WATU sita wanaotuhumiwa kuwa majambazi hatari, wameuawa katika majibizano ya risasi na Polisi katika eneo la Mbezi kwa Yusuf Makondeni katika Manispaa ya Kinondoni, Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Kaimu Kamanda wa Kanda Maalumu, Naibu Kamishna wa Polisi, Lucas Mkondya, watuhumiwa hao waliuawa katika majibizano ya risasi na Kikosi Maalumu cha Kupambana na Ujambazi wa Kutumia Silaha.

Mkondya alisema wamepata taarifa kutoka kwa raia mwema kuwa kuna kikundi cha watu wenye silaha, wamejipanga kufanya tukio la ujambazi kwa kutumia silaha kwa mfanyabiashara aliyekuwa akitoka Benki ya Diamond Trust Bank (DTB), tawi la Barabara ya Nyerere, ambaye angepita katika barabara hiyo kwenda mkoani Morogoro.
Alisema baada ya kupata taarifa hizo, polisi waliweka mtego na majambazi hao wakitumia gari aina ya Toyota Carina lenye namba za usajili T970 DGZ rangi ya fedha, walionekana wakilifukuza gari la mfanyabiashara huyo, kisha kulipita na kumsimamisha kwa nguvu.
“Majambazi wawili wakiwa na bastola walishuka katika gari hilo. Baada ya kugundua kuwa wameingia kwenye mtego wa polisi, walianza kufyatua risasi kwa askari wakitumia bastola na wenzao waliokuwa wamejaa kwenye gari yao walianza kushuka huku wakifyatua risasi kuelekea kwa askari,” alisema Kaimu Kamanda Mkondya.
Alisema kutokana na hali hiyo, askari walianza kujibu mashambulizi na kuwaua majambazi hao na baada ya upekuzi, zilipatikana bastola mbili, moja ya kijeshi aina ya Chinese ikiwa na risasi moja ndani ya kasha la risasi; na nyingine aina ya Browning ikiwa imefutwa namba zake na maganda sita ya risasi yaliyookotwa katika eneo la tukio.
Miili ya watuhumiwa hao imehifadhiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na upelelezi unaendelea ili kubaini mtandao mzima wa ujambazi.
Katika tukio lingine la Oktoba 17, mwaka huu saa 2:00 usiku katika maeneo ya Tegeta Masaiti, watuhumiwa watatu wa ujambazi wakiwa wamepakizana kwenye pikipiki aina ya Fekon yenye namba MC370 BEY, wakiwa na bunduki aina ya shotgun iliyokatwa mtutu na kitako, walivamia duka la Abdallah Juma (46), mkazi wa Tegeta na kupora fedha za mauzo na kuiba vocha za mitandao mbalimbali, ambazo thamani yake haijafahamika.
“Polisi baada ya kupata taarifa waliwafukuza majambazi hao, walipoona wanakaribiwa na askari, walitupa chini begi walilokuwa nalo na kutelekeza pikipiki yao kisha kukimbia, begi lilipopekuliwa lilipatikana na silaha hiyo,” alisema.
Aidha, wananchi wenye hasira waliendelea kuwakimbiza majambazi hao na kumuua mmoja huku wengine wakikimbilia kusikojulikana. Katika hatua nyingine, Mkondya alisema wamekamata watuhumiwa wawili wa unyang’anyi kwa kutumia nguvu wakiwa na pikipiki moja na funguo bandia 75.
Alisema watuhumiwa hao, Ally Makwega (53) mkazi wa Tandika na Fabian Greyson (39) mkazi wa Yombo walikamatwa Oktoba 4, mwaka huu saa 6:00 usiku.
Watuhumiwa hao walikamatwa wakiwa na pikipiki yenye namba MC292 AMD aina ya Boxer rangi nyekundu, wanayoitumia kufanya uhalifu, wakiwa na funguo bandia 75 ambazo huzitumia katika kuvunja nyumba mbalimbali ya biashara za kulala wageni, maghala ya kuhifadhia bidhaa na maduka.
Baada ya watuhumiwa hao kuhojiwa, walikiri kuhusika na matukio mbalimbali ya uvunjaji wa maghala na kuiba katika mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro na Dodoma.
Watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani baada ya upelelezi kukamilika. Mkoani Tanga, Anna Makange anaripoti kuwa mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka mitano ambaye ni mkazi wa Kata ya Sindeni wilayani Handeni, ameuawa kwa risasi na mjomba wake mwenye umri wa miaka sita wakati walipokuwa wakichezea bunduki aina ya gobori nyumbani kwao.
Tukio hilo la kusikitisha, limetokea katika Kijiji cha Kweditilibe, wakati watoto hao ambao ni ndugu wa familia moja walipokuwa wakichezea bunduki hiyo inayomilikiwa na baba wa mtoto aliyeuawa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Benedict Wakulyamba alithibitisha jana kutokea kwa mauaji hayo na kusema yalifanyika Oktoba 17, mwaka huu saa 12:30 jioni.
“Siku hiyo ya tukio, mmiliki wa gobori hilo ambaye ndiye baba mzazi wa mtoto aliyeuawa, inadaiwa alikuwa ameliweka hapo nyumbani na ndipo hao watoto wakaingia na kulichukua kwa ajili ya kulitumia wakati wakicheza nje na ndipo mtoto ambaye inadaiwa ni mjomba wa marehemu alipomfyatulia risasi mwenzake na kusababisha kifo hicho,” alisema Kamanda Wakulyamba.
Kamanda Wakulyamba alisema mmiliki wa gobori hilo ambaye ni mzazi wa marehemu, anaendelea kutafutwa na polisi kwa kuwa hakuweza kupatikana baada ya mauaji hayo na kwamba uchunguzi kuhusu tukio hilo bado unaendelea.
Katika tukio jingine lililotokea kwenye Kata ya Mazinde wilayani Korogwe, mfugaji Maliki Kilimbo (18) amejeruhiwa kwenye goti lake la mguu wa kushoto kwa kupigwa risasi wakati akilisha mifugo ndani ya shamba la mwekezaji. Kamanda Wakulyamba alisema uhalifu huo ulifanyika Oktoba 17, mwaka huu saa 12:30 jioni wakati mfugaji huyo alipoingiza mifugo kwenye shamba la mkonge, mali ya Kampuni ya Toronto.
“Kilimbo alijeruhiwa kwa risasi ya bunduki aina ya gobori na mlinzi wa Kampuni ya Toronto aitwae Benjamin Mgiriki.... upelelezi kuhusu tukio hili bado unaendelea,” alisema.
Mkoani Rukwa, Peti Siyame anaripoti kuwa wananchi katika Kijiji cha Legezamwendo wilayani Sumbawanga, wamemuua kwa kumkata kata kwa mapanga mkazi wa kijiji cha Mkusi, Erick Nkrukizi (30) na kuuchoma moto mwili wake baada ya kumkamata akitaka kuumua mwanamke, Nkundi Masingija.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, George Kyando alisema mauaji hayo yalifanyika Oktoba 19, mwaka huu, saa mbili usiku, baada ya kundi la watu hao, kufanya mauaji hayo. Watu hao hawajafahamika. Uchunguzi wa polisi unaendelea ili kuwabaini na kuwafikisha kwenye vyombo vya dola ili sheria ichukue mkondo wake.