|
WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, ameliagiza Baraza la Famasia nchini kuanza kazi ya kuhakiki vyeti vya wafamasia ili kudhibiti na kuwaondoa wasio na sifa ya kufanya kazi hiyo kwenye maduka ya dawa.
Pia ameliagiza baraza hilo, kuwachukulia hatua kali za kinidhamu na kisheria, ikiwemo kuwafutia usajili wafamasia wanaokiuka kanuni na taratibu za baraza hilo, ambao wamekuwa wakijihusisha na vitendo vya upotevu wa dawa na uuzaji wa dawa na vifaa tiba vya Serikali.
Ummy aliyasema hayo jana mjini Dodoma, katika kikao na Bodi ya Baraza la Wafamasia nchini, ambapo alikemea utaratibu uliojitokeza hivi karibuni wa kutaka kuifanya biashara ya dawa kuwa sawa na biashara nyingine za kawaida za maduka ya nguo, jambo ambalo halikubaliki.
Ameliagiza baraza hilo kufanya operesheni nchi nzima kukagua maduka yote ya dawa ili kubaini upungufu uliopo, kisha kuchukua hatua kali dhidi ya wale watakao gundulika kufanya biashara hiyo bila kufuata taratibu na aliagiza baraza hilo liendelee kupambana na watoa huduma ya dawa wasio na sifa na wanaotengeneza vyeti bandia vya wafamasia.
Ummy ameelekeza kuwa baraza hilo, linatakiwa kuangalia mgongano wa kimaslahi hasa pale ambapo mfamasia wa wilaya, anatuhumiwa kumiliki maduka ya dawa mawili hadi matatu ndani ya halmashauri anayofanyia kazi na akalitaka litoe msukumo kuboresha mafunzo na elimu ili kupata watalaamu na watendaji wenye uwezo.
Akitoa taarifa ya Utendaji Msajili wa Baraza la Famasia, Elizabeth Shekalaghe alieleza kuwa zipo changamoto wà nazokumbana nazo katika kutekeleza majukumu yao, ikiwamo ya maduka mengi ya kuuza dawa, kuendesha biashara hiyo, bila ya kuwa na vibali vya biashara pia kuwepo kwa wauza dawa wasio na sifa ya kufanya shuguli hiyo.
Mwenyekiti wa Bodi ya Baraza la Famasia, Legu Mhangwa, alisema kuwa, baraza hilo limekuwa likifanya kazi kwa kuzingatia sheria ili kufikia malengo liliyojiwekea na kuahidi kuyafanyia kazi maelekezo waliyopewa na waziri.
0 Comments