Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa Rita, Emmy Hudson
TAASISI, asasi za kiraia na kidini pamoja na mashirika yasiyo ya kiserikali zaidi ya 5,000 yanayosajiliwa na Wizara za Mambo ya Ndani ya Nchi na ile ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto pamoja na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) yapo katika hatihati ya kufutiwa usajili.

Aidha, bodi za udhamini 500 zimebainika kuwa mfu.
Hayo yamebainika kutokana na uhakiki uliofanyika kwa miezi mitatu baada ya Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Harrison Mwakyembe kuunda kikosikazi kupitia mifumo ya usajili na kukabidhiwa ripoti hiyo jana.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa Rita, Emmy Hudson alisema taasisi 180 zimepelekwa katika Gazeti la Serikali kwa ajili ya kuchapishwa ili kuzitangaza kufutwa kwa mujibu wa Sheria mwishoni mwa mwezi huu na hatua hiyo imefikiwa baada ya kutangazwa kusudio la kufuta taasisi 200 na 20 pekee kujitokeza kuhakikiwa.
Alisema pia wanaandaa tangazo jingine la kufuta taasisi nyingine 320 ambalo litatolewa mara tu baada ya kufutwa rasmi kwa taasisi 180. Alisema bodi za wadhamini 1,944 kati ya 5,262 zilizosajiliwa, ziliwasilisha taarifa zao wakati wa uhakiki kwa njia mbalimbali kama barua pepe na kupeleka ofisini na kubaini bodi hizo 500 kuwa mfu.
Aliongeza kuwa, walikagua na kuhakiki mahali zilipo na wadhamini wake kwa taasisi 282 katika mikoa ya Dar es Salaam, Arusha, Songwe, Mbeya na Mwanza na kubaini changamoto mbalimbali ikiwemo ya taasisi na asasi kumiliki mali bila kuwa na usajili wa bodi za wadhamini.
Hudson alisema baadhi ya taasisi zinabadilisha majina yao bila kutoa taarifa kwenye ofisi ya msimamizi mkuu wa wadhamini, hivyo kutambulika kwa majina tofauti na yaliyosajiliwa huku taasisi nyingine zikishindwa kujiendesha kutokana na utegemezi wa wafadhili.
Msajili Msaidizi wa Asasi za Kidini na Kiraia katika Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Mary Komba alisema mpaka sasa kuna asasi 16,000 zilizosajiliwa na kati ya hizo, 3,000 zilibainika kuwa na dosari na kuwekwa katika orodha ya kuondolewa mara baada ya taratibu kukamilika.
Komba alisema sasa kuna asasi 1,500 zilizopo katika uchunguzi baada ya kuomba kusajiliwa na kwamba sasa hawajafikia hatua ya kupewa cheti na nyingine 11,500 zinaendelea kuhakikiwa iwapo ni hai na ikibainika kuwa mfu, zitaondolewa.
Alisema uhakiki huo wanaufanya kwa kutumia nyaraka walizonazo kwa kuangalia hesabu zao za mwaka, taarifa muhimu za makao makuu yao na nyinginezo pamoja na taarifa za mikutano yao ya mwaka na kuingiza katika kanzidata mpya.
Naye Mkurugenzi Msaidizi wa Mashirika yasiyo ya kiserikali katika Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Baraka Leonard alisema mashirika yaliyosajiliwa mpaka sasa ni 8,000 na yaliyo hai ni 5,000 huku zaidi ya 2,000 wanaandaa tangazo kutoa taarifa kama zipo au la na ikibainika hazipo watazifuta.
Alisema mashirika yote yasiyo ya kiserikali yanatakiwa kusajiliwa na kufanya kazi kwa mujibu wa sheria na ikibainika kuwepo yasiyosajiliwa watashitakiwa na adhabu yake ni kifungo cha mwaka mmoja jela.
Dk Mwakyembe alikabidhiwa ripoti hiyo na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Amon Mpanju na kusema watakutana na mawaziri kutoka wizara zinazohusika wakiwa bungeni kwa lengo la kuangalia utekelezaji wa ripoti hiyo kutokana na kuwa zipo baadhi ya asasi za kiraia zinatumia vibaya usajili wake.
“Zipo hata taasisi za kidini ambazo zinatumia mwanya wa misamaha ya kodi vibaya kwa kuomba vibali na nyingine ambazo hazipo, hivyo tukikaa tutaangalia jinsi ya kukabiliana na changamoto zilizopo na ikibidi hata kubadilisha baadhi ya sheria,” alisema Dk Mwakyembe.
Alisema katika uhakiki huo zitapunguzwa asasi na taasisi ambazo zimesajiliwa nyingi, lakini hazipo hivyo kuziondoa zilizo hewa hasa za kidini zinazotumia vibaya misamaha ya kodi na nyinginezo.
Awali, Mkurugenzi wa Idara ya Katiba na Ufuatiliaji Haki wa wizara hiyo, Patience Ntwina alisema katika uhakiki huo wamebaini changamoto mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kuingiliana kwa taratibu za kisheria katika usajili na kukosekana ufuatiliaji wa taasisi mbalimbali zilizosajiliwa hasa zilizo mbali na Mkoa wa Dar es Salaam.
Changamoto nyingine ni kiwango kidogo cha ada kisichokwenda na wakati huku sheria ikitumika kwa muda mrefu bila kufanyiwa marekebisho, jambo lililosababisha kuwepo kwa vikundi vya hiari katika vijiji, kata na mitaa ambavyo havijasajiliwa, lakini vinatambuliwa na mamlaka za maeneo hayo na kutaka kutambulika kisheria.