Mkuu wa Bandari ya Tanga, Henry Arika
MAMLAKA ya Usimamizi wa Bandari (TPA) imetenga jumla ya Sh bilioni 9.2 za kuboresha miundombinu katika bandari yake ya Tanga ili kurahisisha mapokezi ya vifaa vya Mradi wa ujenzi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP), unaotarajiwa kuanza hivi karibuni.

Shughuli za uboreshaji huo zinajumuisha kazi kubwa tatu, ikiwemo gati kwa kuongeza kina chake ili iwezeshe meli kubwa zitakazobeba vifaa vya ujenzi kutia nanga kwa urahisi bandarini hapo, tofauti na ilivyo sasa ambapo meli hulazimika kutua nje.
Mkuu wa Bandari ya Tanga, Henry Arika alibainisha hayo katika mahojiano na waandishi wakati wa ziara fupi katika kata ya Chongoleani, kukagua eneo la ujenzi huo utakaosafirisha mafuta kutoka Uganda kupitia Bandari ya Tanga kwenda kwenye masoko ya kimataifa.
“Utekelezaji unaendelea kwa kuongeza kina cha maji pale bandarini, kazi nyingine tunajenga skana (scanner) ya kukagulia mizigo ili kuimarisha usalama na pia tunajenga eneo maalumu lenye ukubwa wa kilometa za mraba 2,600 litakalotumika kuhifadhia shehena ya mzigo wa vifaa hivyo kabla ya kuvisafirisha kwa gari kuelekea eneo la ujenzi,” alisema.
Arika alisema wakati wa maandalizi ya ujenzi wa gati pamoja na bomba hilo la mafuta upande wa Tanzania, TPA inatarajia kupokea jumla ya tani 250,000 za shehena ya vifaa kupitia bandari hiyo ya Tanga, hivyo maboresho yanayofanyika sasa ni ya muhimu sana kwenye mradi huo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Jiji la Tanga, Daudi Mayeji alisema pamoja na kusafisha eneo na kuchonga barabara, wananchi nao wameandaliwa vya kutosha kushiriki utekelezaji wa mradi huo.
“Maandalizi yako vizuri na tayari tumewaandaa vizuri wananchi wetu wakiwemo wa Chongoleani ambao tumewahakikishia kwamba serikali itazingatia sheria ili kila mhusika apate haki yake wakati wa ulipaji wa fidia kwa baadhi ya wakazi ambao mimea, ardhi na mashamba yao yatachukuliwa kwa ajili ya kuingizwa katika eneo la mradi,” alisema.
Akizungumzia uvamizi wa ardhi ya Chongoleani, uliokuwa ukifanywa na baadhi ya wananchi mwanzoni mwa mwaka huu, alisema kasi imepungua.
Aidha, alisema halmashauri kwa kushirikiana na uongozi wa Serikali ya Mtaa huko Chongoleani, wamekubaliana kuendeleza ulinzi shirikishi ili wageni pamoja na mali za mradi visije vikahujumiwa.