa hayo na kwamba ni vyema nchi hizo zikatilia msukumo zaidi kwenye kukuza biashara na kutumia fursa zilizopo.
Haya hivyo alishauri ni vyema wananchi wa nchi hizo wakathamini bidhaa zinazozalishwa katika nchi hizo na kununua na kushauri uwepo wa ushirikiano baina ya sekta binafsi na umma katika kukuza biashara na uchumi.
“Tanzania mmebarikiwa kuwa na rasilimali nyingi na watu wenye vipaji, vinavyoweza kuiletea nchi maendeleo ni vyema mkavitumia vizuri na pia tuhakikishe tunakuza biashara kwa faida ya nchi zetu na watu wake,”alisema Kagame.