Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo
WAZIRI wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo amebainisha mikakati ya serikali ya kuwekeza takribani dola bilioni 30 (Sh trilioni 63) kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda cha kuchakata gesi kitakachojengwa mkoani Lindi.
Muhongo aliyasema hayo jana kwenye viwanja vya Maonesho ya Kilimo ya Nanenane ya Ngongo, Lindi mara baada ya kumaliza kusoma hotuba ya Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan ya ufunguzi wa maonesho hayo.

Alisema wananchi wa Lindi na Tanzania kwa ujumla wajiandae kwa mapinduzi makubwa ya uchumi katika miaka michache ijayo baada ya serikali kufanya uwekezaji wa kihistoria kama ilivyokuwa wakati Rais wa Kwanza Mwalimu Julius Nyerere alipojenga Reli ya Tazara kwa ushirikiano na mwenzake wa Zambia, Kenneth Kaunda.
“Nataka kuwahakikishia wananchi wa Lindi na Tanzania kwa ujumla kuwa uchumi wetu utakuwa kwa kasi kubwa, tunakwenda kuwekeza kiwanda cha kuchakata gesi ambacho uwekezaji wake hautapungua dola za Marekani bilioni 30. “Kiwanda hiki kitajengwa hapa Lindi na eneo tayari limeshapatikana, hivyo mtegemee mabadiliko makubwa maana sasa Lindi na Mtwara mtabeba uchumi wa nchi hii,” alisema Waziri Muhongo na kuwataka wananchi kuwa watulivu wakati wa utekelezaji wa mradi huo.
Alisema mradi huo unatarajia kuchukua muda mrefu wa wastani wa miezi 40 kwa sababu unahitaji uwekezaji mkubwa wa fedha, ujuzi na uzoefu sambamba na usimamizi wake. Muhongo alisema katika utekelezaji wake, serikali itajenga bomba la kusafirisha gesi lenye urefu wa kilomita 200 kutoka baharini hadi kwenye kiwanda.
“Hii si kazi rahisi, itachukua muda mrefu kwani tunatakiwa kutoa gesi baharini umbali wa kati ya kilomita 100 hadi 200, hadi kiwandani ambako gesi itachakatwa na kuwa kama uji. Akizungumzia uwekezaji mwingine wa kiwanda cha mbolea kitakachojengwa Kilwa, Waziri Muhongo alisema ujenzi huo utagharimu dola za Marekani bilioni 1.9 (Sh trilioni 4) mpaka kumalizika kwake.
Alisema kiwanda hicho kinatarajia kuzalisha mbolea tani 3,850 kwa siku na kutoa ajira za moja kwa moja kwa Watanzania zaidi ya 5,000.
Alisema mradi huo utatekelezwa kwa uwekezaji kati ya Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC), Kampuni ya Minjingu na kampuni ya Ujerumani ambayo hakuitaja. Alisema kiwanda hicho kitasaidia kupunguza tatizo la uhaba wa mbolea nchini na pia kitaongeza matumizi ya nishati ya gesi hivyo kuiongezea mapato serikali.
Mbali na uwekezaji huo, Waziri Muhongo alisema katika siku za hivi karibuni nchi imeshuhudia uwekezaji wa bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam na kuingiwa kwa Mkataba wa ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Tanga hadi Uganda unaogharimu Sh bilioni 3.5 (Sh trilioni 7.4) .