Rais John Magufuli akizungumza na Spika wa Bunge, Job Ndugai alipokwenda kumjulia hali nyumbani kwake Salasala, jijini Dar es Salaam jana. (Picha na Ikulu).
RAIS John Magufuli jana aliwatembelea na kuwajulia hali Spika wa Bunge, Job Ndugai na Makamu wa Rais na Waziri Mkuu mstaafu, John Samuel Malecela jijini Dar es Salaam.
Pamoja na kuwajulia hali jana, Rais Magufuli aliyeongozana na mkewe Mama Janeth Magufuli, aliwaombea kwa Mwenyezi Mungu wapone na kupata nguvu haraka ili waweze kuendelea na majukumu yao ya kawaida katika ujenzi wa Taifa.

Akizungumza na Rais Magufuli nyumbani kwake Salasala katika Manispaa ya Kinondoni, Spika wa Bunge, Ndugai alimshukuru Rais Magufuli kwa kumtembelea, kumjulia hali na kufuatilia kwa ukaribu wakati wote alipokuwa akipata matibabu nchini India hadi aliporejea nchini.
“Kwa kweli nimefarijika sana, kwanza naomba nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa sababu nilipopata matatizo haya ya maradhi alikuwa karibu sana na mimi nikiwa hapa nchini na hata nilipopelekwa India alinipigia simu mara kwa mara na kunifariji sana na hapa amekuja kuniona kwa niaba ya Watanzania, kwa kweli namshukuru sana na namuombea kwa Mwenyezi Mungu aendelee kumpa moyo huu wa kuwajulia hali wale wenye matatizo mbalimbali.
“Lakini niwahakikishie Watanzania, kwamba kwa sasa nina nafuu kubwa sana, naweza kufanya kazi nyingi tu sasa, lakini tuendelee kuombeana,” alisema Ndugai alipokuwa akizungumzia hali yake kwa sasa.
Naye Makamu wa Rais na Waziri Mkuu mstaafu, Malecela pamoja na kumshukuru Rais Magufuli na mkewe Mama Janeth Magufuli kwa kumtembelea, alisema afya yake inazidi kuimarika na pia amewashukuru madaktari wanaomtibu.