Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan
MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan amewataka watendaji wa Idara ya Mazingira katika ofisi yake, wajipange vizuri kwa ajili ya kufanya tathmini ya athari za kimazingira mjini Dodoma wakati serikali ikijiandaa kuhamia kwenye mji huo.
Makamu wa Rais alitoa kauli hiyo jana, alipokuwa akifunga Mkutano wa Kazi wa siku mbili na watendaji wa Idara ya Mazingira, ambapo walijadili namna ya kukabiliana na uharibifu wa mazingira unaoendelea kote nchini. Alieleza kuwa hatua hiyo, itasaidia kuuweka mji wa Dodoma salama kimazingira, ikiwemo ubora wa miundombinu za maji taka.

Makamu wa Rais alisema kutokana na idadi kubwa ya watu, hasa watumishi ambao watahamia Dodoma, bila miundombinu imara, hali ya uchafuzi wa mazingira itakuwa si nzuri, hivyo ni muhimu kwa watendaji hao kuweka mipango na mikakati madhubuti ya kuhakikisha mji wa Dodoma, hautaathirika kimazingira.
Kuhusu utendaji kazi wa watumishi wa ofisi yake, aliwataka watumishi wote kufanya kazi kwa ushirikiano na kwa uwazi katika matumizi ya fedha za miradi na hasa inayohusika na uhifadhi wa mazingira, jambo ambalo litaondoa manung’uniko miongoni mwa watumishi na wananchi kwa ujumla.
Alisema ushirikiano huo miongoni mwa watumishi, utasaidia kwa kiasi kikubwa ufanisi katika kazi za kila siku ili kufikia malengo waliyojiwekea.
Makamu wa Rais alisema ataendelea na utaratibu wa kukutana na watumishi kila baada ya miezi minne katika ngazi ya viongozi, kama hatua ya kujitathmini katika mipango ya kazi waliyojiwekea.