RAIS John Magufuli amepokea taarifa ya maendeleo ya mradi mkubwa wa ujenzi wa kiwanda cha kusindika gesi asili (LNG Plant) kinachotarajiwa kujengwa katika eneo la Likong’o, Mchinga mkoani Lindi.

Mwakilishi Mkazi wa Kampuni ya Statoil ya nchini Norway ambayo ni moja ya kampuni zitakazowekeza katika mradi huo Oystein Michelsen alimueleza Rais Magufuli Dar es Salaam jana kuwa ujenzi wa kiwanda hicho unatarajiwa kugharimu Dola za Marekani bilioni 30 sawa na zaidi ya Sh trilioni 65 za Tanzania na kwamba uzalishaji unatarajiwa kuchukua muda wa zaidi ya miaka 40 baada ya kuanza.
Michelsen alibainisha kuwa Serikali ya Norway ina dhamira ya dhati ya kuhakikisha mradi huo unatekelezwa kwa manufaa ya pande zote na ameomba Serikali ya Tanzania iendelee kutoa ushirikiano ili kufanikisha ujenzi wa kiwanda hicho.
Kwa upande wake Rais Magufuli alimhakikishia mwakilishi huyo wa kampuni ya Statoil kuwa Serikali ya Tanzania ipo tayari kuhakikisha mradi unafanikiwa na kuitaka Wizara ya Nishati na Madini kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC) kushirikiana na wadau kutoka wizara nyingine kuharakisha mchakato wa kuanza kwa ujenzi wa kiwanda hicho.
Pamoja na Statoil, kampuni nyingine zinazoshiriki katika uwekezaji wa mradi huo ni Shell, Exxon Mobil, Pavillion na Ophir.