WANAFUNZI wa Kidato cha Sita Shule ya Sekondari Usevya wilayani Mlele Mkoa wa Katavi, wanadaiwa kuwashambulia kwa kuwacharaza viboko walimu wao wawili miongoni mwao akiwemo Makamu Mkuu wa Shule hiyo, Makonda Ng’oka “Membele'‘ (34) ambaye ameng’olewa meno matano kwa kipigo hicho.
Walimu hao wawili wamedai kuwa hawako tayari kuendelea kufundisha katika shule hiyo huku wakisisitiza kuwa ni fedheha kwao kucharazwa viboko na wanafunzi wao wenyewe ambapo Mwalimu Gabriel Kambona aliachwa na ngeu kichwani.
Mei mwaka huu, Ng’oka “Membele” alifikishwa katika Mahakama ya Mkoa wa Katavi kwa tuhuma za kumlawiti mwanafunzi wake akidaiwa kutenda kosa hilo kati ya Novemba 2015 na Aprili mwaka huu.
Ilisemekana kukamatwa na kufikishwa mahakamani kwa Makamu Mkuu huyo wa shule hiyo kulifuatia wanafunzi wa kiume wanaosoma Kidato cha Tano sasa wako Kidato cha Sita katika shule hiyo kumkataa na kutishia kuandamana kupinga vitendo vyake vya kuwalawiti wanafunzi wake.
Wanafunzi hao walidai kuwa mwalimu huyo amekuwa akiwalawiti baadhi yao ikiwa ni adhabu mbadala wanapobainika kufanya makosa shuleni hapo.
Hata hivyo, baada ya kutopatikana ushahidi wa kumtia hatiani Ng’oka, Julai 27, mwaka huu Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Wilaya ya Mpanda ilimwachia huru.
Mwalimu Ng’oka aliripoti kwenye kituo chake cha kazi shuleni Usevya Agosti Mosi mwaka huu ambako kurejea kwake shuleni hapo kunadaiwa kuamsha hasira kwa baadhi ya wanafunzi wa Kidato cha Sita wakidai hawapo tayari kumwona mwalimu huyo na familia yake shuleni hapo.
Akizungumza na wanahabari jana mjini hapa, Ng’oka alidai kuwa hayuko tayari kuendelea kufundisha kwenye shule hiyo akihofia usalama wake na kutokana na kipigo alichokipata cha kushambuliwa na baadhi ya wanafunzi wake wa kidato cha tano na cha sita wakati akiwa nyumbani kwake na familia yake. Akisimulia mkasa huo, alisema Agosti 12, mwaka huu usiku alikuwa nyumbani kwake shuleni hapo pamoja na familia yake pamoja na mwalimu mwenzake, Gabriel Kambona aliyekuwa amemtembelea.
“Ghafla, saa mbili usiku nikiwa maliwatoni nikioga lilitokea kundi la wanafunzi wa kidato cha tano na sita wakiwa na silaha za jadi kama vile fimbo, marungu, mawe na matofali na kuanza kuishambulia familia yangu pamoja na mwalimu Kambona,” alieleza na kuongeza kuwa alilazimika ‘kuchomoka’ bafuni baada ya kusikia mayowe yaliyokuwa yakipigwa na familia yake wakiomba msaada. Alipofika sebuleni alishuhudia wanafunzi hao wakiishambulia familia yake kwa kuwacharaza viboko.
“Ndipo walinigeukia na kuanza kunishambulia kwa kunipiga kwa marungu na fimbo hadi nikapoteza fahamu nilizinduka nikiwa nimelazwa kwenye Kituo cha Afya Usevya na kubaini kuwa nimepoteza meno yangu matano huku nikiwa nimejeruhiwa vibaya kichwani. Baadaye nilihamishiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Mpanda ambako nililazwa wiki moja na nusu kwa matibabu na sasa nimepewa rufaa niende Hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar kwa matibabu zaidi,” alieleza.
Alidai kuwa uhasama baina yake na wanafunzi hao umedumu kwa muda mrefu, lakini anashangaa uongozi wa Halmashauri ya Mpimbwe na Wilaya ya Mlele umeshindwa kumpangia kituo kingine cha kazi na kuchukua hatua yoyote kwa wanafunzi hao licha ya kupeleka majina yao kwa kuwa anawafahamu wote waliohusika.
Mwalimu Kambona alidai kuwa hayuko tayari kuendelea kufundisha kwenye shule hiyo kwamba kitendo cha kupigwa na wanafunzi wake kimemfedhehesha.
Kwa mujibu wa mwalimu huyo, walimu wa shule hiyo waliketi baada ya kutokea kwa tukio hilo, na walifikia maamuzi kuwa wanafunzi wote waliobainika kushiriki kuwashambulia walimu wao wasimamishwe shule akidai kuwa uongozi wa Halmashauri ya Mpimbwe na Wilaya ya Mlele ulipinga.
“Nimeandika barua ya kuomba uhamisho kwani nia aibu kwangu kuendelea kufundisha wanafunzi ambao wamenishambulia na kunitoa ngeo kichwani ….. siku hiyo ya tukio niliibiwa simu mbili za kiganjani lakini jana nimefanikiwa kuikamata simu moja kwa mwanafunzi wa kidato cha tano anayeitwa , Alex Maiko Makona na tayari amemfikisha katika Kituo cha Polisi cha Usevya,” alidai.
Mwenyekiti wa Chama cha Walimu (CWT) Mkoa wa Katavi, Gregori Mshota alisema tayari chama chake kimeanza kuwasiliana na uongozi wa Halmashauri ya Mpimbwe na uongozi wa Wilaya ya Mlele ili kuhakikisha mwalimu huyo anakuwa salama.
Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu akiwa nje ya mkoa, Ofisa Elimu wa Mkoa wa Katavi, Ernest Hinju alidai kuwa suala hilo lipo ofisini kwake na wameanza kulitafutia ufumbuzi. “Jambo hili linahitaji ushirikishwaji wa vyombo mbalimbali ikiwemo Bodi ya Shule ya Sekondari ya Usevya,” alieleza.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipokuwa katika ziara mkoani Katavi mwezi uliopita, mke wa mwalimu Ng’oka alitinga kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kijijini Maji Moto akiwa na bango lenye malalamiko ya kutishiwa usalama wa maisha wa familia yake, na Waziri Mkuu alimwagiza Kamanda wa Polisi wa Mkoa kushughulikia malalamiko hayo.
|
1 Comments