WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe amesema wizara yake imejiwekea mkazo mkubwa kuhakikisha mchango wa utalii katika Pato la Taifa unafikia asilimia 20 kutoka asilimia 17.5 ya mwaka jana. Kwa mujibu wa Waziri Maghembe, ongezeko la Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) halijaathiri sekta hiyo na badala yake mapato yameongezeka.

Amesema, lengo la kuweka mkazo huo ni kuhakikisha robo ya fedha za kigeni zinazoingia nchini zinatokana na pato la utalii na hilo linawezekana kwa kuwa hadi sasa kuna kasi ya ongezeko la watalii nchini.
Akihojiwa kwenye kipindi cha Tunatekeleza kinachoandaliwa na Idara ya Habari-MAELEZO na Kituo cha Televisheni cha Taifa cha TBC1, Profesa Maghembe alisema wizara imejipanga kutekeleza hilo na kuwa katika msimu huu wa utalii ulioanza wameona matokeo ya kazi ya kutangaza nchi kwenye masuala ya utalii.
“Msimu mkubwa wa utalii umeanza na tumeona matokeo ya kazi tulizofanya, watalii wanaokuja Tanzania mwaka huu ni wengi sasa, mfano kutoka Juni hadi Agosti mwaka huu ukilinganisha na kipindi hiki kwa mwaka jana, kuna ongezeko la asilimia 20 la watalii,” alisema Profesa Maghembe.
Alisema ongezeko hilo sio tu kwa watalii wanaokuja nchini, bali pia limeongeza mapato ya utalii kwa asilimia 22, na kusisitiza kuwa ongezeko la Kodi ya Ongezeko la Thamani inayotozwa kwenye huduma za utalii nchini haijaathiri watalii wanaoingia nchini.
“Ni jambo zuri kuona kuna ongezeko la watalii wanaoingia nchini, lakini pia kuna ongezeko la mapato kwa zaidi ya asilimia 22, licha ya watu kuzungumza matatizo mambo wasiyoyajua vizuri ukweli wake,” amesema Profesa Maghembe.
Akifafanua, alisema mwanzo wa bajeti mpya ya serikali kutangazwa mwaka huu na kuonesha kuwa serikali imeondoa msamaha wa kodi iliyowekwa kwenye sheria ya utalii ya mwaka 2006, ambayo ilisamehe kodi ya ongezeko la thamani kwa huduma zote za utalii.
Alisema mwaka 2015, wakati wa kuandaa bajeti ya 2015/2016 urejeshwaji wa kodi hiyo ulijadiliwa na wadau waliomba kupewa muda wa kujiandaa kwa mwaka mmoja na kwamba mwaka huu kwenye bajeti ya 2016/17 serikali ilirejesha kodi hiyo, na wadau walilalamika ilhali walikuwa wakijua hilo.
“Lakini pamoja na hilo watalii wameongezeka sana na ukweli ni kwamba watalii wanakuja Tanzania na ongezeko la kodi hiyo halijaathiri chochote, kiingilio cha kuona hifadhi ni dola 45 sasa ukiweka na VAT inakuwa dola 53,mtalii hawezi kuahirisha safari kwa sababu ya ongezeko la dola nane tu, anachotaka ni vivutio na utulivu wa nchi,” amesisitiza.
Amesema, mfano halisi ni kwamba katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita, Ubalozi wa Tanzania nchini Marekani na hata Uingereza umetoa viza kwa watalii 100 huku balozi za nchi nyingine mfano Kenya, Rwanda na Uganda ambazo zinatumia visa za Afrika Mashariki, zikitoa visa kwa watalii sio zaidi ya 10.
Kutokana na hatua hiyo, Profesa Maghembe alisema wamezungumza na Ujerumani ambao wameandaa kikosi kitakachokuja nchini kupiga picha kwenye hifadhi za taifa mbalimbali na hawatatozwa, bali watajilipia gharama za malazi kwenye hoteli za kitalii.
Alisema baada ya kazi hiyo watarudi kwao na picha hizo zitaanza kuoneshwa Desemba mwaka huu hadi Juni mwakani kwenye vituo tofauti vya televisheni katika nchi za Ujerumani, Austria na nyingine za Ulaya.
Akizungumzia watalii walioweka nafasi kwenye mashirika makubwa 100 ya ndege kwa ajili ya kufanya safari nchini, asilimia 98 ya watalii hao wametekeleza safari zao na hivyo kuifanya Tanzania kuwa nchi ya kwanza duniani kuwa na ongezeko la utalii.
Akizungumzia utoroshwaji wa wanyama hai nchini, alisema hivi sasa serikali imepiga marufuku kusafirisha wanyama hai kwenda nje ya nchi hadi hapo mfumo mzuri utakapowekwa. Alisema mwaka 2010, kulikuwa na uzembe uliosababisha wanyama hai zaidi ya 123 wakiwemo twiga, kutoroshwa.
“Twiga mzima na wanyama 123 walitoroshwa, Waziri Mkuu wakati huo, alipiga marufuku usafirishaji wanyama wakubwa na ukabaki huu wa wanyama wadogo wadogo ambao uko kwa makundi 27, lakini tumeona usafirishaji ule ulifanywa bila kuwepo na mpango mzuri,” amesema Maghembe.
Alisema wanyama waliokuwa wakisafirishwa zaidi ni pamoja na tumbili, na wadudu waitwao beetle (kombamwiko) ambao walitozwa fedha kidogo zisizo na faida kwa maslahi ya nchi, ilhali nchi wanakokwenda wanyama hao wananufaika nao kwa kuwa wanawafanyia utafiti wa dawa mbalimbali. Kuhusu ujangili, alisema serikali ilifanya mikakati dhabiti na kufanikiwa kuwakamata Malkia wa Pembe za Ndovu ambaye hivi sasa yuko gereza la Segerea.
“Tunaendelea kupinga na kudhibiti biashara na ujangili dhidi ya tembo, kwa sababu tembo wetu wanaisha, walikuwa 110,000 sasa wamepungua chini ya 50,000, wale wote tunaowakamata sasa kwa makosa ya ujangili, tunawashitiaki kwa makosa ya uhujumu uchumi,” amesema.
Alisema kwa mtu yeyote awe mkubwa au mdogo katika vita hiyo hakuna msalia mtume, wote wanaohusika watakamatwa na kushitakiwa. Aliongeza kuwa, kwamba hivi sasa ndege maalumu zisizo na rubani zinazoruka kuangalia wanyama zimesaidia kuongeza ulinzi wa wanyama hao kwa zinapiga picha na kuonesha maeneo waliyoko majangili kisha askari wanafuatilia.