WAKATI vifo vya waathirika wa tetemeko la ardhi mkoani Kagera vikiongezeka na kufikia 17, uongozi wa mkoa huo umesema zinahitajika zaidi ya Sh bilioni 2.3 kwa ajili ya mahitaji mbalimbali ya waathirika, na tayari serikali jana imehamasisha na kupatikana zaidi ya Sh bilioni 1.4.
Kati ya fedha hizo zilizopatikana, Sh milioni 700 zilikuwa ahadi, fedha taslimu Sh milioni 646, Dola za Marekani 10,000, Euro 10,000 na mifuko 2,800 ya saruji.
Kampuni za mafuta ya Oilcom, GBP na Moil, zimejitolea kujenga shule mbili za sekondari zilizoathiriwa na tetemeko hilo. Shule hizo zimefungwa. Jumamosi iliyopita, saa 9.27 alasiri mji wa Bukoba ulikumbwa na tetemeko la ardhi, ambalo nguvu ya mtetemo wake ulikuwa ni 5.7 kwa kutumia skeli ya “Ritcher”.
Ukubwa huo ni wa juu kiasi cha kuleta madhara makubwa ikiwemo kuanguka nyumba, nyingine zimepata nyufa, watu 17 wamekufa, na mamia wawamejeruhiwa.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Salum Kijuu alisema, baada ya Kamati ya Maafa ya Mkoa na Kamati ya Maafa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, wamefanya tathmini ya haraka na kubaini mahitaji kwa wananchi walioathirika.
Kijuu aliwaomba wananchi, wadau na marafiki walioguswa na janga hilo katika mkoa na nje ya mkoa, wachangie michango yao kupitia akaunti ya maafa iliyopo katika benki ya CRDB yenye namba 0152225617300 na kwa walioko nje watumie Swift code:CORUtztz, huku akiomba watakaowiwa kutoa wawasiliane na ofisi yake kwa maelezo zaidi.
Alitaja mahitaji ya muhimu ambayo yanahitaji kwa haraka ni dawa, tiba na vifaa tiba, vifaa vya ujenzi mabati 90,000 yenye gharama ya Sh bilioni 1.7, saruji mifuko 9,000 yenye thamani ya Sh milioni 162, mbao zenye thamani ya Sh milioni 450 na misumari yenye thamani ya Sh milioni 12 ambapo jumla ni Sh bilioni 2.3. Majaliwa achangisha bil 1.4/- Wakati Kijuu akisema hayo, Majaliwa amehamasisha wafanyabiashara pamoja na mabalozi, kuchangia na kuchangisha zaidi ya Sh bilioni 1.4.
Katika hafla fupi iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam, Waziri Mkuu Majaliwa alieleza kuwa kutokana na tetemeko hilo kubwa, imelazimu serikali kuzifunga shule mbili za sekondari zilizoharibiwa vibaya za Nyakato na Ihungo. Waziri Mkuu alisema tetemeko hilo ni kubwa ambalo halijawahi kutokea nchini, hivyo haikutarajiwa na wala hakukuwa na maandalizi ya kukabiliana na hali kama hiyo.
Alisema mpaka jana watu 17 walikuwa wamefariki dunia huku 253 wakijeruhiwa na 145 walikuwa wako katika hospitali huku vitu vingi pamoja na miundombinu vikiharibika.
Katika miundombinu ya shule nne za Nyakato, Ihungo, Kashenge na Buhembe, zimeharibika ikiwemo vyoo, nyumba za walimu, kumbi za shule na mabweni yameharibika kabisa pamoja na hospitali na vituo vya afya navyo vimeharibika.
Alisema kuna baadhi ya sehemu hali ni mbaya na wanahitaji msaada ambapo nyumba 840 zimeanguka kabisa chini huku nyumba na majengo 1,264 yakiwa na nyufa na kamati ya maafa katika mkoa pamoja na viongozi wake wanaendelea kufanya tathmini ya kiasi cha hasara iliyopatikana.
Alisema serikali imefanya juhudi katika kukwamua maisha ya wananchi wake na mawaziri watatu wako mkoani humo kuangalia namna ya kukabiliana na majanga hayo ambao ni Waziri wa Ujenzi, Profesa Makame Mbarawa, Elimu Profesa Joyce Ndalichako na Waziri wa Nchi katika ofisi yake, Jenista Mhagama.
Alisema kupitia kitengo cha maafa katika Ofisi ya Waziri Mkuu wamefungua akaunti hiyo katika benki ya CRDB huku wakiendelea na maandalizi ya kupata namba za kuchangia kwa simu ya mkononi huku akiwashukuru wabunge walioamua kuchangia maafa hayo kwa kutochukua posho zao za siku ya jana.
