Mbunge wa Kawe, Halima Mdee
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeendelea kushikilia msimamo wa kuendeleza operesheni UKUTA Septemba mosi mwaka huu.
Rais John Magufuli alipiga marufuku maandamano na mikutano ya kisiasa isiyo na lengo jema ikiwemo ya viongozi kutoka kwenye maeneo yao kwenda kufanya mikutano kwenye maeneo mengine, jambo linalopingwa na Chadema kwa maelezo kuwa ni ukiukaji wa demokrasia.

Mbunge wa Kawe, Halima Mdee, alisema kwenye Baraza la Mashauriano la Kanda ya Pwani, lililofanyika jana Dar es Salaam kuwa wataitaarufu Polisi kuhusu maandamano yao watakayoyafanya bila kubeba silaha ili wapewe ulinzi.
Kwa mujibu wa Mdee ambaye ni Mwenyekiti wa Baraza hilo kwa Kanda ya Pwani, hawategemei kufanya fujo katika maandamano hayo, bali watatekeleza wajibu wao wa kudai demokrasia ambayo ni haki yao ya kikatiba, huku wakiwa wamejifunga vitambaa vyeupe mkononi na fulana nyeusi.
“Atakayefanya fujo katika maandamano hayo hayo Polisi watakuwa na haki ya kumkamata, vinginevyo tutadai haki yetu ya kidemokrasia ya kufanya mikutano na shughuli za kisiasa kwa njia ya amani”, Mdee alisema.