Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala, Mohammed Mchengerwa
KAMATI ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala imekataa mapendekezo ya kufanyia marekebisho Sheria ya Leseni za Uchukuzi ya mwaka 1973 yenye lengo la kuongeza kiwango cha adhabu ya faini hadi kufikia asilimia 500 kwa watakaokiuka masharti ya leseni hizo.
Mapendekezo hayo yaliwasilishwa mbele ya kamati hiyo mjini Dodoma jana na Mamlaka ya Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra).

Baada ya kuyakataa mapendekezo hayo, kamati hiyo imetoa muda wa siku mbili kwa Sumatra kuhakikisha inawasilisha mbele ya kamati hiyo mapendekezo yanayokubalika.
Sumatra inapendekeza kuongeza kiwango cha adhabu ya faini kutoka kati ya Sh 10,000 na Sh 50,000 hadi Sh 200,000 na 500,000 kwa watoa huduma za uchukuzi, watakaokiuka masharti ya leseni zao.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mohammed Mchengerwa alisema mapendekezo hayo, yatazidi kuwaongezea mzigo Watanzania badala ya kuwasaidia. Alisema kiwango hicho cha faini kubwa, kamwe hakitazuia tatizo la ajali za barabarani, zaidi ya kuongeza ukubwa wa tatizo la rushwa.
“Serikali ya Awamu ya Tano imejipanga kuwasaidia wananchi, lakini mapendekezo haya yatazidi kuwaongezea mzigo kwa sababu kiwango cha faini hizi kama kitapitishwa, watoa huduma za uchukuzi watahamishia hasara yao kwa wananchi,” alisisitiza.
Aliitaka mamlaka hiyo, kwenda kuyafanyia kazi tena mapendekezo hayo kwa kuwasiliana na Mwanasheria Mkuu wa Serikali na kuwasilisha viwango vya faini vinavyokubalika. Mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo, Joseph Mhagama ambaye pia ni mbunge wa Madaba, alisema mapendekezo hayo hayana nyongeza yoyote, itakayoisaidia serikali katika kudhibiti tatizo la ajali barabarani.
“Kwa sasa serikali imeweka nguvu zake katika kupunguza ajali za barabarani, lakini kiwango cha faini hizi hakina uhusiano wowote na jitihada hizi zaidi ya kuiongezea Sumatra mapato na kuwapa mzigo walipa kodi,” alisema.
Naye Mbunge wa Mlalo, Rashid Shangazi alisema mamlaka hiyo ilitakiwa itoe kipaumbele zaidi katika kuwaelimisha watoa huduma na watumiaji wa huduma hizo za uchukuzi juu ya haki na wajibu wao; na si kuwaongezea kiwango cha faini.
Aidha, alihoji mamlaka hiyo imetumia kigezo gani hadi kuongeza kiwango hicho cha faini na kufikia asilimia 500.
“Kwa kuwa kazi ya Sumatra ni kudhibiti watoa huduma hawa, ningetegemea wangekuja na mapendekezo ya adhabu ya kifungo jela na si kuongeza faini,” alisisitiza.
Alipendekeza kiwango cha mwisho cha adhabu ya faini kwa wanaokiuka masharti ya leseni kuwa ni Sh 100,000. Kwa upande wake, Mbunge wa Arumeru, Olemeiseyeki Gibson alisema kiwango hicho cha adhabu ya faini ni cha juu na kitachangia kuongeza zaidi tatizo la rushwa.
Akiwasilisha mapendekezo ya mamlaka hiyo mbele ya Kamati hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Sumatra, Gilliard Ngewe alisema mapendekezo ya marekebisho ya sheria hiyo, yamelenga kuondoa kuiboresha zaidi sheria hiyo ya leseni za uchukuzi.
Alisema marekebisho hayo, pia yatasaidia mamlaka hizo kuendana na mahitaji ya sasa hasa katika eneo la adhabu ya faini, hali itakayopunguza kiwango kikubwa cha kukiukwa kwa masharti ya leseni hizo za uchukuzi.