WAKATI leo wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wakiwa wamejipanga kufanya mikutano na maandamano nchi nzima, Kamati Kuu ya chama hicho imetangaza kusitisha kampeni hiyo iliyopewa jina la Ukuta.

Hatua ya kusitishwa kwa maandamano na mikutano hiyo ilitangazwa jana, baada ya Kamati Kuu ya Chadema kukaa juzi na kukubaliana kusitisha kampeni hiyo kutokana na ombi la viongozi wakuu wa dini mbalimbali nchini.
Aidha, watu wa kada mbalimbali wakiwamo wasomi na viongozi wa dini wamepongeza hatua hiyo na baadhi yao kupendekeza kuwa maandamano hayo yafutwe kabisa kwa sababu hayana tija na yangesababisha uvunjifu mkubwa wa amani nchini.
Maandamano hayo yalipigwa marufuku na Jeshi la Polisi nchini na kuzuia mikutano yote ya kisiasa ya hadhara na ya ndani kwa kueleza kuwa kulikuwa na ishara ya uvunjivu wa amani katika mikutano hiyo.
Aidha, Rais John Magufuli alitangaza kuwa wanasiasa ni vyema wakajikita katika suala la maendeleo badala ya kuendesha mikutano katika maeneo yasiyo yao ya kiutawala na maandamano yasiyo ya kikomo.
Akitangaza uamuzi wa kusitishwa kwa kampeni hiyo iliyopewa jina la Umoja wa Kupinga Udikteta Tanzania (Ukuta), Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Freeman Mbowe alisema baada ya kutafakari kwa kina maombi ya viongozi hao wameamua kuahirisha mikutano na maandamano hayo.
Alisema wameamua kuahirisha maandamano na mikutano hiyo kwa mwezi mmoja ili kutoa nafasi kwa viongozi hao wa kiroho kutafuta suluhu ya jambo hilo kwa kukutana na Rais Magufuli na serikali yake.
Viongozi wa dini, asasi Mbowe alisema mbali na viongozi wakuu wa kidini wa madhehebu mbalimbali, pia taasisi mbalimbali za kiraia nazo zimewaomba na kuwasihi kuahirisha Ukuta kwa muda ili mazungumzo na majadiliano yafanyike.
“Tunatambua mchango mkubwa ambao umetolewa na dini zote hapa nchini katika kutunza utulivu uliopo Tanzania na katika ustawi wa kiuchumi na kijamii wa Tanzania… tunaelewa rai ya viongozi wetu wa kiroho juu ya umuhimu wa kutafuta suluhu ya mgogoro huu wa kisiasa kwa mazungumzo na majadiliano,” alisema Mbowe.
Hata hivyo, alisema endapo jitihada za viongozi hao hazitazaa matunda katika kipindi hicho, mikutano na maandamano hayo yatafanyika kuanzia Oktoba mosi, mwaka huu huku akiwataka wanachama na viongozi wao kuendelea kufanya maandalizi.
Alisema mwito huo wa viongozi wa dini una busara na unalijali taifa na watu wake na haupaswi kupingwa kwa sababu nyepesi, hivyo hawawezi kuwakaidi viongozi wa kidini katika mwito huo wa busara.
Alisema katika kipindi cha mwezi mmoja tangu kutangazwa kwa Ukuta, wameshuhudia nchi ikipita katika kipindi ambacho amedai ni Tanzania imekuwa ikiserereka kwa kasi kwenye mteremko wa utawala wa kidikteta.
Aliongeza kuwa sababu iliyowafanya waahirishe maandamano na mikutano yao sio kuwaogopa polisi, bali ni kwa ajili ya mazungumzo na kama wangeendelea na msimamo wao wa kufanya maandamano hayo ni kweli wangekuwa na nia ya kuharibu amani ya Taifa.
Aidha, alisema baada ya viongozi hao pia kuwaomba kurudi Bungeni kwa kuwa watazungumza na Spika wa Bunge, Job Ndugai, watakutana mjini Dodoma kwa ajili ya kujadiliana jambo hilo ili warudi bungeni.
Alisema tangu kutangazwa kwa kampeni hiyo, viongozi wao zaidi ya 230 wameshitakiwa na wengine 28 akiwemo Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salum Mwalimu wanashikiliwa na Polisi. Salum anashikiliwa mkoani Simiyu.
Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho, Edward Lowassa akijibu swali la waandishi waliotaka kujua alizungumza nini na Rais Magufuli walipokutana katika Misa ya Jubilei ya Dhahabu ya miaka 50 ya ndoa ya Rais mstaafu Benjamin Mkapa na mkewe, alisema hakuna jambo kubwa walilozungumza. Alisema hakuna jambo kubwa la msingi alilozungumza na Rais Magufuli, bali alimwahidi kuwa watawasiliana.
“Ni nani miongoni mwenu anayeweza kukataa mkono wa Rais akimtakia amani tena mbele ya Kardinali (Polycarp Pengo) na viongozi wakubwa wa dini. Aliniahidi tutawasiliana na mimi nasubiri mawasiliano,” alisema Lowassa aliyekuwa mgombea urais wa Chadema na vyama vitatu vingine washirika katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka jana na kushindwa na Dk Magufuli. Bana:
Ukuta usingewezekana
Akizungumzia suala hilo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Benson Bana alisema Chadema wametumia mwanya wa viongozi wa dini kupata upenyo kwa kuwa hata wao walijua kuwa Ukuta usingeweza kufanyika.
Alisema hawatakiwi kujificha kwa viongozi wa dini kwa kuwa hawana vyama, bali wajibu wao mkubwa ni kuwaombea Watanzania wote na kuwaongoza katika njia iliyonyooka.
“Mimi nilishaona kuwa hayo maandamano hayapo. Wamepata upenyo wa viongozi wa dini, tunawashukuru viongozi wa dini, lakini wasiishie katika mikutano na maandamano kuna mambo mengine mengi wanapaswa kushauri,” alisema Profesa Bana.
Alisema Watanzania hawapendi kuona maandamano hayo, lakini pia wanachukia kuona Rais wao akikejeliwa na kubezwa na wanataka aheshimiwe na huo ndio utamaduni wa Mtanzania.
Alisema alitambua kuwa mkakati wa chama hicho hauwezi kufua dafu, na kwamba hawakuwa na njia nyingine kwa kuwa shinikizo la viongozi wa dini, taasisi za kiraia na makundi mengine ya wapenda amani lilikuwa kubwa. “…mwanzo walikuwa wakiangalia mambo ambayo serikali ilikuwa haifanyi sasa rais na serikali yake wanafanya yote yale ambayo yalikuwa yakipigiwa kelele, hawana hoja tena,” alisema Profesa Bana na kueleza kuwa kuna mambo matatu ambayo upinzani kama wakiona yale waliyokuwa wakiyasimamia yakitekelezwa wanatakiwa kufanya, ambayo ni kumuunga mkono Rais, kumsaidia kufanikisha anayoyafanya na kama wakiona hawawezi wanatakiwa kukaa kimya hadi 2020.
Shehe: Ni jambo jema Kwa upande wake, Shehe wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum alisema Chadema kusitisha mikutano na maandamano ya Ukuta ambaye yangeanza leo ni jambo jema na hiyo ni ishara wanaheshimu viongozi wa dini.
“Kuitunishia serikali msuli si jambo la busara na kama kweli wametusikiliza sisi ni jambo jema na sisi tunaamini Rais anaheshimu viongozi wa dini na Serikali yetu ni sikivu, hivyo hili jambo litamalizika,” alisema Alhad na kuongeza kuwa Chadema wasifikirie kama kutakuwa na maandamano kwa kuwa jambo hilo litamalizika kabla ya Oktoba Mosi.
Mhadhiri anena
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Bashiru Ally alisema mpango huo wa maandamano ulianza kukataliwa tangu awali ulipotangazwa, kwani ni mpango ulioashiria kuvunja na kudhoofisha amani pamoja na misingi ya umoja wa kitaifa.
Alisema mpango huo ulikuwa wa kitatanishi, ukitoa hali ngumu kwa vyombo vya dola na hata wasiwasi pia kwa siasa za nje.
“Kuahirishwa ni kutimiza wajibu wao, watimize wajibu wao wa kisiasa, wamejisahau na ulikuwa ni mpango hatari licha ya kwamba kwa kuahirisha bado una ukakasi,” alisema na kuongeza kuwa nchi ina namna ya kutatua matatizo yake na demokrasia ina namna ya kusuluhisha matatizo mbalimbali.
Alisema chama hicho kingeweza kutumia vyombo kama Bunge katika kuwasilisha matatizo yake kwa kupeleka hoja mbalimbali, na kama sheria haipo kuweza kuitunga na kama iliyopo ina udhaifu kufanyiwa marekebisho pamoja na kuimarisha sheria zilizopo.
