SERIKALI ya Marekani, kupitia Shirika lake la Misaada ya Maendeleo (USAID), imeipatia Tanzania msaada wa dola za Marekani milioni 407, sawa na zaidi ya Sh bilioni 895 ili kusaidia miradi ya maendeleo.
Kiasi hicho cha fedha, kwa mujibu wa hati ya makubaliano, kitatumika kuendeleza sekta za kilimo, afya, nishati ya umeme, elimu na utawala bora katika kipindi cha miaka mitano ijayo kuanzia mwaka 2016/2020.

Hati za makubaliano hayo, zilitiwa saini jijini Dar es Salaam jana kati ya Mkurugenzi wa USAID, Sharon Cromer, na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dk Servacius Likwelile.
Msaada huo ni sehemu ya dola za Marekani milioni 800, sawa na zaidi ya Sh trilioni 1.76, ambazo Serikali ya Marekani kupitia USAID, imepanga kuipatia Tanzania.
Kwa mujibu wa makubaliano, lengo ni kufanikisha Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa katika kipindi cha miaka mitano ijayo, wenye lengo la kuiwezesha Tanzania kufikia uchumi wa kati kupitia Sekta ya Viwanda ifikapo mwaka 2025.
Kiasi hicho cha fedha, kitatumika na Serikali ya Tanzania kupitia Mfuko Mkuu moja kwa moja wakati kiasi kingine kitatumiwa na taasisi zisizokuwa za kiserikali, zinazofanya shughuli zake hapa nchini, kufanikisha malengo ya msaada huo.
Miradi iliyopewa kipaumbele ni pamoja na kupambana na Ukimwi na kifua kikuu, uzazi wa mpango, kupunguza vifo vya mama na mtoto, kukuza utawala wa kidemokrasia, usimamizi wa rasilimali za Taifa, na kuwekeza kwenye sekta ya umeme ili kuimarisha sekta ya viwanda na uzalishaji mali.