Rais John Magufuli akihutubia wananchi wa Katoro na Buseresere mkoani Geita jana.(Picha na Ikulu).
RAIS John Magufuli amewaagiza viongozi wote wa kuanzia ngazi ya mkoa hadi kitongoji nchini, kufuatilia matumizi ya fedha zinazotolewa na Serikali kwa ajili ya kutoa elimu bila malipo kwa lengo la kudhibiti mianya ya matumizi mabaya ya fedha hizo.
Rais Magufuli alitoa maagizo hayo jana katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Mnadani na kuwajumuisha wananchi wa Katoro na Buseresere mkoani Geita.

Katika agizo hilo, Rais Magufuli aliwaonya walimu ambao wameanza kufanya udanganyifu kwa kuandikisha idadi kubwa ya wanafunzi kuliko idadi halisi, kwa lengo la kupata mgawo mkubwa wa fedha za ruzuku. Alisema Serikali itachukua hatua kali dhidi ya yeyote atakayebainika kufanya hivyo.
“Ninafahamu mgawo wa fedha hizo hutolewa kulingana na idadi ya wanafunzi waliopo, wapo baadhi ya walimu ambao wameanza kuandika wanafunzi hewa katika shule zao, ili kusudi aletewe hela nyingi kuliko idadi ya wanafunzi waliopo. “Wanafunzi kama wapo laki nne yeye anasema shule yangu hii ina wanafunzi laki tano, ili kusudi hela zikija za wanafunzi laki tano, za wanafunzi laki moja wagawane. “Napenda nitoe wito kwa walimu Tanzania nzima, mnatafuta matatizo, narudia mnatafuta matatizo, msijaribu kula hela ya Serikali,” alisema Rais Magufuli.
Pamoja na agizo hilo, alitaka viongozi wa ngazi zote katika mikoa, kuhakikisha wana takwimu za idadi ya wanafunzi katika shule zote zilizopo katika maeneo yao ili kurahisisha ufuatiliaji wa fedha hizo.
Alisema kuwa kuanzia sasa, ataanza kutembelea shule kwa kushitukiza na kwamba kiongozi atakayeonekana kutojua takwimu, itakuwa ni uthibitisho kuwa hatoshi kuendelea na wadhifa alionao.
“Na nitoe wito kwa viongozi wa mikoa, mkuu wa mkoa, wakuu wa wilaya, wakurugenzi, makatibu tarafa, watendaji wa kata, wenyeviti wa vijiji, kila mmoja awe na idadi ya wanafunzi waliopo katika shule zao, hatutaki kuwapunja wanafunzi hela ambayo wanatakiwa kupata, lakini pia hatutaki kutoa hela ambayo haitakiwi,” alisisitiza Rais Magufuli.
Rais Magufuli ambaye alitumia mkutano huo kueleza juhudi mbalimbali zilizofanywa na Serikali yake ya Awamu ya Tano, kutekeleza ahadi yake ya kujenga Tanzania Mpya, pia aliwataka viongozi na watendaji wa Serikali kutekeleza wajibu wao kwa kutembelea wananchi wanaowaongoza badala ya kukaa muda mwingi ofisini huku akisisitiza ofisi hizo kuwepo katika maeneo yenye shughuli husika.
Aidha, alikosoa utaratibu unaotumiwa na halmashauri nyingi za majiji, manispaa, miji na wilaya, kutumia mawakala katika ukusanyaji wa mapato ya halmashauri, akisema mawakala hao wamekuwa wakitumia utaratibu huo, kukusanya fedha nyingi na kisha kuwasilisha kiasi kidogo katika halmashauri husika.