Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda
MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amewasilisha mapendekezo kwa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, akiomba kuondolewa kwa Maofisa Ardhi na Mipango Miji wa Wilaya za Ilala na Kinondoni kwa kushindwa kutekeleza wajibu wao.

Watumishi hao ni Ofisa Ardhi na Mipango Miji wa Wilaya ya Ilala, Paul Mbembela na Ofisa Mipango Miji Wilaya ya Kinondoni, Juliana Letara. Makonda anadai kuwa maofisa hao, wameshindwa kutoa taarifa za mipango miji katika maeneo wanayoyasimamia na kuorodhesha maeneo ya wazi yaliyovamiwa.
Alitoa pendekezo hilo jijini Dar es Salaam jana, wakati alipofanya mkutano na madiwani na watendaji wa mkoa huo, uliokuwa na lengo la kujadili suluhisho la uvamizi wa maeneo ya wazi.
Makonda pia alitumia fursa hiyo, kuwataka wananchi waliovamia maeneo ya wazi ambayo yametengwa kwa matumizi mbalimbali kama ujenzi wa shule, zahanati na masoko, kubomoa nyumba zao kwa gharama zao kabla ya hatua kali hazijachukuliwa dhidi yao.
Aidha alitoa siku 10 kwa madiwani wote wa mkoa wa Dar es Salaam, kuhakikisha wanakabidhi ripoti ya maeneo yao yaliyovamiwa kwa wakuu wa wilaya ili imsaidie kuchukua hatua za kurejesha maeneo hayo yatumike kwa matumizi yaliyokusudiwa.
Alisema ofisi yake itachukua hatua kali kwa watumishi waliohusika kuuza au kubadilisha ramani ya viwanja vya wazi na kusababisha viwanja hivyo kupotea.
“Watumishi hawa watambue kuwa sheria itafuata mkondo wake ikiwa ni pamoja na kuwasimamisha kazi pamoja na kuwawajibisha kwa kufuata sheria. “Hatuwezi kuendelea kupoteza maeneo haya kwa sababu ya kushindwa kusimamia, ni lazima kila aliyehusika kusababisha upotevu huu awajibishwe,” alisema Makonda.
Alisema Jiji la Dar es Salaam lina changamoto nyingi za uvamizi wa viwanja vya wazi na kwamba jambo la kushangaza wavamizi hao, wanazo hati miliki huku pia wamiliki halali wakiwa na hati.
“Maeneo ya viwanja vya mpira yamevamiwa, maeneo ya shule yamevamiwa, maeneo ya zahanati yamevamiwa, lakini wavamizi wote wana hati miliki. Jambo la kujiuliza wamezitoa wapi? Nani aliyehusika kuwauzia? Ni wajibu wenu kuyapitia na kuyabainisha maeneo yote,” alisisitiza.
Alisema pia umezuka mtindo kwa wananchi, kuvamia maeneo ya shule na kujenga baa, jambo ambalo linasababisha usumbufu kwa wanafunzi na haliwezi kuachwa kuendelea.