BAADHI ya majeruhi wa tetemeko la ardhi lililotokea mkoani Kagera, waliopata majeraha makubwa na matatizo ya mifupa, wanaweza kupelekwa Dar es Salaam katika Taasisi ya Mifupa ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MOI) kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi na kupatiwa matibabu zaidi.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alisema kuwa wizara imejipanga na kushiriki ipasavyo, hivyo waathirika wa tetemeko hilo watakaobanika kupata matatizo ya mifupa itabidi wasafirishwe na kwenda kupatiwa matatibu katika taasisi hiyo.
Ummy alibainisha hayo wakati wa kuhitimishwa mjadala wa Muswada wa Sheria wa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu 2016 na Muswada wa Sheria wa Usimamizi wa Wataalamu wa Kemia 2016.
Alisema nia ya serikali ni kuona majeruhi wanapata matibabu haraka ili waweze kupona na kutoa pole kwa watu wote walioathirika na tukio hilo, lililotokea Septemba 10, mwaka huu mkoani humo na katika mikoa ya jirani ya Mwanza, Geita na Shinyanga. Hadi Jumanne serikali imesema jumla ya watu 17 ndio wamekufa kutokana na tetemeko hilo na wengine 252 kujeruhiwa.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene alisema hayo wakati alipokuwa anasoma kauli ya serikali bungeni mjini hapa kwa niaba ya Waziri Mkuu.
Simbachawene alisema tukio hilo lilitokea majira ya saa tisa alasiri na ukubwa wake ulikuwa wa kiwango cha 5.7 katika vipimo vya Richter.
Alisema majeruhi waliolazwa katika hospitali mbalimbali za mkoani humo ni 169, waliotibiwa na kuruhusiwa kurudi nyumbani ni 83 ambapo jumla yao ni majeruhi 252.
Alisema nyumba za makazi zilizoanguka ni 840 na nyumba za makazi zenye nyufa ni 1,264 wakati majengo ya taasisi yaliyoripotiwa kuanguka ama kupata nyufa ni 44.