Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu
WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu ameziagiza hospitali zote za rufaa nchini ngazi ya Mikoa, Kanda na Hospitali ya Taifa Muhimbili kutoa matibabu bure kwa wagonjwa wa fistula.
Aliyasema hayo mjini Tanga kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Bombo katika uzinduzi wa kambi ya matibabu ya wagonjwa wa fistula itakayodumu kwa kipindi cha wiki moja kuanzia juzi hadi Agosti 19, mwaka huu.

Alisema tatizo la fistula limekuwa likiongezeka kila siku na waathirika wengi ni akinamama wa vijijini na wale wa kipato cha chini ambao wanashindwa kupata huduma sahihi za afya ikiwemo kuchelewa kwenda kwenye vituo vya kutolea huduma za afya wakati wa kujifungua.
Takribani akinamama 2,500 hadi 3,000 hupata tatizo la ugonjwa wa fistula kila mwaka japo idadi hii ni ndogo sana kuliko hali halisi ilivyo kwa kuwa wagonjwa wengi hunyanyapaliwa na familia zao na jamii kwa ujumla.
“Serikali ya Awamu ya Tano imejikita zaidi katika kuwahudumia wanyonge, kwa mamlaka niliyopewa natoa msamaha wa kulipia matibabu ya fistula ili kuwapunguzia mateso wanawake hawa. Kwa kuwa wenye tatizo la fistula ni wanawake wa kipato cha chini na wa vijijini, naziagiza hospitali zote za rufaa za mikoa na kanda kutoa matibabu ya fistula bure kwa wagonjwa watakaofika kutaka huduma hiyo,” alisema Ummy.
Alisema ili kuhakikisha huduma hiyo inatolewa, ameziagiza hospitali hizo kuandaa kambi za matibabu ya fistula angalau mara moja kila mwaka na apatiwe taarifa.
Aidha, ameeleza kuwa akinamama wengi wenye tatizo la fistula wamekuwa wakishindwa kufanya shughuli za uchumi kama biashara ndogo ndogo kwa kuwa ugonjwa huu ni wa aibu ambao husababisha watu kunyanyapaliwa na jamii.
Pia alieleza hatua mbalimbali zilizochukuliwa na serikali katika kukabiliana na tatizo la ugonjwa huu ikiwa ni pamoja na uboreshaji wa miundombinu kwa ajili ya huduma za ujauzito na uzazi, mafunzo ya huduma za dharura za uzazi kwa watoa huduma za afya pamoja na usimamizi shirikishi, uimarishaji wa ubora wa huduma za ujauzito na uzazi, kuimarisha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba kwa ajili ya ujauzito na uzazi, kuimarisha mifumo ya rufaa na kuhakikisha huduma za dharura za uzazi zinapatikana hasa maeneo ya vijijini na wataalamu waliobobea katika maeneo hayo.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Dk Asha Mahita alisema Hospitali ya Bombo ina changamoto ya kuwa na miundombinu chakavu, uhaba wa vifaa tiba na watumishi kiasi ambacho wanashindwa kutoa huduma ya kutibu akinamama wenye tatizo la fistula kwa kuwa hawana wataalamu waliobobea katika maeneo hayo.