NAIBU Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Edwin Ngonyani ametembelea Kivukoni upande wa Magogoni jijini Dar es Salaam na kukuta msongamano wa magari yanayosubiri kuvuka.
Kutokana na hali hiyo, ilimlazimu kwenda kutembelea pia Daraja la Nyerere ambako alikuta magari machache sana ndiyo yanayotumia daraja hilo huku magari mengi yakiwa yamejaa Feri kusubiri kuvuka kwa vivuko.

Alikutwa na gazeti hili katika daraja hilo akifanya mahojiano na wafanyakazi wa hapo kutaka kufahamu ni kwa nini watu hawatumii daraja hilo ambalo halina foleni kabisa.
"Niliamua kufanya ukaguzi wa kawaida tu, nilianzia upande wa Feri kule ambako nimeshangazwa kukuta msongamano wa magari yanayoenda Kigamboni ni mkubwa, lakini nikaja huku darajani kweupe kabisa hakuna foleni," alisema Naibu Waziri Ngonyani.
Alisema baada ya kuzungumza na wahusika katika daraja hilo, walimfahamisha kuwa kuna watu wengi pia wanaotumia daraja hilo, lakini inategemea pia na safari ya mtu yaani eneo analotokea na anakokwenda.
“Wataalamu wanasema magari yanapita mengi pia hapa darajani, wanaopita Feri ni wale wanaoona wanakoenda ni karibu zaidi na feri badala ya mzunguko wa kuja darajani, hata hivyo wananchi walilalamikia sana gharama za daraja ambapo serikali ilisema kuwa itafanyia kazi maoni yao," alisema Ngonyani.
Alisema mazungumzo yanaendelea kati ya serikali na mwekezaji aliyejenga daraja hilo, Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) ili kuona tozo hiyo inapunguzwa kwa kiasi gani.