WAKALA wa Jiolojia Tanzania (GST), umetoa ufafanuzi juu ya tetemeko lililotokea mkoani Kagera na kusema kuwa kitovu cha tetemeko hilo, kiko chini ya ardhi urefu wa kilometa 10. Aidha umetoa tahadhari kwa wananchi kwa kuzingatia na kuepuka madhara, yanayoweza kusababishwa na tetemeko la ardhi kabla ya tukio, wakati wa tukio na baada ya kutokea tukio ili kupunguza madhara yanaweza kutokea.
Katika taarifa yake jana, wakala huyo alisema kuwa tetemeko hilo lililonakiliwa na vituo vya kupimia matetemeko ya ardhi, limetokana na misuguano ya mapande makubwa ya ardhi iliyopasuliwa na mipasuko ya ardhi mithili ya mipasuko kwenye bonde la ufa.
“Tetemeko hilo lililotokea Septemba 10 mwaka huu majira ya saa 9:27, mchana kitovu chake kilikuwa kati ya latitudo 10 06’ na longitudo 31055’ eneo ambalo ni kilomita 20 Kaskazini Mashariki mwa kijiji cha Nsunga na kilomita 42 Kaskazini Magharibi mwa mji wa Bukoba, alisema Mtendaji Mkuu wa GST.
“Nguvu za mtetemeko wa ardhi wa tetemeko hilo ni 5.7 kwa kutumia skeli ya “Richter” ukubwa ambao ni wa juu sana kiasi cha kuleta madhara makubwa,” alisema Mtendaji Mkuu wa GST, Profesa Abdulkarim Mruma.
Alisema kutokana na ukubwa huo maeneo mengi ya Mkoa wa Kagera, ikijumuisha mji wa Bukoba yamepatwa na madhara makubwa ikiwa ni kusababisha vifo vya watu 16 kuharibika kwa nyumba nyingi, watu wengi kujeruhiwa kwa kuangukiwa na vifusi na kuta za nyumba.
Aidha taarifa hiyo ilisema kuwa eneo lililokumbwa na tetemeko la ardhi liko karibu na mkondo wa Magharibi wa bonde la ufa la Afrika Mashariki inakisiwa kuwa mtetemo huo ulisababishwa na kuteleza na kusuguana kwa mapande ya miamba juu ya mipasuko ya ardhi ya bonde hilo la ufa.
Aidha alisema mpaka sasa Tanzania na duniani kote, hakuna vifaa au taratibu za kuweza kutabiri utokeaji wa matetemeko ya ardhi na vifaa vyote na taratibu zote za kuratibu au kupima matetemeko ya ardhi vinapima ukubwa na tabia ya tetemeko baada ya tetemeko kutokea.
Alisema wakala huyo tayari umepeleka wataalamu katika eneo la tukio ili kuendelea kufanya utafiti wa kina juu ya tetemeko hilo na kwamba miongoni mwa vituo vya jiolojia vilivyorekodi tukio hilo la tetemeko ni kile cha Geita ambacho ndicho kilicho karibu sana na eneo la tetemeko hilo.
Mtendaji Mkuu alisema jamii inapaswa kupewa elimu ya tahadhari ili kila mmoja aelewe nini cha kufanya linapotokea tetemeko la ardhi ikiwa ni pamoja na kupata mafunzo kutoka kwa watu wa msalaba mwekundu kuhusu namna ya kuhudumia majeruhi ama wahanga na pia jeshi la zima moto ili kupata elimu kuhusu namna ya kutumia kizimamoto.
Alisema wananchi wanashauriwa kujenga nyumba bora na imara kwa kuzingatia viwango halisi vya ujenzi, kuweka misingi imara wakati wa ujenzi, kupata ushauri wa kitaalamu wa aina ya majengo yanayofaa kujengwa katika eneo husika kulingana na ardhi ya mahali hapo.
Wakati wa tetemeko mamlaka hiyo imesema kuwa wananchi wanashauriwa kukaa mahali salama kama vile sehemu ya wazi isiyo na majengo marefu, miti mirefu na miinuko mikali ya ardhi. Pia ilisema watu wanashauriwa kukaa nje ya nyumba katika sehemu za uwazi.
“Endapo tetemeko litakukuta ukiwa ndani ya nyumba unashauriwa ukae chini ya uvungu wa meza imara, ama kusimama kwenye makutano ya kuta na pia ukae mbali na madirisha na makabati ya vitabu, vyombo au fenicha ili kuepuka kuangukiwa na vitu hivyo,” ilieleza taarifa hiyo ya Profesa Mruma.
