WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amewaomba viongozi wa dini zote kutumia nyumba za ibada, kuhamasisha waumini wao umuhimu wa kulinda na kudumisha amani na utulivu uliopo nchini.
Amesisitiza kuwa Serikali itadumisha amani na utulivu nchini kwa nguvu zote ili Watanzania wawe na uhakika wa kuendelea kufanya kazi zao za kuwaingizia kipato na kuwaletea tija. Waziri Mkuu alisema hayo wakati akizungumza na waumini wa dini ya Kiislamu baada ya kumaliza swala ya Idd el Haji kwenye viwanja vya Mwembe Yanga, Temeke Dar es Salaam jana. Akizungumza kwenye Baraza la Idd alisema;
"Serikali itaendelea kuimarisha ulinzi katika maeneo yote nchini. Wito wangu kwa viongozi wa dini msisitize waumini juu ya utunzaji wa amani pamoja na kukemea vitendo viovu ili Taifa lizidi kusonga mbele".
Majaliwa aliwasisitiza wananchi kuendelea kuwaombea mahujaji waliopo Makka na Madina nchini Saudi Arabia, wakiendelea na Ibada ya Hija warudi salama.
Pia Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo, kuwaomba wananchi kuwasaidia kwa hali na mali watu waliokumbwa na tetemeko la ardhi mkoani Kagera, ambako jumla ya watu 16 walikufa, wengine 253 kujeruhiwa na maelfu ya wananchi kukosa makazi baada ya nyumba 840 kuanguka na nyingine 1,264 kupata nyufa, yakiwemo majengo 44 ya taasisi mbalimbali za umma.
Awali, akisoma hotuba ya Idd viwanjani hapo, Mhadhiri wa Kimataifa, Shehe Nurdin Kishki alisema Uislamu ni dini ya amani, hivyo amewaomba waislamu kujiepusha na vitendo vya uvunjifu wa amani yakiwemo mauaji ya watu wasiokuwa na hatia. Shehe Kishki alisema ni muhimu watu kulinda amani, kwani ikitoweka ni vigumu kuirudisha.
Alitoa mfano wa nchi za Libya na Misri, ambazo hadi sasa zimeshindwa kuirudisha. Alisema mtu yeyote anayejihusisha na vitendo vya umwagaji wa damu, kudhulumu mali za watu na kuwavunjia heshima wenzake, atakuwa ameangamia, hivyo aliwataka Watanzania hususan wakazi wa Temeke kujiepusha navyo.
"Temeke sasa inaongoza kwa matukio ya mauaji, wanaua hadi walinzi. Askari wameuawa bila hatia, jambo hili linasikitisha sana. Watu waliokuwa wanafanya kazi ya kulinda raia na mali zao wanauawa bila ya hatia,” alizungumza kwa masikitiko na kuwaomba Watanzania wajiepushe na vitendo hivyo.Pia Shehe Kishiki aliipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuonesha dhamira ya dhati ya kuwatumikia wananchi na kuwaletea maendeleo hivyo aliwaomba wananchi wawe mstari wa mbele kutoa ushirikiano ili taifa liweze kusomba mbele.
"Ndugu zangu tumepewa heshima kubwa leo kuswali Idd na Waziri Mkuu, tena amekuja hapa kwenye viwanja hivi vya Mwembe Yanga, hii inaonesha ukaribu wa viongozi wetu wakuu kwa wananchi wao hususan wa hali ya chini," alisema.
Bakwata yalia na weledi wa viongozi
Katika hatua nyingine, Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), limewataka waislamu kubadilika kwa kufanya mambo kulingana na taaluma ili kuepuka viongozi wenye mmomonyoko wa maadili na wasiojitambua.
Mufti wa Tanzania, Shehe Mkuu Abubakar Zuberi aliyasema hayo jana baada ya swala ya Idd katika Makao Makuu ya baraza hilo, Kindononi, iliyofuatiwa na Baraza la Idd lililohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali. Mufti alisema wakati umefika kwa Waislamu kubadilika, kwani wapo wanaofanya kazi kinyume na taaluma zao.
Pia alisema baraza hilo linatarajia kufungua vituo vya kutoa elimu ya kuongeza maarifa 'Nyumba ya maarifa', lengo likiwa ni kuongeza ujuzi na maarifa ya elimu ya dini katika jamii na nchi. "Uwepo wa vituo hivi utasaidia kutoa ujinga na kuwa na viongozi bora kutokana na elimu ya nafasi fulani aliyosoma na kujua kuishi na watu, awali Bakwata haikuwahi kuwa na vituo vyake vya dini vinavyojitegemea," alisema.
Aidha Mufti alitoa wito kwa Waislamu nchini kuanzisha vituo vya kufundisha elimu ya dini pamoja na masomo mengine kama lugha, ufundi. Alisema ni vema kila Mtanzania awe na uchungu na nchi yake na kujitambua kwa kufanya kazi na kuamrishana yaliyomema kwa kukataa maovu pamoja na kuvumiliana ili kuleta maendeleo.
"Tunaamrishwa uadilifu kutenda mema kama hakutakuwa na watenda mema nchi itaharibika, tuamrishane mema kufanya ibada na kufanya kazi...Mungu anapenda," alisema.
