Mkuu wa Wilaya ya Same Rosemary Staki Senyamule akikagua magunia yaliyokutwa yakiwa yamejazwa Rumbesa

Mkuu wa Wilaya ya Same Rosemary Staki Senyamule akizungumzia unyonyaji wanaokumbana nao wananchi kutoka kwa wafanyabiashara wanaotaka magunia yaliyojazwa Rumbesa


Gari aina ya Fuso likiwa limekamatwa mara baada ya kubainika kuwa limebeba magunia ya vitunguu ambayo yamejazwa Rumbesa



Mkurugenzi
Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Same Anna-Claire Shija akisisitiza jambo wakati wa mkutano na wananchi Wilayani humo



 Dc Staki akikagua mashamba ya wakulima mara baada ya kuzuru katika maeneo hayo




 Mkuu wa Wilaya ya Same
Rosemary Staki Senyamule akisisitiza jambo wakati wa mkutano wake na wananchi

Mkuu wa Wilaya ya Same
Rosemary Staki Senyamule pamoja na kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya hiyo wakisikiliza malalamiko ya wananchi



Na Mathias Canal, Kilimanjaro




Wakulima wa mazao mbalimbali likiwemo zao la vitunguu wametakiwa
kutofanya biashara kwa kujaza rumbesa ili kuwanufaisha wafanya biashara
ambao wanajitokeza vijijini kunua mazao kwani jambo hilo linawanyonya
zaidi wakulima na kuwanufaisha wafanya biashara.



Marufuku hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Same Mkoani Kilimanjaro
Rosemary Staki Senyamule mara baada ya kuitisha mkutano wa wananchi
katika ziara yake ya kuwahimiza kwa pamoja kujitokeza kushiriki katika
zoezi la upimaji ardhi linaloendeshwa na Halmashauri ya Wilaya ya Same.




Hata hivyo lengo mahususi la kuamua kuwapo kwa zoezi la upimaji ardhi
ni kutaka kuondoa migogoro ya ardhi iliyokithiri katika maeneo
mbalimbali Wilayani humo sambamba na kupinga kipimo cha Rumbesa
kinachowanyonya wakulima wengi nchini.



Katika mkutano huo
uliofanyika Katika Kitongoji cha Jitengeni na Mvungwe
uliwahusisha pia wataalamu wa kilimo na ardhi kutoka katika Halmashauri
ya Wilaya hiyo sambamba na wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama katika
Wilaya hiyo.



Katika mkutano huo Mkuu wa Wilaya hiyo aliwataka
wakazi wa Kijiji cha Ruvu Jiungeni kushiriki kikamilifu katika zoezi la
upimaji ardhi hivyo kuwaarifu pia wananchi wote kujitokeza katika
mashamba yao wakati wa zoezi la upimaji ili kuondoa adha inayochochea
migogoro kati ya wakulima na wafugaji.



Dc Staki alisema kuwa
wananchi wanapaswa kupinga kuzidisha kipimo halisi kinachokubalika kwani
kutofanya hivyo ni kukubali kupunjwa na kuinyima Halmashauri mapato.




Alisema kuwa wakulima wanapaswa kujiamini kwani mazao wanayolima yana
soko popote nchini hivyo kidanganywa kwa kuweka Lumbesa ni kujinyima
haki yao ya msingi katika kukabiliana na wimbi la umasikini.



Aidha kabla ya mkutano na wananchi Dc Staki alitembelea mashamba ya vitunguu na kujionea jinsi ambavyo Rumbesa inavyofungwa.




Sambamba na hayo pia Mkuu huyo wa Wilaya alimtaka mkuu wa Polisi Wilaya
ya Same Asteriko Maiga kusimamia na kulikemea suala la Rumbesa kwenye
mageti yote na endapo watawabaini wafanya biashara wanaofanya hivyo
wanapaswa kukamatwa na kuchukuliwa hatua.



Kwa upande wake Mkurugenzi
Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Same Anna-Claire Shija alisema kuwa
wananchi wanapaswa kuwa makini katika kuimarisha kilimo na kujitokeza
kwa wingi katika shughuli za maendeleo.