Rehema Mwilu
KIU ya Rehema Mwilu (16), ni kusoma na anatamani apate fursa hiyo ili atimize ndoto zake za kuwa mwalimu.
Lakini ni mwaka wa tatu sasa yuko nyumbani, akisubiri bahati yake huenda msamaria, akajitokeza ili kumwezesha kwenda shule kusoma. Rehema ni binti anayeishi Mtoni Kijichi, Dar es Salaam. Alihitimu elimu ya msingi katika Shule ya Msingi Mtoni Kijichi mwaka 2013 na kufaulu.

Alichaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari ya Kibada. Hata hivyo, hakuweza kuripoti shuleni kutokana na ugumu wa maisha, uliosababisha aendelee kukaa nyumbani hadi leo.
Ni mtoto wa tatu kuzaliwa akiwa msichana pekee kati ya watoto watano wa familia ya Ally Mwilu (47) na mama Hadija Makongo (39). Ndugu zake Rehema ni Hussein Mwilu ambaye ni mtoto wa kwanza, Nashiri Mwilu wa pili, Selemani wa nne ambaye anasoma elimu ya msingi na Baraka ni kitinda mimba, yeye bado ni mdogo.
Kati ya ndugu zake hao wawili wakubwa, hawakuchaguliwa kuendelea na masomo ya sekondari, baada ya kuhitimu elimu ya msingi , na hivi sasa kila mmoja anajitegemea na kufanya shughuli ndogo zinazowasaidia kujikimu na wakati mwingine kusaidia familia yao.
Kwa miaka yote mitatu, binti huyo amekuwa akiwaza kuwa ipo siku atasoma, na hiyo ni moja na sababu ya yeye kukataa kuozwa na wazazi wake, kwa kuwa bado anaamini kuwa iko siku atasoma, na elimu hiyo kuwa mkombozi wa maisha yake.
Mkasa wa binti huyo ni funzo kwa wasichana wengine wenye kiu ya elimu kwa sababu, pamoja na ugumu wa maisha hajakata tamaa wala kujiingiza kwenye makundi yasiyofaa, bali ameendelea kujitunza akiamini iko siku atasoma na kuwa mwalimu.
Sauti ya Rehema
Siku moja Nashiri, kaka yake Rehema, alimpelekea mama yake magazeti mbalimbali ayasome, kwa kuwa hupenda kusoma magazeti. Na miongoni mwa magazeti hayo, kulikuwa na gazeti la HabariLeo.
Baada ya Rehema kuyaona, alipekua na kubahatika kuona mawasiliano ya viongozi wa Kampuni ya Magazeti ya Serikali ya TSN, kwenye gazeti la HabariLeo, kisha akaamua kupiga namba za simu zilizoandikwa, akiamini kuwa kiu yake ya elimu itafanikiwa.
“Nilifungua magazeti tofauti, ila nilipofungua gazeti la HabariLeo niliona kuna sehemu zimeandikwa namba za simu mbalimbali za viongozi, nilipiga namba mojawapo ya Voda, ila nikakata kwa sababu nilijua sitaweza kuongea kwa kirefu itaisha salio kwa sababu ninatumia mtandao wa Tigo, hivyo niliamua kupiga namba nyingine ya Tigo na kufanikiwa kuzungumza na mmoja wa viongozi”, alisema Rehema.
Baada ya kuwasiliana na mmoja wa viongozi wa Kampuni hii, Rehema alielekezwa mahali ofisi zilipo na kufika kisha kuelezea maisha yake, na ndipo hatua ya kutafuta ukweli wa jambo hilo, ikaanza kwa kufuatilia kuanzia shule ya msingi aliyosoma hadi shule ya sekondari aliyopangiwa na nyumbani kwao na hata kwenye Ofisi ya Serikali ya Mtaa wake.
Rehema alisema baada ya kuhitimu masomo mwaka 2013, alifaulu kujiunga na kidato cha kwanza, ila hakuweza kuripoti shuleni kwa sababu ya hali duni ya wazazi wake na huo ukawa mwanzo wa yeye kukaa nyumbani hadi leo.