Mabalozi, Wafanyabiashara Mkuu wa Jumuiya ya Mabalozi, Balozi wa Zimbabwe nchini, Edzai Chimonyo alisema kutokana na tarifa hiyo kuwa ya ghafla na wako sehemu mbalimbali duniani watakusanyika na kuwasilisha michango yao. Lakini, hata hivyo, balozi mbalimbali zilijitokeza kuwasilisha michango yao ikiwemo Ubalozi wa China, uliotoa Sh milioni 100, wafanyabiashara wa Kichina walitoa Sh milioni 100 na Ubalozi wa Kuwait Sh milioni 50.
Pia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, ilitoa mchango wa wafanyakazi wake Sh milioni 10 huku ikiandaa matembezi ya kuchangisha fedha zaidi kwa waathirika wa tetemeko hilo yatakayofanyika Jumamosi wiki hii. Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dk Azizi Mlima alisema wameanza kwa kukabidhi fedha hizo ambazo ni mchango wa wafanyakazi, lakini Jumamosi wamealika wadau mbalimbali katika matembezi hayo watakayochangia zaidi.
Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Reginald Mengi alisema wafanyabiashara wako pamoja katika kuhakikisha wanakabiliana na tatizo hilo na kuipongeza serikali kwa hatua za haraka walizochukua kukabili majanga hayo.
Mengi alichangia Sh milioni 110, Kampuni ya Mohammed Enterprises (MeTL) kupitia kwa Ofisa Mtendaji Mkuu wake, Mohamed Dewji ilitoa Sh milioni 100, Kampuni ya Bia (TBL) Sh milioni 100, Chama cha Wauzaji Mafuta kwa Rejareja Sh milioni 250 huku Umoja wa Waagizaji Mafuta ukiahidi kuchangia baada ya kikao watakachokaa leo.
Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage alishukuru kwa wafanyabiashara na mabalozi kwa michango hiyo na kuomba ipatikane kwa haraka ili kusaidia wananchi wa mkoa huo kurejea katika maisha yao ya kawaida.
RC afafanua zaidi
Kijuu alisema shule za sekondari Ihungo na Nyakato zimefungwa kwa muda wa wiki mbili kutokana na miundombinu yake kuharibika, ambayo ni madarasa, vyoo na mabweni baada ya kuta kuanguka au kupata nyufa kubwa na kuonekana haifai kutumika tena, huku wanafunzi wakiruhusiwa kurudi katika familia zao baada ya kuonekana kuathirika kisaikolojia.
Alisema Kamati ya Maafa kuanzia sasa, inajenga miundombinu hiyo ndani ya muda wa wiki mbili ili irudi katika hali yake ya kawaida na wanafunzi warudi shuleni na kuendelea na masomo yao kama kawaida.
Pia serikali imefanya juhudi za kuleta wataalamu wa afya ambao ni madaktari bingwa sita kutoka katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando iliyoko jijini Mwanza ili kutoa msaada kwa wagonjwa wanaohitaji msaada zaidi wa kitabibu huku Ubalozi wa nchi ya China ukileta waganga wa kusaidia matibabu kwa waathirika hao.
Aidha, katika uchunguzi uliofanywa na wataalamu kutoka Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST) kuhusu tetemeko hilo, walibainisha sababu kuwa ni kitovu cha tetemeko hilo kuwa kiko chini sana ya ardhi kwa kutafsiri umbile la tetemeko hilo lililonakiliwa na vituo vya kupima matetemeko ya ardhi ambapo inaonekana kuwa limetokana na misuguano ya mapande makubwa ya ardhi iliyopasuliwa mithili ya mipasuko kwenye Bonde la Ufa.
Pia Serikali ya Mkoa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali hasa wataalamu kutoka GST wameandaa vituo mbalimbali katika mkoa ili kutoa elimu jinsi ya kufanya mazoezi ya kuchukua tahadhari kabla ya tetemeko, wakati wa tetemeko na baada ya kutokea ili kujizoesha kwani mara nyingi wakati wa matukio kama ya majanga kama hayo watu huchelewa kuchukua uamuzi wa haraka kujinusuru kwamba wafanye nini. Taarifa ya serikali bungeni
Akisoma taarifa ya serikali bungeni, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa - Tamisemi), George Simbachawene kwa niaba ya Waziri Mkuu, alisema tetemeko hilo lenye ukubwa wa 5.7 katika vipimo cha “Ritcher”, kufikia jana lilisababisha vifo vya watu 17 na kujeruhi watu 252, kati yao 169 wakiwa wamelazwa hospitalini.
Alisema nyumba za makazi zilizoanguka ni 840 huku nyumba za makazi zenye nyufa zikiwa 1,264 na majengo ya taasisi yaliyoripotiwa kuanguka ama kupata nyufa ni 44. Kutokana na athari hizo, serikali imetangaza kuchukua hatua kadhaa, ikiwemo ya kuokoa na kuwapeleka hospitalini waathirika kwa ajili ya matibabu.
