Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TPDC, Profesa Sufian Bukurura
BODI ya Wakurugenzi ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) imethibitisha kumsimamisha Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo, Dk James Mataragio na kuongeza kuwa pia imewasimamisha wakurugenzi wanne kutokana na tuhuma za ukiukwaji wa taratibu za utendaji kazi.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana iliyosainiwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya shirika hilo, Profesa Sufian Bukurura, kusimamishwa kazi kwa watendaji hao kunatokana na tuhuma za awali zikiwemo za ukiukwaji wa sheria na kanuni za manunuzi ya umma.
Aliwataja wengine wanne waliosimamishwa kazi ili kupisha uchunguzi wa tuhuma zinazowakabili ni Mkurugenzi wa Mkondo wa Juu, Kelvin Komba, Mkurugenzi wa Fedha, George Seni, Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Ndani, Gabriel Mwero na Mkurugenzi aliyekuwa anasimamia ugavi na manunuzi, Edwin Riwa.
Akizungumzia tuhuma za awali zinazowakabili watendaji hao, Profesa Bukurura alisema ni pamoja na ukiukwaji wa sheria na Kanuni za Utumishi hususan mgongano wa kimaslahi, kubadili matumizi ya fedha za bajeti bila idhini ya mamlaka ya juu na kutokutoa taarifa muhimu na nyeti hususan za shughuli za shirika hilo.
Alisema hatua hiyo ya kuwasimamisha kazi kupisha uchunguzi imekuja baada ya bodi hiyo kukutana kwenye kikao cha dharura kilichofanyika Agosti 24, mwaka huu.
Aidha, alisisitiza kusimamishwa kazi kwa watajwa hao hakuna maana kuwa wamepatikana na hatia kwa sasa, bali ni hatua ya awali ya kuwezesha uchunguzi kufanywa katika mazingira rafiki ili kubaini ukweli wa tuhuma hizo kama zina uzito kisheria au la. Alisisitiza watapewa nafasi ya kujieleza na kujitetea kulingana na kanuni za utumishi wa umma.