Jua lilivyopatwa Dar es Salaam
HISTORIA imeandikwa katika kijiji cha Ihanga katika kata ya Rujewa wilayani Mbarali mkoa wa Mbeya, baada ya tukio la kihistoria la kupatwa kwa jua, kushuhudiwa kwa asilimia kubwa mjini hapa jana.
Pamoja na eneo la Rujewa na Wanging’ombe mkoani Njombe ambako asilimia 90 ya tukio hilo ilionekana vizuri kuliko maeneo mengine Afrika, pia jua lilionekana ingawa si vizuri sana katika maeneo ya Rukwa na Katavi na nchi ya Madagascar.

Maelfu ya watu kutoka ndani na nje ya nchi, walijitokeza kushuhudia tukio hilo la kihistoria. Baadhi yao walianza kwanza kutambika kimila, wengine kwenda kanisani na msikitini kwa lengo la kumshukuru Mungu kwa kukiinua kijiji hicho na wilaya nzima kutambulika zaidi duniani.
Tukio hilo lilianza saa 4.15 asubuhi jua hilo lilianzwa kupatwa kitendo kilichoamsha hamasa kwa wananchi ambao walianza kuazimana miwani. Wakati kwa macho ya kawaida jua hilo lilionekana kawaida, lakini kwa kutumia miwani hiyo maalumu kipande cha mwezi kilionekana kikianza kuziba sehemu ya jua hali iliyofanya miale ya jua katika eneo hilo kuanza kufifia.
Kadri muda ulivyosogea ndivyo hali ya hewa ilivyobadilika kwa mwanga na ukali wa jua ulianza kufifia. Saa 5.25 asubuhi jua lilifichwa na mwezi kwa takribani nusu yake na kijiji hicho kikawa kimefunikwa na sehemu kidogo ya kivuli cha mwezi.
Majira ya saa 5.50 asubuhi jua hilo lilifikia kilele cha kufunikwa na mwezi na kubakia eneo la pete. Eneo hilo liligubikwa na mwanga hafifu, wakati katika hali ya kawaida mida hiyo ya saa sita jua huwa kali, lakini Rujewa kulibadilika na kuwa kama saa 12 jioni.
Hali ya hewa ilibadilika na baridi kuanza kupiga hali iliyosababisha umati mkubwa wa washuhudiaji kukimbilia makoti. Hali katika eneo hilo ilizizima kila mtu akitaka kushuhudia zaidi tukio hilo la kihistoria.
Hata hivyo, jua hilo lilidumu katika kilele kwa sekunde kadhaa kwani miale ya jua ilianza kujitokeza na mwezi kuonekana kusogea na kuliachia jua. Jua hilo lilipatwa kwa muda wa saa nne kuanzia saa 4.15 mpaka saa 8.45.
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makala, Mbunge wa Mbarali, Haroon Pirmohamed na Mwanasayansi mwenye taaluma ya Astonomia na Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria Tanzania, Dk Noorali Jiwaji ndio walioongoza maelfu ya watu hao, kushuhudia tukio hilo la kupatwa kwa jua linalotokea kwa nadra nchini.
Alfajiri watu walianza kufurika katika kijiji hicho kinachozalisha mchele kwa takribani asimia 67 nchini, na kujikusanya kwenye eneo lililoandaliwa na wanasayansi ambalo lilikuwa maalumu kwa ajili ya kushuhudia tukio hilo.
Kadri muda ulivyozidi kwenda ndivyo umati mkubwa wa washuhudiaji ulizidi kuongezeka na hatimaye majira ya saa nne viongozi wa mkoa na wilaya nao waliwasili.
Wananchi waliokusanyika katika eneo hilo walipatiwa miwani maalumu zilizowawezesha kutazama jua hilo bila kupata madhara. Kutokana na wingi wa watu waliojitokeza kushuhudia jua hilo miwani zilizotengwa hazikutosheleza na kuibua malalamiko.
Dk Jiwaji wakati akiwaelezea wananchi kuhusu kinachoendelea kila baada ya muda alisema hali hiyo inatokana na mzunguko wa kawaida wa sayari za jua, dunia na mwezi. Alisema jua hupatwa baada ya sayari hizo kujipanga katika mstari mmoja huku mwezi ukiwa katikati na hivyo kuziba takribani asilimia 97 ya miale ya jua inayomulika duniani.
