SHAHIDI wa 19 katika kesi ya utakatishaji fedha na wizi wa kutumia mfumo wa mtandao wa kibenki wa Sh bilioni saba, inayowakabili wafanyakazi 13 wa benki ya Exim tawi la Arusha,Thadeus Madawe (37), amesema ushahidi wa risiti za benki waliupata kutoka kwa kampuni za utalii zilizolipa benki kwa ajili ya kupata huduma ya utalii ndani Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA).

Madawe amesema mahakamani leo wakati akiongozwa kutoa ushahidi na Mwanasheria Mwandamizi wa Serikali, Poul Kaduchi mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Arusha na Arumeru, Deusdedit Kamugisha.
Amesema, NCAA iliomba malipo ya risiti za benki kwa kampuni hizo za kitalii baada ya kubaini kuwa karatasi ya kuonesha kuweka na kutoa fedha benki ya Mamlaka hiyo, akaunti ya dola ya shirika hilo na kitabu cha mizania ya malipo zinatofautiana na bila ya kupata karatasi ya kuweka fedha hizo wasingeweza kubaini wizi huo.
Madae amesema, kampuni za kitalii zilitoa ushirikiano na ziliwasilisha baadhi ya karatasi za kuweka fedha kwa uongozi wa NCAA na walipofanya uchunguzi ndipo walipobaini baadhi ya dola 790,000 hazikuingia katika akaunti ya shirika hilo.
Amesema hayo yote yalifanyika kwa kushirikiana na jeshi la polisi Arusha na makao makuu Dar es Salaam na timu yake ya uchunguzi na nyaraka zote kukabidhi polisi katika ofisi ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (RCO). Kesi hiyo inatarajiwa kuendelea tena leo na shahidi wa 21 katika kesi hiyo atatoa ushahidi wake.
Watuhumiwa hao kwa nyakati tofauti kati ya mwaka 2011 hadi 2012, walifanikisha wizi huo kwa kuziibia kampuni mbalimbali za utalii na mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro kupitia kugushi nyaraka za akaunti ya dola na fedha za kitanzania na mfumo wa malipo ya kadi.
Mshitakiwa wa kwanza katika kesi hiyo ni Bimal Gondalia Gomes (34) ambaye alikuwa Meneja wa Exim, tawi la Arusha, Lilian Mgaya (33), Livistone Mwakiyaba(36),Joyce Kimaro (36), Daud Mosha.
Wengine ni Doroth Tigana (50),Evans Kashebo(40), Tuntufe Agrey (32),Joseph Meck(34) ,Janes Massawe (32), Christophe Lyimo(34), Gervas Lubuva ambaye si mfanyakazi wa benki ya Exim na Deodet Chacha (35).