Aidha alitumia nafasi hiyo kuwaombea waliopata na maafa ya tetemeko la ardhi lililotokea katika Mikoa ya Kagera, Mara na Mwanza hivi karibuni. Kwa upande wake, Rais mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi alisema ni vema kubadilika na kujenga Bakwata mpya kwani tayari Mufti ameonesha nia. "Nataka ndugu zangu tubadilike tuanze na haya aliyozungumza Mufti kuonesha Bakwata ni nini na itafanya ni nini tumsaidie kwani kidole kimoja hakivunji chawa nia hii ni nzuri mno," alisema Mwinyi.
Alisema kila jambo jipya huanza kwa unyonge hivyo kila mtu anapaswa kuongeza nguvu ili kuleta mabadiliko. Shein akerwa na mifarakano ya Waislamu Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein, akizungumza katika Baraza la Idd, aliwataka wananchi wa Zanzibar kudumisha amani na utulivu na ili kutoa nafasi kwa Serikali kutekeleza mipango ya maendeleo ambayo katika kipindi cha awamu ya pili utekelezaji wake umeanza vizuri.
Alisema hayo katika ukumbi wa Shule ya Sekondari Mkanyageni Pemba katika hotuba ya Baraza la Iddi. Alisema katika kipindi cha miaka mitano ijayo, serikali ipo katika hatua ya kuimarisha miradi ya huduma za jamii na maendeleo, ikiwemo maji safi na salama ambapo kwa sasa utekelezaji wake umefikia asilimia 80.
Alisema mkazo zaidi katika upatikanaji wa huduma hiyo umewekwa vijijini, ambapo hadi kufikia mwaka 2020 huduma hiyo iweze kuwafikia wananchi kwa asilimia 97. Alisema kwamba utekelezaji wa miradi ya majisafi na salama, unakwenda vizuri kutokana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuungwa mkono na mashirika ya kimataifa na taasisi za fedha.
‘Wito wangu kwa wananchi wa Unguja na Pemba ni kuimarisha amani na utulivu wa nchi na watu kupendana ili kutoa nafasi kwa Serikali kutekeleza miradi yake mbalimbali ya huduma za jamii na maendeleo...tumeanza vizuri kwa kutumia nguvu zetu za ndani pamoja na kuungwa mkono na nchi washirika wa maendeleo,” alisema.
Alisema kwamba mafanikio makubwa yamefikiwa katika sekta ya afya. Kwa upande wa Kisiwa cha Pemba, vituo vya afya 27 vipo katika hatua ya mwisho kukamilika ikiwemo ujenzi mkubwa wa Hospitali ya Abdalla Mzee iliyopo Mkoani Pemba.
Alisema ujenzi wa hospitali hiyo unaofanywa kwa ushirikiano mkubwa na Serikali ya China, upo katika hatua za mwisho kukamilika na utafanya wananchi wa Pemba kupata huduma zote za afya Pemba, bila ya kusafiri kwenda nje ya kisiwa. Alisema hospitali hiyo ina sifa za hospitali ya rufaa. Kwa upande wa vituo vidogo vya afya, alitaja vituo vipya vitakavyojengwa kuwa ni Ndagoni,Tasini, Vikunguni na Chake Chake na Mkoani Pemba.
“Tumejizatiti kuhakikisha huduma za Sekta ya Afya zinakuwa bora na kuwafikia wananchi wote ikiwemo wa vijijini...hatutaki kuona mwananchi analazimika kwenda Unguja kutafuta tiba kwa kutumia gharama kubwa,” alisema.
Aidha, alisema kazi ya ujenzi wa barabara inaendelea kisiwani Pemba na lengo lake kurahisisha usafiri hadi vijijini kwa ajili ya kuimarisha Sekta ya Kilimo.
Alitaja barabara za Mgagadu hadi Kiwani yenye urefu wa kilomitar 7.6, barabara ya Kengeja hadi Ole yenye urefu wa kilomitar 35 pamoja na ile barabara ya Tasani hadi Kangani umekamilika kwa kiwango cha kifusi.
Alisema maendeleo hayo yote yatafanikiwa, kama suala la amani na utulivu litapewa kipaumbele kwa wananchi kutii sheria pamoja na viongozi wa vyama vya siasa. Dk Shein aliwakumbusha wananchi kwamba miongoni mwa mafunzo makubwa, yanayopatikana kwa Waislamu katika kipindi cha sikukuu ya Idd el Haj ni umoja na mshikamano.
Alisema ibada hiyo imewafanya mamilioni ya waislamu, kukusanyika kwa pamoja katika uwanja wa Arafat bila ya kujali uwezo wao wa kifedha au utukufu wa makabila yao.
Swala ya Idd pamoja na baraza ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa chama na serikali, akiwemo Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Iddi, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Issa Haji Ussi, Spika wa Baraza la Wawakilishi Zubeir Ali Maulid na Kadhi Mkuu wa Zanzibar Khamis Haji. Habari hii imeandikwa na Sophia Mwambe Dar na Khatib Suleiman, Zanzibar
|
0 Comments