WABUNGE wametaka mara baada ya kupitishwa Muswada wa Sheria ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali ya Mwaka 2016 ambao pamoja na mambo mengine utaiwezesha maabara hiyo ifanye uchunguzi unaohusisha matumizi ya teknolojia ya vinasaba, ikiwamo uhalali wa mzazi kwa mtoto, serikali ihakikishe inatunga kanuni mapema na kutenga bajeti ya kutosha ili sheria ianze kazi mara moja.
Wakichangia muswada huo juzi jioni wabunge hao kwa nyakati tofauti walisema muswada huo umekuja kwa wakati na itawezesha Mkemia Mkuu kufanya kazi kwa ufanisi.
Mbunge wa Nzega, Hussein Bashe (CCM) akichangia muswada huo kwanza alishauri mkemia mkuu apewe muda wa kazi wa miaka mitano hadi 10 ili afanye kazi yake kwa ufanisi.
“Naomba pia serikali sheria hii itakapopita mara moja serikali iweke kanuni ili ianze kazi, tumezoea hapa tunachangia na kupitisha sheria halafu makabrasha yanakwenda kuwekwa kwenye makabati hakuna utekelezaji,” alisema Bashe.
Alitaka pia serikali kutenga bajeti kwa ajili ya maabara ya mkemia mkuu pamoja na kuwalipa wanafunzi wa kemia watakaokuwa wakifika kwa ajili ya mafunzo ya vitendo kabla ya kuhitimu na kuongeza kuwa maabara hiyo ni eneo muhimu la kimkakati nchini.
Mbunge wa Bunda Vijijini, Boniface Getere (CCM) alitaka maabara ya mkemia mkuu ipewe ruzuku ili watu wasio na uwezo wa kulipia vipimo wapimwe bure.
Mbunge kutoka Baraza la Wawakilishi, Jaku Hashim Ayoub (CCM), alisema mkemia mkuu ana majukumu mengi na nyeti hivyo anapaswa kuwekewa bajeti ya kutosha kwa ajili ya kuendesha shughuli zake na kununua vitendea kazi.
“Nchi nzima hii mashine ya ya kupima vinasaba vya binadamu (DNA) iko moja tu na mashine moja ni karibu milioni saba, mimi naona sasa kwa sheria hii mkemia mkuu atakuwa na uwezo wa kufanya kazi kwa uhuru na ufanisi, aongezewe bajeti, zinunuliwe mashine mpya hata sita haraka,” alisema.
Alisema idadi ya watumishi 192 kwa mkemia mkuu ni ndogo, hivyo waajiriwe haraka watumishi wapya angalau wafike hata 400 ili kuwezesha ofisi ya mkemia mkuu kufanya kazi kwa ufanisi na haraka zaidi.
Katika maoni na ushauri wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Muswada wa Sheria ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali Mwaka 2016 yaliyowasilishwa na Faustine Ndugulile, ilishauri mara tu baada ya kupitishwa sheria mamlaka iwezeshwe kibajeti ili kuongeza mashine na vitendea kazi vingine ili viendane na kazi na jukumu iliyopewa.
Kamati hiyo pia ilishauri serikali kuhakikisha inatunga kanuni mapema ili sheria iweze kuanza kufanya kazi mapema, lakini pia ilitaka serikali ihakikishe inatoa kibali cha ajira ya watumishi 100 ili mamlaka iwe na watumishi wa kutosha na wenye sifa zinazotakiwa kutekeleza majukumu kwa ufanisi.
|
0 Comments