Imewapatia pia makazi ya muda baadhi ya wananchi ambao nyumba zao zimeathirika. Serikali pia imeongeza nguvu ya madaktari bingwa 15 kutoka mkoani Mwanza ili wasaidie kutoa huduma za haraka kwa waathirika, huku ikiwahamasisha wananchi wasaidiane kila inapowezekana.
Alisema serikali pia imeelekeza wanajiolojia kutoa maelekezo ya kisayansi ili kuwatoa hofu wananchi kuhusu hali hiyo.
Taarifa hiyo imesema Serikali inaendelea kuhakikisha hatua za dharura zinachukuliwa kwa kushirikiana na wadau wengine kuhakikisha kuwa hatua za muda mfupi na muda mrefu zinatambuliwa na kutekelezwa ili kuwasaidia waathirika.
Wakati hayo yakiendelea, Serikali inaendelea kufanya tathmini ya athari zilizosababishwa na tetemeko la ardhi. Kutokana na janga hilo, serikali imewaomba wadau wa ndani na nje wanaotaka kuchangia waathirika, wawasiliane moja kwa moja na Ofisi ya Waziri Mkuu na Kamati ya Maafa ya Mkoa wa Kagera, huku ikionya watu kuacha kutumia maafa hayo kujinufaisha.
“Wananchi mnaombwa kuwa wavumilivu na kuendelea kushirikiana na Serikali katika kutatua tatizo ambalo limeipata nchi ili wananchi waendelee kupata huduma kulingana na athari za tetemeko,” alisema Simbachawene.
Wabunge waunga mkono
Kutokana na kuguswa na tukio hilo, wabunge jana waliunga mkono juhudi za Serikali na wameridhia kwa kauli moja kukatwa posho yao ya siku moja, sawa na Sh 220,00 kila mmoja ili kuchangia maafa hayo.
Bunge lina wabunge 389.
Uamuzi huo ulitokana na hoja ya Mbunge wa Mlalo, Rashid Shangazi (CCM) aliyeomba Bunge liahirishe mjadala uliokuwa mezani wa Muswada wa Sheria ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu 2016 na Muswada wa Sheria ya Usimamizi wa Wataalamu wa Kemia 2016 ili kujadili tukio la tetemeko la ardhi Kagera ambalo ni la dharura.
Alipendekeza pia wabunge wajadili kwa muda wa nusu saa suala hilo pamoja na kuchangia posho yao ya siku moja. Naibu Spika, Dk Tulia Ackson alipokea ombi la Shangazi na kusema kuwa ataruhusu mjadala huo kwani kanuni zinaruhusu.
Hata hivyo, alisema kitakachojadiliwa ni hoja ya dharura na mchango wa wabunge, lakini sio kujadili Kauli ya Serikali kuhusu tetemeko hilo iliyotolewa na Waziri Simbachawene kwa niaba ya Waziri Mkuu.
Hata hivyo, katika hali ya kushangaza, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (Chadema) alionesha utovu wa nidhamu mbele ya Bunge na Naibu Spika kwa kumnyooshea kidole Dk Tulia jambo lililofanya avunje Kanuni ya 74 inayomtaka mbunge kutoonesha dharau yoyote kwa aliyekalia kiti cha uongozi bungeni.
Mdee atia doa Naibu Spika alimkanya Mdee, akisema, “Mheshimiwa Halima Mdee acha kuninyooshea kidole, acha kunyoosha vidole, huo ni utovu wa nidhamu kwa kiti… hebu Halima Mdee uwe na heshima kidogo, hebu kuwa na heshima kidogo.”
Baada ya kauli hiyo ya onyo, Halima alionekana kususa na kutoka nje ya Bunge wakati wabunge wakianza kujadili hoja ya dharura iliyoletwa mezani na Shangazi. Akichangia Shangazi alianza kwa kupendekeza wabunge kuchangia posho yao ya siku hiyo ambayo ni Sh 220,000 ili kuwafariji wananchi waliopatwa na tatizo la tetemeko hasa manispaa ya Bukoba.
“Tunamshukuru Mungu tukio limetokea mchana, kama ingekuwa usiku huenda maafa yangekuwa makubwa zaidi. Tukio hili litufunze kuweka kanda maalumu zinazoshughulikia maafa ili tatizo linapotokea litatuliwe haraka,” alisema.
Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche (Chadema) alisema tukio hilo la tetemeko liwaunganishe wabunge wa kambi zote, kwani Bunge ni chombo cha wananchi na kutaka wabunge bila kujali itikadi kusaidia kuielekeza serikali nini cha kufanya kukabiliana na maafa hayo.