Alisema pia kama wangeona Bunge hapafai wangekwenda mahakamani, na kuongeza kuwa wamesumbua amani ya nchi bila sababu na kuyumbisha watu, ni vyema wakaachana na mipango hiyo ambayo ni ya kihalifu wakijua kuwa siasa sio genge, bali watambue kuwa wao ni chama cha siasa kinachostahili kufuata sheria, kanuni na taratibu, maandamano hufanywa na magenge ya wahuni.
Waziri asisitiza amani
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yussuf Masauni alisisitiza kuhusu kulindwa amani ya nchi, na wanasiasa wanapaswa kutii mamlaka na sheria za nchi na wasiwahamasishe wananchi kushiriki katika matukio yasiyo na tija kwao.
Alisema serikali haitokubali wala haitokuwa na mazungumzo kwa wenye nia ya kuvunja amani ya nchi.
“Kama dhamira yao ni kupata umaarufu, hilo halikubaliki na wananchi wanahitaji maendeleo,” alieleza Masauni.
Meya apongeza Naibu Meya wa Manispaa ya Ilala, Dar es Salaam, Omary Kumbilamoto amesema hatua hiyo ya Chadema ni nzuri kwa kuwa wananchi wengi walijawa na hofu kutokana na vitisho vilivyojitokeza.
Kumbilamoto, Diwani wa Kata ya Vingunguti (CUF), amesema licha ya madai yao ya kutaka kuwa na mikutano ya kisiasa, lakini njia waliyokuwa wanataka kuitumia Chadema haikuwa sahihi.
Katibu wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Amani Golugwa amesema wamepokea usitishwaji wa maandamano hayo kwa heshima ya viongozi wa chama na dini na kueleza kuwa, wametoa muda wa mwezi ikiwa hawataafikiana katika masuala ya msingi, maandamano hayo yatafanyika.
Polisi walikwisha jipanga
Mapema jana, makamanda mbalimbali wa mikoa nchini walieleza kuwa wamejipanga kuhakikisha yeyote atakayefanya maandamano anakabiliana na mkono wa dola.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Ulrich Matei alisema askari wa vikosi mbalimbali wa jeshi hilo wamejipanga kwa ajili ya kuwashughulikia wote watakaojitokeza kufanya maandamano ya Ukuta kinyume na sheria.
Kamanda Matei alisema hayo jana baada ya kumalizika kwa mazoezi ya ukakamavu yaliyoanza saa 12 asuhuhi hadi saa mbili kwa kutembea kilometa kadhaa ikiwa ni moja ya majukumu ya kila siku ya mazoezi ambayo pia yalishirikisha vikosi vya Ulinzi na Usalama vya Polisi, Magereza, Mgambo na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
Kebwe, Gambo wanena Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk Kebwe Stephen Kebwe, alisema juzi mjini hapa kuwa vyombo vya ulinzi na usalama vimejipanga kukabiliana na watakaothubutu kuandamana kwenye maandamano ya Ukuta.
Mwenyekiti wa Wilaya wa NCCR-Mageuzi, Maulid Ibangi akizungumza na gazeti hilo jana alisema uongozi wa Chadema Taifa hadi Mkoa hawajavishirikisha vyama vinavyounda Ukawa suala hilo hivyo halihusiki na umoja huo.
Alisema kwa kuwa ni operesheni ya chama kimoja, hawawezi kuwaunga mkono katika maandamano yao. Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo aliwasihi wananchi wasishiriki na kuwahakikishia kuwa wamejipanga kuhakikisha hakuna maandamano wala vurugu zitakazotokea. Gambo alikuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake.
Alisema vyombo vya ulinzi na usalama mkoani humo vimejipanga kuhakikisha hakuna vurugu zinazotokea wala maandamano ya Ukuta.
Nao Umoja wa Wafanyabiashara wa Soko la Kilombero lililopo jijini humo ulisema hawatashiriki maandamano hayo kutokana na athari za kisiasa walizokumbana nazo kipindi cha nyuma.
Mwenyekiti wa umoja huo, Abdi Mchomvu, alisema leo wataungana na kushirikiana na wanajeshi kufanya usafi katika soko hilo.
Imeandikwa na Katuma Masamba, Lucy Lyatuu, Theopista Nsanzugwanko, Fransisca Emmanuel (Dar), John Nditi, Morogoro, Veronica Mheta, Arusha.