Majeneza ya watafiti hao
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema serikali itachukua hatua kuhakikisha kuwa waliohusika na mauaji ya watafiti wa Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Selian Arusha (SARI) wanakamatwa na kufikishwa kwenye mikono ya sheria.
Amebainisha kwamba watafiti hao waliouawa jioni ya Jumamosi iliyopita katika Kijiji cha Iringa Mvumi wilayani Chamwino katika Mkoa wa Dodoma, walifika Dodoma kutokana na agizo la serikali la kufanya uchunguzi wa matetemeko ya ardhi kama yatakuwa endelevu nchini. Mbali ya hayo, amewatoa hofu wale wanaokuja Dodoma kwa ajili ya kikazi au kuwekeza kwani Dodoma ni shwari.

Waliouawa kwa kucharangwa kwa silaha kama mapanga na shoka na kisha kuchomwa moto ni Nicas Magazine aliyekuwa de reva, mtafiti Theresia Nguma (43) na kijana aliyekuwa akianza kazi ya utafiti, Jaffari Mafuru, wote kutoka SARI jijini Arusha.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mjini hapa jana, Waziri Mkuu Majaliwa alisema serikali imesikitishwa sana na tukio hilo la watumishi wa serikali kuuawa wakati wakiendelea na majukumu yao ya kazi.
Asikitishwa na vifo
“Ni jambo la kusikitisha sana tunawaombea roho zao zipumzike kwa amani, kama serikali tutachukua hatua kwa kuhakikisha waliohusika wanakamatwa na kufikishwa kwenye mikono ya sheria,” alisema na kuongeza kuwa watafiti hao walitumwa na serikali kutokana na tetemeko la ardhi lililotokea mkoani Kagera.
“Walikuja Dodoma kutoka Arusha kufuatia agizo la serikali la kufanya uchunguzi wa matetemeko ili ijulikane kama tetemeko ni endelevu,” alibainisha na kuongeza kuwa kufanyika kwa utafiti huo, serikali iliomba Wizara ya Nishati na Madini kupitia Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST) kufanyika utafiti huo, hivyo serikali kupita kwa taasisi zake iliamua kufanya uchunguzi kuhusu matetemeko hayo kama yataendelea ama la.
“Waliweka mpango kazi wapite mkoa wa kati kwenye Bonde la Ufa, walifanya kazi zao kwa siku tano siku ya sita ndipo wakakumbana na umauti. Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi,” alieleza Waziri Mkuu na kufafanua kuwa jukumu la serikali ni kuhakikisha wanaokuja Dodoma wajue Dodoma ni salama, historia ya Dodoma haioneshi kama ina matukio ya ajabu kama haya.
“Jukumu la Serikali ni kuhakikisha Dodoma ni salama, wanaokuja wataikuta Dodoma ni salama,” alisema Majaliwa ambaye alihamia mjini hapa mwishoni mwa wiki iliyopita kuanza utekelezaji wa Serikali ya Awamu ya Tano kuhamia Dodoma kuanza sasa hadi ifikapo mwaka 2020.
Makamu wa Rais alaani
Naye Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan amelaani mauaji ya watafiti wawili wa Seliani na dereva waliokuwa kazini katika Kijiji cha Iringa Mvumi, Chamwino.
Akifungua Kongamano ya 30 la Kimataifa la Wanasayansi lililoandaliwa na Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) kwenye Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam jana, Samia alisema tukio hilo ni baya na amewahakikishia watafiti wanaoshiriki kongamano hilo kuwa serikali itachukua hatua stahiki kwa watu waliofanya kitendo hicho cha kinyama ili kukomesha tabia hiyo.
“Haiwezekani hata kidogo watu kufanya mauaji hayo ya kikatili na waachwe bila kuchukuliwa hatua kali za kisheria,” alisisitiza Makamu wa Rais.
Akizungumzia masuala ya utafiti, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan amesema serikali inatambua kazi nzuri inayofanywa na watafiti hao hivyo serikali itaendelea kutoa mchango wake wa hali na mali ili kuhakikisha watafiti hao wanafanya kazi zao kwa ufanisi unaotakiwa.
Waziri ashiriki maziko Arusha Naye Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, William ole Nasha akitoa salamu za serikali wakati wa maziko ya Nguma, jana Olasit jijini Arusha, alisema msiba huu ni msiba mzito kwa serikali kwani imepoteza watafiti wake waliokuwa wakichukua sampuli za udongo kwenye maeneo mbalimbali na hatimaye wakakutana na mauti.
Alisema serikali haipo tayari kuvumilia tukio hilo na ndio maana inaendelea na uchunguzi wa tukio hilo ikiwemo kuwashikilia watu zaidi ya 43 hadi jana.
Ole Nasha alisema serikali haijawahi kupata tukio la unyonyaji damu na wala hakuna matukio hayo Tanzania na hakuna ukweli wowote juu ya tukio hilo na kutoa rai kwa wananchi kuacha tabia yakujichukulia sheria mkononi.
Alisisitiza kuwa kama wananchi au wanakijiji wana hofu ya jambo fulani ni bora kwenda polisi au uongozi wa kijiji ili kulitatua badala ya kujichukulia sheria mkononi.
“Acheni kujichukulia sheria mkononi kama mna hofu na watu nendeni sehemu husika badala ya kuwaua watu wasio na hatia na hizi tuhuma za kunyonya damu zinatoka wapi wakati katika nchi yetu hakuna mambo kama haya,” alieleza naibu waziri.
