MBUNGE wa Jimbo la Kaliua, Magdalena Sakaya amepingana na hatua ya Mkuu wa Wilaya hiyo kuwahamisha wananchi wanaodaiwa wako kwenye hifadhi hadi hapo tume itakapoundwa kukamilisha uchunguzi.
Sakaya amesema hayo wakati akizungumza na wananchi katika maeneo mbalimbali ya Jimbo la Kaliua ikiwa sehemu ya ziara ya kikazi.
Hivi karibuni, Mkuu wa Wilaya ya Kaliua mkoani Tabora, Abel Busalama aliwahamisha wananchi kadhaa ambao wamedaiwa wamevamia hifadhi katika baadhi ya maeneo ya wilaya hiyo na wengi wao walikosa makazi. Hatua hiyo ilisababisha zaidi ya kaya 2,700 katika kitongoji cha Wachawaseme kata ya Igagala Namba Tisa kuishi kando ya barabara iendayo kata ya Usinge na mkoani Kigoma.
Sakaya alisema kwa sasa Serikali Kuu imeunda tume itakayokwenda kwenye maeneo ambayo yamedaiwa kuwa ni hifadhi na wananchi wakadaiwa kuvamia.
Alisema hadi sasa licha ya eneo kubwa la Kaliua asilimia 90 ni hifadhi, lakini kuna maeneo watu wameishi zaidi ya miaka 10 na kuwaondoa bila utaratibu ni kukiuka haki za binadamu.
Mbunge huyo alisema zipo shule za msingi na sekondari, zahanati ambazo nazo zimesajiliwa na kutambulika kisheria hivyo tume itakayoundwa kuja kuchunguza ndiyo itagundua upungufu huo.
Alisema “wananchi hawa walishatumika sana kisiasa kwa kuelezwa hawako kwenye hifadhi na hivyo walipewa kadi za chama(hakukitaja) wakawa wanashiriki chaguzi mbalimbali lakini leo hii wametelekezwa”.
Hata hivyo, Sakaya alikana madai ya baadhi ya viongozi na baadhi ya watendaji kudai yeye ndiyo chanzo cha wananchi kuvamia maeneo yanayodaiwa ni hifadhi na kudai wananchi hao wakati yeye anakuwa mbunge tayari walikuwa wapo.
Tayari Mkuu wa Wilaya, Busalama alishatoa agizo kwa wananchi wote waliovamia hifadhi kuondoka mara moja.
|
0 Comments