Follow us: Subscribe via RSS Feed Connect on YouTube Connect on YouTube
Maganga One Blog kwa habari za kitaifa,kimataifa,burudani na michezo kila siku. Tutumie habari na matukio yoyote kwa email yetu ya magangaone@gmail.com

Aug 4, 2016

Majaliwa: Mvomero twaeni mashamba yasiyoendelezwa

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amewaagiza viongozi wa Serikali wa wilaya ya Mvomero mkoa wa Morogoro, kutwaa mashamba yote yasiyoendelezwa.
Pia amewataka wafugaji wenye mifugo mingi nchini, kujiweka tayari kwa ajili ya kuhamia kwenye maeneo yatakayotengwa na serikali katika ranchi mbalimbali nchini ili wafuge kisasa.

Aidha, amewataka wafugaji hao kushirikiana na serikali katika kuboresha miundombinu ya maeneo hayo, ikiwemo ujenzi wa visima vya maji na majosho ili ufugaji wao uwe na tija. Alitoa kauli hiyo jana alipotembelea kiwanda cha kusindika nyama cha ranchi ya Nguru Hills wilayani hapa.
Alisema kitendo cha wafugaji hao kuhamia katika ranchi, kitawezesha mifugo yao kuwa na ubora kwa sababu aina ya ufugaji wa sasa ya kutembeza mifugo umbali mrefu inasababisha ufugaji wao kuwa na tija ndogo.
Akizungumzia kuhusu uwepo wa kiwanda cha kuchakata nyama wilayani Mvomero, alisema kitamaliza mgogoro wa muda mrefu kati ya wakulima na wafugaji kwa kuwa wafugaji watapata fursa ya kuuza mifugo yao kiwandani hapo.
Mkurugenzi na Mshauri wa kiwanda cha Nguru Hills, Dunstan Mrutu alisema kiwanda hicho chenye uwezo wa kuchinja ng’ombe 300, mbuzi na kondoo 1,500 kwa siku, kinatarajiwa kufunguliwa Desemba mwaka huu.
Alisema takriban asilimia 80 ya nyama itafungashwa na kuuzwa nje ya nchi, hasa Uarabuni kwa sababu nyama ya mbuzi ya Tanzania, imebainika kuwa na ubora na kukubalika katika nchi hizo.
“Mbali ya kiwanda cha nyama, pia tunatazamia kuwekeza katika mnyororo wa thamani kuanzia kusindika ngozi inayotoka kiwandani hadi kuzalisha viatu, mikanda na bidhaa zote za ngozi na kupunguza uagizaji wa bidhaa hizo kutoka nje ya nchi,” alisema.
Mrutu alisema nia yao ni kuitikia mwito wa Rais John Magufuli wa kutaka viwanda vizalishe viatu nchini kuanzia vya majeshi na wananchi wote, ambapo wamepanga kuanzia mwakani wataanza kuuza bidhaa hizo.
Aliongeza kuwa uwepo wa kiwanda hicho utatoa fursa kwa wafugaji na wakulima kuuza majani, mifugo na mazao ya chakula kama mtama, mahindi, ambapo tayari wameanza kuhamasisha jamii za wafugaji na wakulima wa Mvomero, Ngerengere na sehemu zinazozunguka eneo la kiwanda kuchangamkia fursa hiyo.

Share this article :

0 Maoni:

 
Maganga One Blog © Copyright 2017. All Rights Reserved.

Powered by Maganga One.
Back to TOP