Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na usalama Wilaya ya Ikungi
Miraji Jumanne Mtaturu akizungumza
na askari wa Jeshi la polisi mara baada ya ziara yake katika makao makuu ya
Wilaya hiyo eneo la Ikungi.


Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Miraji Jumanne Mtaturu akisaini kitabu cha wageni mara baada ya
kuwasili Kituoni hapo.

 Dc Mtaturu akikagua
chumba cha mahabusu kituoni hapo
 Askari watiifu wa Jeshi la Polisi Wilayani Ikungi
waliposimama kutoa heshima zao kwa Mkuu wa Wilaya ya Ikungi alipotembelea
katika ofisi yao (Picha zote na Mathias Canal)

Dc Mtaturu akikagua maeneo mbalimbali
katika viunga vya Jeshi la Polisi Mkao Makuu Wilayani Ikungi
Askari watiifu Wilayani Ikungi wakimsikiliza kwa makini
Mwenyekiti wa kamati ya Ulinzi na usalama Wilaya Ya Ikungi
Dc Miraji Jumanne Mtaturu

 
Na
Mathias Canal, Singida




Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ambaye ni
Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Mkoani Singida Mhe
Miraji Jumanne Mtaturu
ameliasa jeshi la polisi Wilayani humo kutofanya
kazi kwa mazoea badala yake kuimarisha ulinzi na usalama wa Raia na mali zao.

Mtaturu
ameyasema
hayo wakati wa kikao cha pamoja na askari wa jeshi hilo Wilayani humo ikiwa ni
ziara yake ya mwanzo kudhuru katika ofisi za makao makuu ya Jeshi hilo kwa
ajili ya kujionea hali ya utendaji wa askari hao sawia na kukagua ofisi hizo
ili kujua changamoto zinazowakabili katika utendaji wao.

Mkuu huyo wa Wilaya amesema kuwa kitendo cha baadhi
ya askari kupokea Rushwa kutoka kwa wananchi ni miongoni mwa sababu
zinazopelekea wananchi kukosa imani na serikali na kulipaka matope jeshi hilo
ikiwa ni pamoja na kuifanya serikali ionekane haifanyi kazi yake ipasavyo.

“Hakuna asiyetambua kuwa Rushwa ni adui wa haki
hivyo nawasihi askari wapambanaji kutochukua Rushwa ili kuifanya jamii kuwa na
imani na askari wao jambo hilo litaongeza heshima kwenu na kwa serikali kwa
ujumla, lakini mnapaswa kutambua kuwa kupokea Rushwa kunasababisha wananchi
kujichukulia sheria mkononi jambo ambalo ni hatari kwa ustawi wa nchi yetu” Alisema Mtaturu

Mtaturu
alisema
kuwa Jeshi la Polisi ni sehemu ya ukombozi wa Taifa pia ni
sehemu muhimu  ya  kuimarisha usalama wa Wananchi, hivyo ikifikia
hatua wananchi wanakosa imani na jeshi la polisi ni wazi kuwa nchi itakuwa
inaelekea mahali ambapo sio sahihi.

Pamoja na mambo mengine Mkuu huyo wa Wilaya alisema
kuwa serikali inatambua kuwa kuna upungufu wa nyumba za kuishi askari, vifaa vya
utendaji kazi, Pamoja na mazingira na miundombinu kuwa duni hivyo serikali
imejipanga kuimarisha kadhia hizo kwa Jeshi la Polisi ambapo tayari kuelekea
kwenye maboresho wilaya ya Kinondoni Jijini Dar es salaam kuwa eneo la mfano
(Pilot Area) ili kuondoa changamoto hizo.

Dc
Mtaturu
ametoa mwito kwa askari hao kuwashirikisha wananchi
kwa kiasi kikubwa pale inapobidi ili kupunguza sintofahamu iliyopo katika jamii
ya askari kufanya kazi wenyewe pasina kushirikisha Raia kikamilifu.

“Nina amini katika utendaji wa ushirikishwaji kwa
wananchi kufanya hivyo ni kuwasaidia wananchi kupunguza hisia hasi walizonazo
juu ya utendaji wa Jeshi la Polisi, lakini pia nawaomba mfanye upelelezi kwa
haraka kwa kesi zilizopo mezani kwenu ili kurahisisha kupunguza mlundikano wa
kesi jambo linalopelekea kutotendewa haki kwa baadhi ya wananchi” Alisema Mtaturu

Kikao cha pamoja kati ya Mkuu wa Wilaya ya Ikungi na
Askari wa Jeshi la Polisi Wilayani humo kilikuwa na taswira chanya ya
kufahamiana, kuimarisha umoja kiutendaji pamoja na kukumbushana majukumu ya
kazi.

Mkuu huyo wa Wilaya ya Ikungi pia amewapongeza
askari hao pamoja na mazingira magumu waliyonayo lakini wanafanya kazi vizuri
kwa mujibu wa viapo vyao.