Serikali ya Tanzania imepokea msaada wa tani 183 za vyakula mbalimbali kutoka Serikali ya Burundi kwa ajili ya kuwafuta machozi waathirika wa tetemeko la ardhi lililotokea mkoni Kagera mapema mwezi huu na kuathiri maisha ya wakazi wa mkoa huo.

Makabidhiano ya msaada wa vyakula hivyo kutoka nchini Burundi yamefanyika mpakani mwa Tanzania na Burundi katika eneo la Kituo cha Ushuru cha Pamoja (OSBP) cha Kabanga wilayani Ngara ambapo Serikali ya Tanzania iliwakilishwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Suzan Kolimba na Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali Mstaafu Salum Kijuu wakati Burundi iliwakilishwa na Waziri wa Afrika Mashariki Bi. Leontine Nzeyimana na Waziri wa Mambo ya Ndani wa nchi hiyo Bw. Pascal Barandagiye.
Akikabidhi vyakula hivyo, Waziri Bi. Leontine amesema kuwa Serikali ya Burundi na Warundi wote walipatwa na mshtuko mkubwa na majonzi baada kusikia taarifa ya maafa yaliyowatokea ndugu zao wa mkoani Kagera."Kwa Kirundi tunasema, "Umubanyi niwe muryango" ikimaanisha jirani yako ni ndugu yako, kwa maana hiyo imekuwa ni wajibu kwa Serikali ya Burundi kuagiza wawakilishi wake ili waweze kufika hapa nchini Tanzania mkoani Kagera kuwaona ndugu zetu Watanzania na kuwapa pole".
Waziri Bi. Leontine aliendelea kusema "Ndio maana tumekuja na kifurushi kidogo tu ili tuweze kuwaliwaza ndugu zetu waliofikwa na matatizo hayo" alisema Waziri Bi. LeontineWaziri Bi. Leontine alivitaja vyakula hivyo kuwa ni pamoja na mchele tani 100, mahindi tani 50, sukari tani 30 na majani ya chai tani 3.
Akizungumzia suala la mahusiano ya Tanzania na Burundi, Waziri Bi. Leontine amesema kuwa udugu uliojengeka baina ya nchi hizo mbili na wananchi wake ni wa kihistoria, si wa leo au wa jana na kusema Serikali yake inadhamira ya kuendeleza udugu huo vizazi na vizazi huku akiamini Tanzania nayo ina dhamira hiyo hiyo.
Akitoa shukrani baada ya kupokea msaada huo, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Suzan Kolimba ameishukuru Serikali ya Burundi kwa msaada waliotoa kwa Tanzania na kuongeza kuwa msaada waliotoa ni kielelezo cha mahusiano ya karibu na ya kidugu baina ya nchi hizo mbili na watu wake.
Pia Naibu Waziri Dkt. Suzan amewataka viongozi wa Serikali ya Burundi wafikishe salamu na shukrani za dhati za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa Rais wa Jamhuri ya Burundi Pierre Nkurunzinza na kuwathibitishia kuwa Tanzania itaendeleza uhusiano mzuri uliopo baina ya nchi hizo.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Kagera ambao ndio umeathirika na tetemeko hilo Meja Jenerali Mstaafu Salum Kijuu ambaye pia ni Mkuu wa Ulinzi na Usalama wa mkoa huo ameihakikishia Serikali ya Burundi kuwa msaada walioutoa utawafikia walengwa kama ilivyokusudiwa.Msaada huo uliotolewa na Burundi umekuwa ni mwendelezo wa misaada inayotolewa na nchi za Afrika Mashariki kwa Tanzania kufuatia tetemeko la ardhi lililotokea Septemba 10 mwaka huu na kuathiri mikoa ya kanda ya ziwa.
Burundi imeungana na nchi za Uganda na Kenya kwa kutoa misaada kwa waathirika wa tetemeko hilo ambapo September 17 mwaka huu Rais Dkt. John Pombe Magufuli alipokea mchango wa fedha taslimu kiasi cha Dola za Kimarekani laki 2 ambazo ni sawa na takribani Shilingi za Kitanzania milioni 437 kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Uganda Yoweri Kaguta Museveni na mchango wa mabati, blanketi na magodoro vyenye thamani ya Shilingi za Kitanzania milioni 115 kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Kenya Uhuru Kenyatta kwa ajili ya kuwasaidia waathirika wa tetemeko la ardhi Mkoani Kagera.