Aliunga mkono hoja kuchangia posho ya siku ya jana, ingawa alisema tayari kwa upande wao wapinzani walishachangishana Sh 100,000 kila mmoja kwa ajili ya kusaidia waathirika wa tukio hilo.
Mbunge wa Viti Maalumu, Zainab Vullu (CCM) naye aliunga mkono hoja ya kuchangia posho yao ya siku na kuongeza suala hilo limegusa hisia za watu na kuonya wanasiasa kutotumia maafa hayo kujiinua kisiasa.
Vullu aliipongeza serikali kwa juhudi zake tangu kutokea kwa tukio hilo, lakini alisisitiza haja ya kutolewa elimu zaidi ya kukabiliana na maafa na njia za kuokoa watu yanapotokea matukio ya dharura kama hilo la tetemeko la ardhi.
Mbunge wa Muleba, Profesa Anna Tibaijuka (CCM) alisema ametoka Bukoba na kwamba ameshuhudia hali ilivyo mbaya katika maeneo yaliyoathirika na tetemeko hilo na kuongeza kuwa ni mkono wa Mungu tu ndio umeepusha maafa kuwa makubwa zaidi.
Alisema suala hilo sio la kisiasa na kwamba wananchi wanahitaji faraja na kutaka kama taifa Watanzania wawe wamoja bila kujali itikadi zao na kutaka tathmini ifanywe kitaalamu zaidi.
Alitaja baadhi ya maeneo aliyotembelea na kujionea athari kubwa ikiwemo Manispaa ya Bukoba, ambapo alisema kati ya nyumba 10 tatu zimeharibika kabisa, hivyo inahitajika tathmini ya kitaalamu sana ili kubaini iwapo eneo husika linafaa tena kujenga au watu wanatakiwa kuhama.
Mbunge wa Buchosa ambaye pia ni Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk Charles Tizeba alisema tetemeko limeleta uharibifu mkubwa katika mkoa wa Kagera ingawa maeneo mengine yameguswa ikiwemo Mwanza, Geita na Shinyanga.
Mara baada ya wabunge hao kumaliza kuchangia, Naibu Spika Dk Tulia alilihoji Bunge ambalo kwa pamoja liliunga mkono kutoa posho kwa ajili ya kuchangia waathirika wa tetemeko Bukoba.
Akishukuru kwa niaba ya Waziri Mkuu, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi aliwashukuru wabunge kwa kutoa mkono wa faraja na kuungwa mkono na Bunge zima.
“Hili ni jambo letu sote, kwani ni utamaduni wa Watanzania kusaidiana na kuchangiana yanapotokea majanga kama haya. Serikali inaahidi mchango wenu utawafikia walengwa kama ilivyokusudiwa,” alisema.
Aliongeza kuwa serikali inalichukulia suala hilo kwa ukubwa wake na ndio maana, Rais John Magufuli aliahirisha safari ya kikazi Lusaka, Zambia na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa yuko Dar es Salaam akikutana na wataalamu na wadau wa ndani na kimataifa kuona namna gani walikabiliana na maafa ya tukio hilo.
Athari Bukoba
Alisema Manispaa ya Bukoba ndiyo iliyoathiriwa zaidi, kwani imepoteza watu 15 waliokufa kutokana na tetemeko hilo, huku majeruhi wakiwa 142 kati ya 252. Aidha, nyumba 753 zimeanguka katika Manispaa ya Bukoba pekee, huku nyumba 1,037 zikipata nyufa.
Kwa upande wa taasisi alisema, shule kongwe ya Sekondari Ihungo imelazimika kufungwa kutokana na uharibifu mkubwa, kwani tetemeko limeangusha ukumbi wa shule, bweni moja huku mengine sita yakitajwa kuharibika vibaya na kutofaa kukaliwa na wanafunzi.
Aidha, madarasa 16 yamebomoka, huku vyoo 25 vikiharibiwa sambamba na mabafu mawili. Nyumba tatu za walimu zimeanguka na nyingine 17 zikipata nyufa.
Taarifa hiyo imeeleza kanisa na msikiti shuleni hapo vimebomoka, wakati maabara tatu zimepata nyufa ilhali mtego wa Radi moja umeanguka. Shule nyingine iliyofungwa ni Nyakato ambayo mabweni yake sita yameharibika na hayawezi kukaliwa huku mengine manane yakipata nyufa.
Aidha, vyumba vitano vya madarasa vimeharibika na vingine 15 vikipata nyufa. Pia tetemeko limeharibu jengo moja la utawala, nyumba nane za walimu ambazo hazifai kutumia wakati nyingine 17 zimepata nyufa. Athari za tetemeko zimezikumba pia halmashauri za wilaya ya Bukoba, Missenyi, Muleba, Karagwe na Kyerwa.
|
0 Comments