BARAZA la Madiwani Halmashauri ya Wilaya ya Igunga mkoani Tabora, limekataa kupokea taarifa ya utengenezaji wa madawati ya halmashauri hiyo na kuagiza aliyetoa taarifa ya kumdanganya Rais John Magufuli na umma aende kwenye vyombo vya habari kukanusha taarifa hizo.

Maamuzi ya madiwani hao yanafuatia taarifa ya utengenezaji wa madawati iliyotolewa na Ofisa Elimu wa Shule za Msingi wa Wilaya, Mwisungi Kigosi kwenye mkutano wa kawaida wa baraza hilo kuonesha mabadiliko ya takwimu zilizotolewa kwa Rais na walizosomewa wao.
Waliochangia hoja hiyo kwa nyakati tofauti ni baadhi ya madiwani, Charles Bomani wa Kata ya Igunga, Gedi Nkuba wa Kata ya Nguvumoja, Henry Saidi wa Kata ya Mwamala na Juliana John wa Viti Maalumu Kata ya Igunga, wote wakiwa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Walisema kutokana na taarifa hiyo kukinzana, kuwa na mkanganyiko na taarifa iliyotolewa kwa Rais ya kutokuwa vizuri, hawaipokei taarifa hiyo na wanairudisha kwenye Kamati ya Fedha wakaipitie tena na kisha kuipeleka kwenye Baraza la Madiwani.
Hata hivyo, diwani Juliana alibainisha kuwa kutokana na kuwepo kwa upungufu wa madawati, alishauri Mkaguzi wa Ndani afuatilie taarifa ya madawati hayo pamoja na tathmini ya fedha zote zilizokusanywa kwa ajili ya utengenezaji wa madawati hayo ibainike.
Diwani wa Kata ya Mwamala aliyekuwa mmoja wa wajumbe wa tume ya kufuatilia utengenezaji wa madawati, Henry Saidi amebainisha kwamba baada ya kubaini kuwepo kwa mianya ya ufujaji wa fedha za madawati ya Halmashauri ya Igunga, walishindwa kuendelea na mchakato huo wa utengenezaji wa madawati.
Ofisa Elimu wa Shule za Msingi Wilaya ya Igunga, Mwisungi Kigosi alisema hadi Septemba 21, mwaka huu, wilaya hiyo ilikuwa na upungufu wa madawati 2,232 baada ya kukarabati 725 upungufu halisi uliopo ni madawati 1,507.
Anna Nyarobi ambaye ni Diwani wa Viti Maalumu kupitia Chadema, akichangia hoja hiyo alipendekeza kwamba watu waliotoa taarifa za uongo waende kwenye vyombo vya habari na kukanusha taarifa hiyo kwa kusema kuwa taarifa waliyotoa ilikuwa ni ya uongo ili warudishe imani za wananchi kwa madiwani wao.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Igunga, Revocatus Kuuli alisema alipotembelea katika Shule ya Msingi Ganyawa alikuta wanafunzi wakiwa wanaendelea na masomo huku wakiwa wamekaa chini, hivyo alitoa ushauri kwa madiwani kuungana pamoja kwa kuendesha harambee ili tatizo la madawati litatuliwe.