SIKU moja baada ya Rais John Magufuli kutoa siku saba kwa wadaiwa wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), wawe wamelipa madeni yao, shirika hilo limeendelea kupigilia msumari kauli hiyo na kuwataka wadaiwa wake kuhakikisha wanalipa kabla hawajachukuliwa hatua.
Aidha, limesema kabla ya kauli hiyo ya Rais Magufuli tayari walishatoa notisi kwa wadeni wake za kuwashinikiza kulipa madeni yao, kabla ya kutolewa vitu vyao nje.
Juzi, Dk Magufuli alitoa siku saba kwa taasisi zote za serikali zinazodaiwa malimbikizo ya kodi na NHC, kuhakikisha zinalipa madeni yao, vinginevyo mali zao zitatolewa nje.
Pia amemtaka Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, Nehemia Mchechu kutomuogopa mtu yeyote, awe Rais, Waziri, CCM, Chadema au kiongozi yeyote wa serikali, endapo hajalipa pango lake la nyumba, atolewe nje mali zake.
Akizungumza na gazeti hili jana, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano NHC, Suzan Omari alisema wameizingatia kauli hiyo ya Raisi na zitakapokamilika siku hizo saba, watachukuwa hatua kwa wote wanaohusika.
“Labda niseme tu kauli ya rais haijaharibu notisi ambazo tumezitoa kwa wadeni wetu, kila mmoja aliye na notisi anatakiwa kulipa na baada ya siku hizo saba tutaingia kwenye hatua nyingine,” alisema Omari ambaye alibainisha kuwa makao makuu hawakuwa na taarifa kama wapo wadeni waliolipa jana baada ya tamko la Rais Magufuli. Pia aliwataka wananchi kuacha kutafsiri vibaya kutolewa kwa mali za Mwenyekiti wa Taifa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe kutokana na deni lake na kusema kuwa alitolewa kutokana na notisi yake kuisha.
“Watu wanatafsiri vibaya, kwanza sisi hatukumlenga Mbowe, ila tulilenga ofisi kama mdaiwa wetu, notisi yake iliisha siku ile na ndio tukachukua hatua ya kutoa nje vitu vya ofisi hiyo na ni vyema watanzania watambue kuwa wadaiwa ni wengi na tutaendelea kuwachukulia hatua kama tulizochukua kila baada ya notisi ya mtu kuisha,” alisema.
Hivi karibuni, Mchechu alitoa mwezi mmoja kwa kampuni 29 za taasisi mbalimbali za serikali, zilizokwepa kulipa madeni yake kwa shirika hilo la nyumba la Taifa.
Mchechu alisema mbali na taasisi hizo za serikali, kuna watu binafsi wanaodaiwa akiwamo Mbowe, ambaye hivi karibuni mali zake zilitolewa nje kwa kushindwa kulipa deni lake. Mbowe anayeendesha Mbowe Hotels and Club Bilicanas iliyoko maeneo ya Posta, Dar es Salaam, anadaiwa zaidi ya Sh bilioni 1.1.
Miongoni mwa taasisi hizo zinazoongoza kudaiwa na NHC madeni ambayo yamefikia zaidi ya Sh bilioni tisa ni Ofisi ya Rais inayodaiwa zaidi ya Sh milioni 10 na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano inayodaiwa zaidi ya Sh bilioni mbili.
Taasisi nyingine ni Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo inayodaiwa zaidi ya Sh bilioni moja; Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inadaiwa zaidi ya Sh bilioni moja; Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki inadaiwa Sh milioni 613 na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora inadaiwa Sh milioni 360.
|
0 Comments