“Hili ni tukio la kihistoria si watu wengi wamelishuhudia, mara yangu ya kwanza kuliona ilikuwa mwaka 1980 katika eneo la Lembeli, wilayani Mwanga mkoani Kilimanjaro. Tangu nimeshuhudia kipindi hicho kwa kweli ni jambo ambalo halijanitoka. Hii ndio sayansi inayofundishwa kila siku,” alisisitiza.
Kitendo hicho cha jua kuwa katika hali ya kipete ilidumu kwa sekunde chache kwani mwezi huo ulianza kuliachia na miale ya jua ikaanza kuonekana tena katika kijiji hicho huku wananchi wakiendelea kufuatilia kila hatua.
Dk Jiwaji alisema wakati jua likiwa kwenye kilele cha kupatwa, hali ya hewa hubadilika, mchana unageuka kuwa kama jioni na anga nzima inakuwa haina hata wingu moja zaidi ya mwanga hafifu wa jua unatokana na kipete hicho.
Mara kadhaa mwanasayansi huyo amekuwa akilazimika kuwaonya wananchi na wadau wote waliofurika katika kijiji hicho, kutoliangalia jua hilo kwa macho yao ya kawaida na badala yake watumie miwani hizo maalumu ili wasiathirike.
Gazeti hili lilishuhudia kwenye eneo hilo, baadhi ya vijana wakiwa na vifaa mithili ya mikanda inayotumika kwenye mikanda ya kaseti na kuiuza kwa Sh 500 wakiwaaminisha wananchi kuwa ni sehemu ya miwani hizo za kuangalizia jua hilo wakati likipatwa.
Baadhi ya wananchi wa Rujewa waliozungumzia tukio hilo, wengi wao walikiri kuwa ni mara yao ya kwanza kushuhudia na kubainisha kuwa ndio maana viongozi wa kijiji hicho waliamua kutambika ili kutoa shukrani kwa tukio hilo kutokea katika kijiji hicho.
Mkazi wa eneo la Mbaruku wilayani Mbarali, Juma Mgeni alisema alfajiri ya jana wazee hao walidamkia kutambika kimila huku wakazi wengine wa eneo hilo wakienda kwenye nyumba za ibada kanisani na msikitini kwa ajili ya kutoa shukurani.
“Sisi tunaamini kuwa Rujewa na Mbarali kwa ujumla tumebahatika sana, tunatamani tukio hili litokee kila siku. Tunaamini kuwa ni bahati kijiji chetu kuwa sehemu ya tukio kubwa la kisayansi kama hili ndio maana tumeomba na kushukuru,” alisema Mgeni.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Rujewa, Olipa Mbupa alisema tukio hilo limetoa fursa nzuri kwa wanafunzi wa kijiji hicho na wote waliokwenda kulishuhudia kwa kuwa suala la kupatwa kwa jua limekuwa likifundishwa kinadharia na sasa wamelishuhudia kwa vitendo.
Alisema tukio hilo si muhimu pekee kwa wanafunzi hao, bali hata kwa walimu kwani anaamini ni walimu wachache tu ndio waliowahi kushuhudia kupatwa kwa jua huku akijitolea mfano yeye mwenyewe kuwa aliwahi kushuhudia tukio hilo mwaka 1975 akiwa na umri wa miaka sita na wala halikumbuki vizuri.
Kwa upande wa mwanafunzi wa kidato cha tatu katika shule ya sekondari Rujewa, Isaya Sanga alisema amefurahi kushuhudia tukio hilo moja kwa moja kwani ni siku kadhaa tu zilizopita ndio wamefundishwa suala la mzunguko wa sayari katika somo la Jiografia.
Meneja Mawasiliano wa Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (Tanapa), Pascal Shelutete alisema katika kutumia fursa ya tukio hilo, wamefungua mlango wa Ikoge kwa ajili ya kuwezesha wakazi wa Mbarali, Mbeya na mkoa mpya wa Songwe kuingia katika Hifadhi ya Taifa ya Ruaha.
Shelutete alisema hapo awali, wakazi wa maeneo hayo walilazimika kuingia katika hifadhi hiyo kupitia Iringa mjini lakini sasa wanaweza kutumia mlango huo na kuwarahisishia kufanya utalii wa ndani. Aidha, alisema takribani watalii 30 waliwasili nchini kupitia Mbeya kwa ajili ya kushuhudia tukio la kupatwa kwa jua.