“Nilimaliza elimu ya msingi mwaka 2013, nikachaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza ila sikuweza kwenda shule kwa sababu wazazi wangu hawana uwezo na shule ilikuwa mbali, ila mimi nataka kusoma sitaki kuolewa na nilikataa mchumba kwa sababu ndoto zangu ni elimu kwanza”, alisema Rehema.
Akielezea jinsi alivyokataa kuozwa, Rehema alisema, baada ya kukaa nyumbani mwa muda, alitokea mwanamume aliyezungumza na wazazi wake na kupeleka barua ya posa na wazazi wakamtaka Rehema aridhie kuolewa kwa sababu hana pa kwenda.
“Alikuja mtu nyumbani na wazazi wanasema kaleta barua ya posa hivyo nikubali kuolewa, ila nilikataa na kusema ninataka kusoma, na hapo ndipo wazazi wangu wakakasirika na kuniambia shauri yangu nitajijua mwenyewe, ila sikukata tamaa ninajua iko siku nitasoma”, alisema Rehema.
Safari ya kuusaka ukweli
Maelezo ya Rehema yalinifanya nifunge safari pamoja na Rehema hadi Shule ya Msingi Mtoni Kijichi na kujitambulisha, kisha kueleza lengo la safari yangu, maelezo yaliyowaridhisha walimu na kufanikiwa kuzungumza na Mwalimu wa Taaluma shuleni hapo, Mary Kivyiro.
Mwalimu Kivyiro alimhoji Rehema maswali machache na Rehema aliyajibu kwa kujiamini, huku mmoja wa walimu aliyemfundisha Rehema akitokea na kumchangamkia. Baada ya mahojiano hayo, Mwalimu Kivyiro aliangalia kwenye kumbukumbu za shule na kuthibitisha kuwa ni kweli Rehema alisoma shuleni hapo na alichaguliwa kujiunga na elimu ya sekondari Kibada.
“Ni kweli Rehema Ally Mwilu alikuwa mwanafunzi wetu aliyemaliza mwaka 2013 na namba yake ni PS 0206054/255 alikuwa miongoni mwa wanafunzi 196 waliochaguliwa kijiunga na kidato cha kwanza mwaka 2014, sasa kama hakwenda kuripoti shuleni sisi hatukupewa taarifa”, alisema Mwalimu Kivyiro na kuongeza… … ila kama angerudi kusema wazazi wameshindwa kumpeleka shule wakati ule ule alipochaguliwa, uongozi wa shule ungemsaidia kwa kutoa taarifa kwa Ofisa Elimu, ambaye angemsaidia, ila ndio kwanza unatuambia habari hizi leo, wenzake wako kidato cha tatu sasa”, alisema Mwalimu Kivyiro.
Safari ya kuelekea Sekondari ya Kibada
Baada ya kuthibitishiwa hayo, safari ya kuelekea Shule ya Sekondari Kibada ilifuata na kufanikiwa kuzungumza na Kaimu Mkuu wa Shule, Fulgence Daudi ambaye alithibitisha kuwa Rehema Mwilu alichaguliwa shuleni hapo, ila taarifa zinaonesha hakuripoti shuleni.
‘Ni kweli tuna jina la Rehema Ally Mwilu ambaye alipangiwa hapa kujiunga kidato cha kwanza mwaka 2014, ila hakuripoti na kwa sababu zisizofahamika na kwa mujibu wa taratibu kama ameshindwa kuhudhuria ndani ya siku 90, huwa anajiondoa kuwa mwanafunzi kwa sababu hatukuwa na taarifa zake”, alisema Mwalimu Daudi.
Hata hivyo, alisema kinachowezekana kumsaidia binti huyo ni yeye kuandika barua kwa Mkurugenzi wa Manispaa husika, barua ipitie kwa Ofisa Elimu Sekondari kupitia kwa mkuu wa shule alikochaguliwa, na ieleze nia yake ya kuomba kusoma na aweke viambatanisho vya sababu iliyomzuia awali ashindwe kusoma, na kama kuna sababu nyingine aziandike.
“Barua hiyo ipitie shuleni ili mkuu wa shule ya msingi aliyosoma, athibitishe kuchaguliwa kwa mwanafunzi huyo na kisha itaenda ngazi husika, na pia kama ni tatizo la kifamilia na ameshindwa kusoma mbali, kwenye barua iandikwe na aombe shule ya karibu itakayomsaidia yeye na changamoto za familia yake’’, alisema Mwalimu Daudi.
