|
SIKU nne baada ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kutamka kuwa atahamia Dodoma Septemba mwaka huu, wizara zote za serikali zimetuma maombi kwa ajili ya kuoneshwa maeneo watakapojenga ofisi zao.
Katika hatua nyingine, sekta binafsi mkoani Dodoma imejigamba kujipanga vizuri kuhakikisha inatumia fursa ya masoko kujiimarisha kibiashara kutokana na matarajio ya Makao Makuu kuingiza wabia wengi wa kibiashara kutoka ndani na nje ya nchi.
Katika mahojiano na waandishi wa habari jana, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA), Pascas Muragili alisema katika harakati za serikali kuhamia Dodoma mamlaka hiyo imepokea barua za maombi ya wizara zote wakitaka kuoneshwa maeneo yao.
Barua za Wizara Muragili alisema hayo yanafanyika ikiwa ni mwitikio wa kauli ya Rais John Magufuli ya serikali kuhamia mkoani Dodoma, sambamba na Waziri Mkuu Majaliwa kuitaka mamlaka hiyo kuhakikisha wanatenga maeneo mbalimbali kwa ajili ya kuifanya Dodoma kuwa Makao Makuu.
“CDA imeshapokea maombi kutoka wizara zote za serikali zikitaka kuoneshwa maeneo yao na kazi ambayo tunaifanya kwa sasa ni kushughulikia barua hizo na kuweza kujua jinsi gani tunazipanga kulingana na wizara hizo,” alisema.
Alisema kuwa kwa sasa hawawezi kuanza na ujenzi wa Makao Makuu kwa maana kuwa serikali itahamia mara moja, badala yake watahakikisha katika mpango wa muda mrefu kila wizara itajenga ofisi zake kwenye eneo la mji wa serikali.
“Ikumbukwe Siku ya Mashujaa Waziri Mkuu (Majaliwa) alitoa ufafanuzi na kuweka wazi kuwa kila wizara inapokuja kwenye vikao vyake vya Bunge ina sehemu za kufikia kwa hiyo serikali imeamua kwa kuanzia itaanza na ofisi ambayo wizara zilikuwa zikitumia kwa kipindi cha vikao vya Bunge,” alisema Muragili.
Alisema Mamlaka hiyo inao mpango kabambe wa kuhakikisha Mji wa Dodoma unakuwa katika mpangilio mzuri na usiokuwa na msongamano. Alisema katika mpango huo zipo barabara za kutosha ambazo kwa sasa hazionekani kwa macho.
“Tunayo Master Plan ambayo imeshaainisha barabara zote, kwa hiyo barabara ni nyingi mno, kwani kila mtaa utakuwa unapitika kirahisi kutokana na mji kupangwa vizuri,” alisema Muragili.
Akizungumzia kasi ya upimaji wa viwanja alisema mamlaka yake imejipanga na ina timu ya kutosha kwa ajili ya kufanya kazi hiyo.
Aliyataja baadhi ya maeneo ambayo yana viwanja kuwa ni eneo la Mkalama na Miganga ambayo yapo nje kidogo ya Mji wa Dodoma huku akisema, kutokana na ujio Makao Makuu, upo uwezekano mkubwa wa maeneo hayo kugawiwa kwa wahitaji na kumalizika ndani ya wiki moja kutokana na wananchi wengi kujitokeza kutuma maombi ya viwanja.
Aliwatahadharisha wananchi kuacha tabia ya kununua viwanja kupitia kwa madalali kwani wakifanya hivyo watahesabiwa wamevamia maeneo kutokana na kutofuata taratibu zilizowekwa za ugawaji wa maeneo.
Sekta binafsi Katika hatua nyingine, sekta binafsi mkoani humo imesema imejipanga kuhakikisha inatumia fursa ya masoko kujiimarisha kibiashara kwani ujio wa Makao Makuu utawaingiza wabia wengi kutoka ndani na nje ya nchi.
Mwenyekiti mwenza wa Baraza la Biashara Mkoa wa Dodoma, Ringo Iringo alisema sekta binafsi imejipanga kufanya biashara kwani ujio wa Makao Makuu utakuwa na msururu wa taasisi za fedha na hivyo kuongeza fursa za upatikanaji wa mikopo kwa wafanyabiashara.
Iringo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Umoja wa Wasindika Mafuta ya Alizeti alisema hata fursa kwenye kilimo zitaongezeka kwani viwanda vitakavyojengwa vitahitaji zaidi malighafi ili kukidhi uzalishaji. Aliwataka wakazi wa Dodoma kuanza kutumia nafasi hiyo kujiimarisha kibiashara ili wasibaki nyuma kwani ushindani lazima uwepo.
Mmoja wa wajasiriamali wa Mkoa wa Dodoma, Regina Joram alisema kuna haja ya kutolewa kwa elimu ili wananchi wengi wafaidi fursa za uwepo wa Makao Makuu. Mwenyekiti wa Wafanyabiashara Ndogondogo Mkoa wa Dodoma, Norbert Pangasero alisema ujio huo usiwaache mbali wafanyabiashara ndogo bali watengewe maeneo kwa ajili ya kufanya biashara.
0 Comments