Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT Wazalendo, Kabwe Zitto (katikati), akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam leo asubuhi, wakati akitoa tamko la kamati kuu ya chama hicho baada ya kufanyika kikao chake cha kawaida jana. Kushoto ni Kaimu Katibu mkuu wa chama hicho,  Juma Sanani na kulia ni Makamu Mwenyekiti Tanzania Bara, Shaban Mambo.
Taswira meza kuu. Kutoka kushoto ni Kaimu Katibu mkuu wa chama hicho,  Juma Sanani , Kiongozi Mkuu wa chama hicho, Kabwe Zitto, Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Tanzania Bara, Shaban Mambo, Makamu Mwenyekiti Tanzania Zanzibar, Ramadhan Ramadhan na Naibu Katibu Mkuu Tanzania Bara, Msafiri Mtemelwa.
Mkutano na wanahabari ukiendelea.
Waandishi wa habari wakichukua taarifa hiyo.

Na Dotto Mwaibale

CHAMA Cha ACT Wazalendo kimesema  katika kipindi cha miezi 6 tu ya kwanza ya utawala wa Rais Dk. John Magufuli uchumi wa nchi umepungua hadi kufikia asilimia nne ukilinganisha na vipindi vingine vilivyopita.

Hayo yamebainishwa na Kiongozi Mkuu wa chama hicho, Kabwe Zitto Dar es Salaam leo wakati akitoa tamko la kamati kuu ya chama hicho kuhusu hali ya nchi baada ya kikao cha kawaida kilichofanyika jana.

Kabwe alisema katika miaka 10-15 iliyopita, nchi yetu imejenga uchumi ambao umekuwa ukikua kwa kiwango cha asilimia 6-7 kwa mwaka katika kipindi chote hiki. Ukuaji huu wa uchumi ulitokana na juhudi za nchi katika kuvutia wawekezaji na kuchochea shughuli za uzalishaji mali kwa wananchi wenye kipato cha chini. 

Alisema awamu ya tano ya Serikali ya Chama cha Mapinduzi imerithi changamoto ya uchumi unaokua bila kuwafaidisha wananchi wa kawaida. Hili ndilo tulitegemea Serikali mpya ishughulike nalo. 

 " Kamati kuu yetu imeshtushwa na hali ya kuanza kudorora kwa shughuli za uchumi katika kipindi cha miezi kumi ya utawala wa awamu ya tano" alisema Kabwe

Akitolea mafano alisema taarifa za Benki Kuu zilizopo kwenye tovuti yake (Quarterly Economic Review na Monthly Economic Review) kwa robo ya mwisho ya mwaka 2015 (Oktoba?- Desemba 2015) zinaonesha kuwa kasi ya ukuaji wa Pato la Taifa ilikuwa 9%. Katika robo ya kwanza ya mwaka 2016 (Januari - Machi 2016) kasi ya ukuaji wa Pato la Taifa ilishuka hadi kufikia 5.5%. Kiuchumi, hii inamaanisha kuwa ukuaji wa shughuli za kiuchumi katika kipindi cha miezi 6 ya mwanzo ya utawala wa awamu ya tano chini ya Rais Magufuli umepungua kwa 4%!?

Alisema shughuli za uchumi zinazohusu wananchi masikini zimeshuka kutoka kasi ya ukuaji ya 10.20% katika robo ya mwisho ya mwaka 2015 mpaka 2.7% katika robo ya kwanza ya mwaka 2016, ikiwa ni punguzo la 8% ndani ya kipindi kisichozidi miezi sita. Hii inamaanisha kwamba Wananchi wetu wanazidi kudumbukia kwenye ufukara kwa kasi tangu awamu ya tano ya Serikali ya Chama Mapinduzi iingie madarakani.

Aliongeza kuwa ukuaji wa sekta ya ujenzi katika robo ya mwisho ya mwaka 2015 ulikuwa ni 13.8% lakini ukuaji wa sekta hiyo katika robo ya kwanza ya mwaka 2016 ilikuwa ni 4.30%, ikiwa ni tofauti ya takribani -10%. Hii ni kwa sababu uwekezaji katika sekta hii umeanza kushuka. 

"Kasi ya ukuaji wa sekta ya usafirishaji imeporomoka kutoka kukua kwa 14.50% robo ya mwisho ya 2015 mpaka kukua kwa 7.9% robo ya kwanza ya 2016, ikiwa ni kuporoka kwa 7% katika kipindi cha miezi 6 tu ya kwanza ya utawala wa Rais Magufuli. Kuporomoka kwa sekta ya usafirishaji itaathiri watu wengi, wakiwemo madereva, matingo, pamoja na mama ntilie wanaowauzia chakula" alisema .

Alisema kwa kuzingatia mwenendo wa hali ya uchumi katika nchi, kaamati kuu ya chama hicho wanaitaka serikali izingatie ‘’sayansi ya uchumi’’ katika kuendesha uchumi wa nchi. Uamuzi wa CCM wa kuitelekeza serikali yake kwa mwanasiasa mmoja anayedhani ndiye anayejua kila kitu na yeye kugeuka kuwa mshauri wa washauri wa uchumi badala ya washauri wa uchumi kumshauri yeye, itasambaratisha uwekezaji nchini na kuua kabisa juhudi za miaka 20 za kuvutia wawekezaji na kujenga uchumi shirikishi. 

Alisema kamati hiyo inahimiza wananchi kuzingatia kuwa msingi wa uchumi wetu ni uwekezaji kutoka ndani na nje ya nchi. Msingi wa kuvutia wawekezaji ni utawala wa sheria. Juhudi za serikali ya CCM za kuua utawala wa sheria zitaua uwekezaji na kuangamiza uchumi wa nchi. Tusiruhusu CCM iue uchumi wa nchi kwa maslahi yake ya kisiasa na viongozi wake.