Follow us: Subscribe via RSS Feed Connect on YouTube Connect on YouTube
Maganga One Blog kwa habari za kitaifa,kimataifa,burudani na michezo kila siku. Tutumie habari na matukio yoyote kwa email yetu ya magangaone@gmail.com

Sep 2, 2016

Madalali wa NHC wavamia ofisi za Mbowe

MADALALI wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Foster Auctionare wamevamia ofisi za Kampuni ya Free Media, wachapishaji wa gazeti la Tanzania Daima na ukumbi wa disco wa Billicanas na kutoa nje samani na vifaa mbalimbali.
Hatua hiyo inatokana na madai kuwa, mpangaji wa jengo hilo lililopo katika mtaa wa Mkwepu na Indira Gandhi, jijini Dar es Salaam, Freeman Mbowe, anadaiwa Sh bilioni 1.172 na Shirika hilo la Nyumba la Taifa.

Tukio la kutoa vifaa lilianza mapema jana asubuhi. Katika eneo la tukio, madalali wa NHC walionekana wakitoa nje samani katika ofisi zilizoko katika jengo hilo, ikiwemo ya gazeti hilo na vifaa vingine katika eneo la ukumbi wa disco wa Billicanas.
Akizungumza wakati madalali wakiendelea kutoa vitu nje, Meneja wa kitengo cha Madeni kutoka NHC, Japhet Mwanasenga alisema mpangaji wa jengo hilo anadaiwa kiwango hicho cha fedha na hajalipa kuanzia miaka ya 90.
Alisema kutokana na kutokulipa fedha hizo, licha ya kupewa notisi, ndio maana Shirika limeamua kuingia na kutoa vitu nje ili aweze kulipa. Alisema mpangaji huyo, aliambiwa na alipewa notisi na NHC ya siku 30 pamoja na notisi ya dalali lakini hakulipa deni ndani ya muda huo.
“Sasa hakuna namna nyingine usipolipa deni lazima uondolewe katika jengo, ni fedha za miaka mingi kuanzia miaka ya 90,” alisema Mwanasenga. Alisema baada ya kumhamisha kwa lazima, wataendelea kufanya utaratibu wa kumdai.
Kuhusu vifaa, alisema vinaenda kwa dalali ambaye ataomba kibali NHC juu ya kuviuza vifaa hivyo baada ya siku 14 kama deni halitalipwa. Kuhusu ubia katika upangaji katika jengo hilo, Mwanasenga alisema hakuna suala kama hilo na NHC inamhesabia kama mpangaji wa kawaida.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa kampuni hiyo ya udalali, Joshua Mwaituka alisema wao watahifadhi vifaa hivyo katika ghala lililopo Buguruni, jijini humo na ndani ya siku 14 wakipata idhini kutoka NHC wataviuza.
Kwa muda wote, kazi ya kuhamisha ilipokuwa ikiendelea hadi saa 8 mchana, mpangaji wa jengo hilo hakufika katika eneo la tukio kuzungumzia suala hilo, huku kazi ya kuhamisha ikiendelea.
Mwishoni mwa Agosti, NHC kupitia Mkurugenzi Mkuu, Nehemia Mchechu, ilitangaza kuwaondoa wadaiwa wote sugu wanaoishi katika nyumba za shirika hilo. Mchechu alisema pamoja na jengo hilo, linalomilikiwa na Mbowe, Shirika linazidai taasisi za umma, binafsi na watu binafsi jumla ya Sh bilioni 15.

Share this article :

0 Maoni:

 
Maganga One Blog © Copyright 2017. All Rights Reserved.

Powered by Maganga One.
Back to TOP