SERIKALI ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli imesema iko imara, haijalala na wala haijashindwa kuongoza nchi na kwamba imejipanga kuiongoza Tanzania kuelekea mafanikio makubwa ya kiuchumi.
Hayo yalisemwa bungeni mjini hapa jana na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipokuwa akijibu swali ya Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Hai kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
"Serikali haijashindwa kuongoza nchi. Nataka niwahakikishieni waheshimiwa wabunge na wananchi wote kwamba tutaongoza nchi hii kwa mafanikio makubwa na kazi hiyo imeanza kwa marekebisho makubwa kwa maeneo ambayo tunadhani yatafanya Taifa hili liweze kupata mafanikio makubwa,” alisema na kushangiliwa.
Kauli ya Waziri Mkuu ilikuja baada ya Mbowe kutaka kufahamu serikali ina mkakati gani wa kunusuru mdororo wa uchumi, unaoinyemelea nchi.
Mbowe akijenga hoja yake, alidai hali ya uchumi nchini imeshuka na kwa mujibu wa taarifa za Benki Kuu ya Tanzania (BoT), uagizaji wa bidhaa kutoka nje ya nchi, uuzaji wa bidhaa nje ya nchi vimepungua, kama ilivyo kwa sekta ya ujenzi, hali aliyosema inaashiria kudorora kwa uchumi.
Alihoji pia kupungua kwa idadi ya mizigo inayopitia Bandari ya Dar es Salaam.
Akijibu, Waziri Mkuu alisema pamoja na Mbowe kutaja viashiria vya kiuchumi, serikali haiwezi kulizungumzia hilo bila ya kufanyika kwa tathmini, huku akisisitiza kamwe serikali haitalala ili kuhakikisha uchumi wa nchi unakua.
Akizungumzia kupungua kwa mizigo katika Bandari ya Dar es Salaam, alisema si rahisi kupata takwimu halisi kujua, lakini inalifanyia kazi jambo hilo na kwamba Bunge litajulishwa.
Hata hivyo, alisisitiza kupungua kwa mizigo si suala la Tanzania pekee, akisema alikutana na wafanyabiashara maarufu wa usafirishaji wa majini duniani kutoka nchini Malaysia, waliosema usafirishaji kwa njia hiyo umeshuka duniani kote, sababu kubwa ikielezwa ni kushuka kwa bei ya mafuta na gesi.
Aidha, kwa upande wa Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, alisema sababu kubwa ya kupungua kwa wasafirishaji wa mizigo kutoka nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Rwanda, Burundi na Zambia ulikuwa na sababu za msingi, lakini pia za mpito.
Alitolea mfano DRC na Zambia zilikabiliwa na vuguvugu la kisiasa kueleka katika uchaguzi, hali iliyochangia usafirishaji wa mizigo katika nchi hizo kupungua. Hata hivyo, alisema tayari wafanyabiashara wa Rwanda na DRC wameihakikishia serikali kwamba mizigo yao yote itakuwa inapitia Bandari ya Dar es Salaam hasa kutokana na kuwapo kwa mkakati wa pamoja wa ujenzi wa reli ya kisasa inayoanzia Dar es Salaam-Tabora - Isaka.
Kutokana na uhakika wa kupokea mizigo ya Rwanda na DRC, alisema kasi ya uchumi itazidi kupaa, kwani nchi hizo zitachangia kuing’arisha Bandari ya Dar es Salaam. Kauli ya Waziri Mkuu, Majaliwa inaungwa mkono na takwimu mbalimbali za kiuchumi nchini ambapo Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) zinaonesha pamoja na changamoto mbalimbali hali ya uchumi iko salama.
Kwa upande wa TRA, takwimu za makusanyo kuanzia Novemba mwaka jana tangu Rais Magufuli alipoingia madarakani zinaonesha kuwa viashiria mbalimbali vya uchumi imara vimeendelea kuwa katika uwiano mzuri ikiwemo makusanyo ya mwezi ya kodi ambayo hayajawahi kushuka chini ya asilimia 90 ya lengo lililowekwa.
Takwimu hizo pia zinaonesha kuwa katika kipindi cha mwaka huu wa Bajeti, ulioanzia Julai, 2016 makusanyo ya Serikali yamekuwa yakipanda kutoka Sh 1,069,458,000.50 Julai hadi Sh 1,158,573,000.66 Agosti mwaka huu.
Wachambuzi zaidi wa uchumi wanasema, kauli ya Waziri Mkuu, Majaliwa pia inabebwa na ukweli kwamba ikilinganishwa muelekeo wa mapato ya Serikali kwa kipindi kama hiki mwaka jana, Serikali ya Magufuli, inafanya vyema kiuchumi. Wakati takwimu zinaonesha kuwa makusanyo ya Julai na Agosti 2015, yalikuwa ni Sh bilioni 925.38 na Sh bilioni 923.31, makusanyo ya kipindi kama hicho mwaka huu yamefikia Sh trilioni 1.158.
Kwa upande wa nchi kuaminika duniani, wataalamu wanasema uchumi wa Tanzania bado unaaminika sana. “Hata hili la kukua kwa Deni la Taifa ambalo wengi wanadhani ni jambo baya kiuhalisia ni ishara ya kuaminika kwa nchi na kwamba inaweza kuendelea kukopesheka kwa ajili ya miradi ya maendeleo,” alisema Profesa Haji Semboja.
Waziri Mkuu pia alisema serikali itahakikisha inaendelea kuimarisha amani na ulinzi kwenye maeneo yote nchini na kwamba vyombo vya dola viko macho.
“Watu wote wanaojihusisha na vitendo vya uhalifu yakiwemo mauaji watakamatwa popote walipo na kuchukuliwa hatua za kisheria,” alisema na kuwataka Watanzania kufanya shughuli zao bila ya hofu yoyote, kwani nchi iko salama.
Alisema licha ya serikali kusikitishwa na mauaji ya watu wasio na hatia kuanzia ya mkoani Tanga, Mwanza na hivi karibuni Mbande, Dar es Salaam na Vikindu, Mkuranga mkoani Pwani wilayani, wananchi wasiwe na hofu kwani wahusika wote watakamatwa na kufikishwa katika vyombo vya dola.
|
0 Comments