Pembe za ndovu zilizokamatwa katika operesheni maalumu ya kusaka majangili.
RAIS John Magufuli ameagiza kikosi kazi cha kupambana na ujangili, kutafuta na kukamata watu wote wanaoua tembo, ikiwemo walioua tembo ambao pembe zao zimekamatwa Dar es Salaam.
Alisema hayo alipofanya ziara ya kushtukiza katika Ofisi za Wizara ya Maliasili na Utalii (Mpingo House), jijini Dar es Salaam kwa lengo la kufuatilia utekelezaji wa operesheni ya kukabiliana na ujangili, inayofanywa na Kikosi Kazi kilichoundwa na wizara hiyo.

Taarifa iliyotolewa na Ikulu, Dar es Salaam jana, ilisema akiwa katika ofisi hizo jana Rais Magufuli aliyekuwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Meja Jenerali mstaafu Gaudensi Milanzi alishuhudia pembe 50 za ndovu zilizokamatwa kati ya juzi na jana jijini Dar es Salaam.
Aidha, Rais Magufuli alioneshwa magari yaliyokamatwa yakiwa yamebeba pembe hizo na watuhumiwa wanane, wanaodaiwa kujihusisha na mtandao wa biashara haramu ya pembe za ndovu.
Rais aliwapongeza askari wote waliopo katika Kikosi Kazi cha kudhibiti na kupambana na biashara haramu ya pembe za ndovu pamoja na raia wema wote, wanaotoa ushirikiano katika operesheni hiyo na aliwahakikishia kuwa anatambua kazi kubwa wanayoifanya na anawaunga mkono.
“Nawapongeza sana kwa kazi nzuri mnayoifanya na ninawahakikishia kuwa ninawaunga mkono, chapeni kazi, wakamateni wote wanaojihusisha na biashara hii haramu, hakuna wa kumbakiza, awe mkubwa au nani, kamateni, wala msijali cheo chake, umri wake, dini yake, kabila lake, umaarufu wake, sheria ni msumeno.
“Watafuteni wote mpaka watu wakiona tembo wawe wanakimbia wenyewe ili tuokoe wanyama wetu ambao wanaendelea kuteketezwa. “Hapa mmekamata pembe 50 maana yake tembo 25 wameuawa, haiwezekani maliasili yetu ikawa inapotea hovyo hovyo kwa sababu ya watu wachache wenye tamaa ya kutaka utajiri wa haraka haraka,” alisisitiza Rais Magufuli.