MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amezindua rasmi programu maalumu, inayolenga kuboresha sekta ya usafiri wa pikipiki maarufu kama bodaboda pamoja na bajaji, ambao sasa watasajiliwa kwa namba zao maalumu, zitakazokuwa zimeandikwa katika sare watakazokuwa wamevaa.

Programu hiyo itafahamika kama Mwonekano mpya wa Pikipiki na Bajaji Dar es Salaam. Itakapoanza, hakutakuwa na ulazima wa polisi kukimbizana na bodaboda na itakuwa rahisi kupunguza vitendo vya uhalifu.
Akizungumza wakati wa kuzindua programu hiyo, Makonda alisema itamsaidia abiria endapo itatokea jambo lolote, mtu atakuwa na uwezo wa kutumia simu yake ya mkononi kwa kuingiza namba maalumu, kama za huduma za kifedha na kwenda katika kipengele cha huduma ya Bodaboda na Bajaji Mkoa wa Dar es Salaam, kisha kuingiza namba iliyoko katika sare ya dereva.
Makonda alisema baada ya kuingiza namba hiyo, ataweza kupatiwa jina halisi la dereva, namba ya usajili wa pikipiki yake, eneo analoegesha, kiongozi wa eneo lake kwa upande wa bodaboda na namba zake za simu pamoja na za kiongozi huyo.
Pia bodaboda na madereva bajaji wote mkoani humo, watakuwa na sare maalumu ambazo watagawiwa bure pamoja na kofia ngumu.
Alisema amekusudia kuboresha sekta hiyo ili iwe ya kuaminika pamoja na kuepusha usumbufu wanaokumbana nao madereva hao. Aliongeza kuwa kuzinduliwa kwa programu hiyo kutaepusha bughudha katika usafiri hasa baina ya madereva na Polisi, hali iliyojenga uhasama.
“Maboresho haya yamekusudia pia kutaka kuwaondoa kabisa wakamataji wa pikipiki na bajaji jijini Dar es Salaam,” alisema na kuwataka madereva hao, kufuata sheria zilizowekwa ili kuepuka ajali zisizo za lazima pamoja na makosa yanayoweza kuepukika.
Aliagiza Jeshi la Polisi Kitengo cha Usalama Barabarani mkoani humo, kuongeza idadi ya askari katika barabara zote kuanzia leo ili kuhakikisha kwamba sheria zinafuatwa na kuheshimiwa.
Katika hatua nyingine, Makonda amezindua rasmi Chama cha Madereva na Wamiliki Bodaboda na Bajaji mkoani humo, ambapo alipongeza hatua hiyo na kuwataka wanachama kukitumia ili kujitelea maendeleo.
Awali, Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Bodaboda na Bajaji mkoani humo, Daud Laurian alimpongeza mkuu huyo wa mkoa kwa ubunifu huo na kwamba hatua hiyo itaiongezea heshima kubwa sekta ya usafiri huo ambayo ilikuwa ikitafsiriwa kuwa ni ya uhalifu na uhuni.
Alisema, bodaboda na bajaji kwa kila wilaya yaani Temeke, Kinondoni, Ilala, Ubungo na Kigamboni watakuwa na rangi zao za sare pamoja na namba zao.
Aliongeza kuwa pamoja na mambo mengine, mwonekano huo mpya umelenga kuongeza fursa za kibiashara katika usafiri huo, ambapo mtu, taasisi au shirika litakalohitaji kubandika tangazo katika kofia ngumu au pipiki atalazimika kulipia.
“Lakini pia, sekta hii sasa inachangia kwa kiasi kikubwa katika pato la taifa, ambapo kwa mkoa wa Dar es Salaam kwa mwaka inaweza kuingiza zaidi ya shilingi bilioni mbili,” alisema Laurian.
Uzinduzi huo uliandaliwa kwa ushirikiano mkubwa baina ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Nchi Kavu na Majini (SUMATRA), Chotec Limited, Jeshi la Polisi, Shell Advance, Clouds FM, Event Master na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali pamoja na madereva wa bodaboda na bajaji.