Changamoto za elimu
Mwalimu Daudi alisema bado kuna changamoto kwa baadhi ya wazazi na walezi kwenye maeneo mbalimbali, yakiwemo ya Pwani, kutokuwa na mwamko wa elimu kwa watoto wao na hupenda zaidi kuthamini sherehe za mila na tamaduni, ambazo wakati mwingine huwalazimu wanafunzi kuacha masomo na kuhudhuria.
Hodi nyumbani kwa akina Rehema
Gazeti hili lilifika pia nyumbani kwa familia ya Rehema eneo la Mtoni Kijichi na kuzungumza na wazazi wake, ambao walisema tatizo kubwa lililokwamisha elimu ya binti yao ni umasikini.
“Tulipenda sana binti yetu asome, ila umasikini ndio ulinikwamisha, ingekuwa ni kipindi hiki angeweza kusoma kwa sababu hakuna ada serikali inagharimia , ila natamani asome na yeye anapenda ila hatuna jinsi na mama yake ni mgonjwa , hivyo familia ya watoto sita ninaihudumia mwenyewe kwa kuuza mkaa”, alisema baba yake Rehema, Mwilu.
Mwilu anauza mkaa, ambapo hutumia baiskeli yake kufuata gunia moja au magunia mawili wilayani Mkuranga na kisha kurejea kuuza, ili kupata fedha za kuendeshea familia kwa sababu mkewe ni mgonjwa wa tumbo na hawezi kufanya kazi, kwa sababu mwili umevimba na inakuwa tabu kutembea.
Mama yake mzazi Rehema, Hadija alisema awali baada ya mtoto wake kuchaguliwa, alifanya juhudi za kuomba uhamisho kupitia kwa ofisi ya diwani, ila hakufanikiwa na alipofika shuleni Kibada, alifafanuliwa gharama za ada na michango mingine inayofikia Sh 180,000.
“Baada ya kuambiwa gharama hizo, kwa kweli sikuwa na jinsi, kwa sababu ni fedha nyingi na familia yangu haina uwezo, ilibidi tu Rehema abaki nyumbani”, alisema Hadija, mama mzazi wa Rehema, ambaye pia alikiri familia ilipokea barua ya posa ila binti yao alikataa. “Ni kweli mchumba alijitokeza na binti yetu alikataa, na sisi hatukumlazimisha”, alisema Hadija mama mzazi wa Rehema.
Posa ya Rehema
Akielezea ilivyokuwa hiyo posa, Rehema alisema yeye anataka kusoma na kwamba wazazi wake walimtaka aolewe baada ya mchumba kuleta barua ya posa nyumbani ambayo wazazi waliiridhia.
“Ililetwa barua ya posa na wazazi wakaridhia kwa kumtaka huyo mchumba aje anione, na alipokuja mimi sikukubali kuolewa kwa sababu malengo yangu ni kusoma na sio kuolewa kwa umri huu”, alisema Rehema.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa anena Naye Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Butiama anakoishi Rehema, Haji Mgaya alisema anamfahamu binti huyo na aliuliza iwapo anasoma na kuambiwa anajifunza ufundi wa kushona, ila hakuambiwa kama binti huyo alitaka kuozwa.
Msaada wako
Binti Rehema ni jasiri na kitendo cha yeye kupiga simu kuomba msaada wa kusomeshwa, kinaonesha kiu aliyonayo ndani ya moyo wake, kwani pamoja na yeye kupenda shule, wenzake aliomaliza nao elimu ya msingi hivi sasa wako kidato cha tatu, na wamekuwa wakimcheka wakidhani alikataa shule, la hasha!
Ni changamoto na umasikini wa familia yake, ndivyo vimemkwamisha. Lakini, hajachelewa, unaweza kubadilisha maisha yake kwa kumsaidia Rehema atimize ndoto zake za kuwa mwalimu, ili aelimishe wengi kuhusu haki ya elimu hususan kwa mtoto wa kike. Watakaoguswa, wawasiliane na uongozi wa gazeti hili jinsi ya kumpata Rehema.