Marekani na Urusi zimekubaliana mpango unaolenga kumaliza vita nchini Syria na kuanza mchakato wa mpito wa kisiasa.
Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani , John Kerry, anasema mpango huo utahusisha usitishwaji wa vita kwa kipindi cha siku saba mfululizo kote nchini Syria, kuanzia jumatatu.
Bwana Kerry anasema mpango huo unatoa mwelekeo bora zaidi kuliko mapendekezo mengine ambayo yashawahi kutolewa, na iwapo utatekelezwa na pande zote mbili, basi utatoa nafasi ya majadiliano kuhusu mustakabali wa kisiasa nchini Syria.
Waziri wa mambo ya kigeni wa Urusi , Sergei Lavrov, amesema mpango huo ni muhimu na halisi, na kuongeza kwamba tayari, Rais wa Syria Bashar al assad amejuzwa kuhusu mpango huo, na kutakiwa kuufanikisha.
Maafikiano hayo ni yepi?
John Kerry anasema baadhi ya mambo muhimu katika mpango huo ni kwamba vikosi vya serikali ya Syria havitaruhusiwa kuendesha oparesheni za angani katika maeneo ya waasi wa upinzani wanaoungwa mkono na serikali ya Marekani.
Amesema kwamba swala hilo huenda litakabadilisha hali ya vita ilivyo sasa, kwa kuzuia mashambulizi ya mabomu yasiyobagua na kupunguza vifo vya raia.
Vikosi vya serikali na upinzani vitahitajika kufungua barabara zinazoelekea mji uliozingirwa, Allepo, na kwamba mashirika ya msaada yaruhusiwe kuingia mjini humo bila kudhibitiwa.
Kerry pia amesema kwamba iwapo vita vitapunguzwa kwa kipindi kirefu kote nchini Syria, basi Urusi na Marekani watashirikiana kuvamia Islamic State na kundi la Nusra Front.
0 Comments