Aidha ilisema baada ya kutokea tukio la tetemeko wananchi wanashauriwa kuzima umeme katika majengo ili kuepuka kutokea kwa hitilafu ya umeme kama mitetemo itaendelea.
Pia wametakiwa kukagua majengo kwa uangalifu ili kuhakikisha kama hayakupata madhara na kama yanaweza kuendelea kutumika na ikibidi uwaita wataalamu wa majengo ili wayafanyie ukaguzi. Waathirika waomba msaada Katika hatua nyingine waathirika wa tetemeko hilo wameiomba serikali kuwasaidia kuwajenga mahema kwa ajili ya kujihifadhi, baada ya nyumba zao kuanguka kutokana na tetemeko hilo.
Mmoja wa waathirika hao, Joyce Ndukeke alisema kuwa tangu wamepatwa na janga hilo hawajapata msaada na kuwa wanachokifanya ni kujikusanya pamoja na kulala nje. Ndukeke ambaye ana watoto wanne alisema kuwa wakati tetemeko hilo likitokea alikuwepo nyumbani pamoja na watoto wake huku mumewe akiwa safarini kikazi.
"Nyumba zetu zimeanguka hatujapata msaada, hatuna pa kulala tunalala nje na watoto, lakini sasa tuna hofu zaidi maana hata jana (Jumapili) limepita tena, tunaomba tusaidiwe kujengewa mahema maana huu ni msimu wa mvua inaweza kunyesha wakati wowote tukanyeshewa pamoja na vitu vyetu tulivyofanikiwa kuokoa vikaharibika," alisema.
Pia muathirika mwingine, Mutalemwa Emmanuel alisema kuwa kutokana na janga hilo wanaendelea kuogopa hata kwenda kutafuta vyumba vya kuishi katika nyumba nyingine maana nyumba nyingi zina nyufa na kutokana na tetemeko kupita kwa mara nyingine, wanahofia hata nyumba hizo zinaweza kuanguka.
Alisema hata kwa wale ambao nyumba zao bado zimesisimama hawawezi kwenda kuomba hifadhi humo maana nyingi zina nyufa, tetemeko limepita tena mara mbili baada ya lile la Jumamosi ingawa ni kwa kiwango kidogo si kubwa kama la kwanza, kwa hiyo wanahofia na nyumba zenye nyufa zinaweza kuangua. Alimwomba Rais John Magufuli kuwasaidia kupata msaada wa haraka angalau kuwapatia mahema ya kuishi maana sasa wanalala nje.
Wakati wananchi hao wakitoa malalamiko hayo ya kutopata msaada wowote, Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Deodatus Kinawiro aliwataka wananchi hao kuwa na subira kidogo maana serikali inaendelea kufanya kila jitihada ili kuhakikisha wanapata msaada wa haraka.
"Sasa imeundwa kamati ya kufuatilia wananchi waliopatwa na janga hilo, ili kujua hasara iliyotokana na tetemeko hilo lakini pia kubaini misaada ya haraka inayohitajika kwa kila mmoja, tunaendelea na vikao lakini katika wilaya yangu tunakadiria watu zaidi ya 3,000 ndiyo hawana makazi," alisema.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Meja Jenerali mstaafu Salum Kijuu alisema kuwa hakuna vifo vilivyoongezeka, na kwamba majeruhi waliolazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wamepungua kutoka 253 hadi 61. Kuhusu dawa na vifaa tiba vingine vinavyohitajika alisema hakuna upungufu na kuwa huduma zinaendelea kutolewa kwa majeruhi wote.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kagera, Costansia Buhiye alisema kuwa watu hao wanahangaika sana kwani wanalala nje kwahiyo ni vizuru serikali kwa kushirikana na wadau mbalimbali na taasisi wakatoa msaada huo wa halaka ili kuondoa adha hiyo.
Pia aliwashauri wananchi na wadau mbalimbali kujitokeza kuchangia damu katika hospitali ya rufaa ili kuifanya benki ya damu kuwa na damu ya kutosha kwani majeruhi wanahitaji damu na kwamba viongozi wa chama hicho wamejitoa kwa ajili ya kuchangia damu katika Hospitali ya Mkoa huo pamoja na wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Omumwani ambayo inamilikiwa na Jumuiya ya Wazazi ya CCM.
|
0 Comments