Mtoto wa marehemu kusomeshwa
Aidha, alibainisha kuwa wanaendelea kuzungumza na familia za Magazine na Mafuru kufahamu nini cha kufanya, lakini kwa familia ya Theresia, serikali itamsomesha mtoto wake wa kiume Gabriel kwa kumlipia ada katika Chuo cha Uhasibu Njiro jijini Arusha huku mtoto mwingine wa kike, Lisa serikali ikiendelea na mazungumzo na familia.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Utafiti Makao Makuu ya wizara, Dk Hussein Mansuri alisema Theresia na Magazine anawafahamu kwa kuwa ni watumishi wa Seliani na wamefanya kazi kwa zaidi ya miaka 10 sasa.
Alisema Theresia aliomba kupata safari hiyo ili apate ada ya kuwalipia watoto wake, lakini amekufa akiwa kazini hivyo kituo hicho kimepoteza watu muhimu waliojitolea kwa ajili ya kusaidia wananchi.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Gabriel Daqqro alisisitiza serikali haitawavumilia watu wanaojichukulia sheria mkononi na kutoa rai kwa wananchi wa Arusha kutii sheria, kanuni na taratibu na endapo kuna taarifa za mashaka miongoni mwa jamii inayowazunguka vipelekwe sehemu husika ili kudhibiti mauaji au uharibifu wa mali.
Paroko: Tusilipize kisasi, tusamehe
Kwa upande wake, Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Yoseph Mfanyakazi Olasiti, Boniface Mbite amewasihi waumini wa madhehebu mbalimbali kuwasamehe wale wote waliohusika na tukio la kuwaua na kuwachoma moto watafiti wa Selian.
Akizungumza katika misa ya kumuaga Theresia aliyezaliwa Oktoba 10, 1973, Paroko Mbite alisema msiba huo ni msiba mzito, lakini ni lazima kumshukuru Mungu kwa kila jambo na tukio hilo lililotokea ni la kusikitisha, lakini ikumbukwe kuwa wanadamu bila kujali tofauti za dini, kabila jinsi na vinginevyo, wote ni wanawali wa Mungu.
“Lakini licha ya kuwa wanawali wa Mungu, miongoni mwetu wapo wapumbavu na wenye busara na kila mmoja amepewa taa yake ambayo ili iwake ni lazima usali na kukubali kusamehe hata katika jambo linaloudhi kama hili lililotokea kwa wenzetu,” alisema Paroko Mbite na kuongeza: “Msilipize kisasi, serikali ipo na inafanya kazi yake tuiache ifanye kazi yake.
Tujifunze kusamehe waliohusika na tukio hili vyombo vya dola zitawachukulia sheria na lazima tutambue ya kuwa sisi wote tunapita hatuna haja ya kuhuzunika, bali tushukuru Mungu kwa hili lililotendeka hakika bwana atatenda.
” Alisisitiza kuwasamehe wote walifanya mauaji hayo ingawa ni ngumu, lakini alisema Mungu alitoa neno kuwa ni “lazima tusamehe wale wanaofanya mambo mabaya kama haya yaliyotokea.”
Marehemu Theresia amezikwa eneo la nyumbani kwake ambako ni karibu na kanisa hilo huku watu mbalimbali wakihudhuria maziko yake wakiwemo watafiti kutoka vituo mbalimbali mikoani, wafanyakazi wenzake, ndugu jamaa na marafiki.
Polisi: Acheni kujichukulia sheria mkononi
Nalo Jeshi la Polisi nchini limetoa onyo kwa wote wenye tabia ya kujichukulia sheria mkononi kuacha mara moja huku ikibainisha kuwa kuanzia Januari hadi Agosti mwaka huu, kumekuwapo na matukio 705 ya kujichukulia sheria mkononi.
“Katika siku za hivi karibuni kumeendelea kuwepo kwa vitendo na tabia ya baadhi ya wananchi kujichukulia sheria mkononi kwa kuwapiga, kuwachoma moto na kuwaua baadhi ya watu wasio na hatia pamoja na wanaoshukiwa kujihusisha na vitendo vya kihalifu jambo ambalo ni kinyume cha sheria, kanuni na taratibu za nchi.
“Mpaka sasa takwimu za makosa ya kujichukulia sheria mkononi yaliyoripotiwa katika vituo vya Polisi katika kipindi cha Januari hadi Agosti mwaka 2016 ni matukio 705.Katika matukio hayo yaliyoripotiwa, Jeshi la Polisi nchini limefanikiwa kuwakamata na kuwafikisha mahakamani watuhumiwa 393,” ilieleza taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Polisi Makao Makuu, Advera Bulimba.
“Kufuatia hali hiyo, Jeshi la Polisi nchini linatoa onyo kali kwa wote wenye tabia ya kujichukulia sheria mkononi kuacha mara moja. Aidha, kwa kuzipuuza sheria za nchi zilizopo na wakati mwingine kuzikiuka kwa makusudi na mbaya zaidi baadhi yao kufikia hatua ya kuwaua watu wasio na hatia kwa hisia. Mwananchi yeyote anapaswa kutoa taarifa kwa vyombo vya dola ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi ya mhalifu au mtu yeyote wanayemtilia mashaka katika maeneo yao,” alisema Bulimba.
“Aidha, Jeshi la Polisi nchini litaendelea kuchukua hatua kali za kisheria kwa kufuatilia na kuwakamata watu wote wanaojihusisha na tabia za kujichukulia sheria mkononi. Jeshi la Polisi linatoa wito kwa watu wote wakiwemo wenye ushawishi mkubwa katika jamii kuendelea kukemea na kutoa elimu juu ya madhara ya kujichukulia sheria mkononi na badala yake wananchi kuendelea kutii na kufuata sheria za nchi zilizopo,” iliongeza taarifa ya Bulimba.
Imeandikwa na Sifa Lubasi, Dodoma na Veronica Mheta, Arusha.