SERIKALI imebaini kuwa asilimia kubwa ya madini aina ya tanzanite na dhahabu yanatoroshwa nchini na wanawake ambao huyavaa kwenye maeneo tofauti mwilini na kusema ni mapambo hivyo wanapopita kwenye mashine za ukaguzi katika viwanja vya ndege huwa vigumu kubaini kama ni utoroshaji.
Kutokana na hali hiyo, serikali imejipanga kudhibiti sonara mbalimbali nchini zinazotengeneza mapambo ya madini hayo kwa kuwa imebainika wizi mkubwa unafanywa na wao kwa kivuli cha kutengeneza mapambo.

Hayo yalibainishwa juzi jioni na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo wakati akizungumza kwenye kipindi cha ‘TUNATEKELEZA’ kinachorushwa na Kituo cha Televisheni cha Taifa (TBC1).
“Unakuta mama, amevaa madhahabu, bangili nyingi na vito vingine unadhani amejipamba kumbe ndio anatorosha madini yetu nje hivyo, huwezi kumzuia, sasa tumejipanga kushughulika na sonara, tumegundua wizi mkubwa wa madini hayo unafanywa huko,” alisema Profesa Muhongo.
Alisema pamoja na serikali kupunguza kasi ya wizi wa madini hayo, bado tatizo linaendelea na kwamba hivi karibuni Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA) ulikamata tani 10 za madini zilizokuwa zikitoroshwa nje.
Alisema juhudi za serikali tangu mwaka 2012 zimekuwa zikifanywa za kuanzisha madawati kwenye viwanja vya ndege nchini yanayofuatilia na kudhibiti utoroshwaji wa madini na tangu kuanza kwa kazi kwa madawati hayo wamefanikiwa kudhibiti kiasi kikubwa cha madini.
Wakati Profesa Muhongo akisema hayo, Kamishna wa Madini nchini, Paul Masanja alizungumzia utoroshwaji wa madini hayo nje katika maeneo tofauti na kusema kiwango kinachotoroshwa ni kikubwa.
Alisema takwimu za mwaka 2013 zinaonesha kuwa asilimia 80 ya madini ya tanzanite yalisafirishwa nje ya nchi kwa njia za panya na kuzinufaisha nchi za Kenya ambayo ilisafirisha na kuuza tanzanite yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 100.

India nayo iliuza tanzanite yenye thamani ya Dola milioni 300 wakati Tanzania inayozalisha madini hayo ikiambulia Dola milioni 38 kutokana na mauzo ya nje ya madini hayo.
Akizungumzia sekta ya madini kwa ujumla, Profesa Muhongo alisema inawezekana kwa siku za nyuma nchi ilifanya makosa, lakini ni vyema wakaangalia hali ya sasa na baadaye ili kusifanywe makosa tena.
“Tuwe wakweli, inawezekana hapo zamani tulifanya makosa kwenye madini, lakini tunachofanya sasa ni kuangalia tulipo na baadaye ili tusifanye tena makosa, tunataka sekta hii ichangie mapato ya taifa kwa asilimia 10 kutoka asilimia 3.5 ya sasa,” alisema.
Alisema serikali inachofanya hivi sasa ni kusaidia Watanzania ambao ni wachimbaji wadogo wadogo wa madini ili wawe wa kati, kwa kuwawezesha zana za kisasa za uchimbaji ili wakuze uchumi wao na taifa badala ya kutegemea wachimbaji wakubwa kutoka nje.
Katika kutekeleza hilo, alisema Septemba 15, mwaka huu wachimbaji wadogo wataanza kupewa ruzuku ya vifaa hadi vya Sh milioni 200 kwa ajili ya kuwawezesha kuchimba kisasa na kuongeza mapato.
Kuhusu usambazaji wa umeme, Waziri Muhongo alisema kwa mwaka huu wa fedha 2016/17 bajeti ya ndani pamoja na wahisani kutoka nje ya nchi ya kusambaza umeme vijijini imefika Sh trilioni moja na hiyo ni hatua kubwa itakayofanya mapinduzi kwenye maeneo mengi vijijini.
“Tumepitisha kwenye Bunge la Bajeti la mwaka huu, tumetenga shilingi bilioni 535.4 sawa na ongezeko la asilimia 50 haya ni mafanikio ya REA II, na wahisani nje wametupa fedha na jumla ya bajeti kwa mwaka huu ya umeme vijijini ni trilioni moja,” alisema na kuongeza kuwa katika kutekeleza mradi wa umeme vijijini wa REA III, idadi ya wananchi watakaopata umeme itaongezeka.
Kuhusu sekta ya gesi, alisema hivi sasa asilimia 45 hadi 50 ya umeme unaozalishwa nchini unatokana na gesi, jambo lililookoa fedha nyingi ambazo zingetumika kuzalisha umeme wa mafuta.
Alisema faida za gesi nchini ni nyingi na kwamba matumizi ya gesi katika kuzalisha umeme yamesaidia kuwapunguzia wananchi mzigo kwa kufuta tozo ya huduma kwenye manunuzi ya umeme na pia kwa wateja wapya wanaoomba kuunganishiwa umeme kwa mara ya kwanza, hawalipi fedha za fomu ya maombi.
Akizungumzia kwa mara nyingine mabadiliko ndani ya Shirika la Umeme (Tanesco), Profesa Muhongo alisema ni lazima lifanyiwe mabadiliko makubwa ili liende na kasi ya Serikali ya Awamu ya Tano.
“Sitaki kuzungumza mengi hapa kuhusu Tanesco, lakini kwa muundo wake na utendaji wake na huku tunakokwenda lazima lifanyiwe mabadiliko makubwa sana, itakuwa Tanesco inayochapa kazi kwa kasi yetu, isiyo na rushwa, wizi, uzembe iko njiani inakuja hiyo,” alisema.
Akizungumzia mafuta na gesi alisema ili nchi iwe ya uchumi wa kati, taifa linategemea uchumi wa gesi na viwanda na kwa kuanza kiwanda cha mbolea kitajengwa Kilwa mkoani Lindi kwa ushirikiano baina ya Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) na majadiliano yako kwenye hatua nzuri na wadau wakiwemo Ujerumani, Denmark na Pakistan.
Baada ya ujenzi wake kukamilika, alisema kwa siku kitazalisha mbolea tani 3,850 na uzalishaji huo utasaidia kuboresha sekta ya kilimo na hivyo kuisaidia pia sekta ya viwanda.